ANGALIA LIVE NEWS

Monday, April 11, 2011

Okwi aikabidhi Yanga kombe

  Ngassa `avaa` kiatu cha dhahabu
Mashabiki wa Yanga wakishangilia ubingwa wa timu yao nje ya uwanja wa Taifa jijini Dar es Salaam jana.

Penalti aliyokosa mshambuliaji wa Simba, Emmanuel Okwi, katika dakika za lala-salama, iliwafanya Simba washindwe kutetea ubingwa wao wa Ligi Kuu ya Tanzania Bara uliokwenda kwa mahasimu wao Yanga ambao waliishushia Toto African ya Mwanza kipigo kikali cha 3-0 ugenini CCM Kirumba.
Simba iliyokuwa ikiongoza kwa magoli 4-1 dhidi ya timu iliyoshuka daraja tayari ya Majimaji ya Songea kwenye Uwanja wa Taifa jijini Dar es Salaam, huku dakika zikiyoyoma, ilihitaji goli moja zaidi ili bingwa aamuliwe kwa kuangalia timu yenye magoli mengi ya kufunga kwani lingetosha kufanya uwiano wa magoli ya kufunga na kufungwa ufanane kati yake na Yanga kutokana na timu zote mbili kuwa na pointi 49.

Mkenya Jerry Santo aliangushwa ndani ya eneo la hatari katika dakika za majeruhi, lakini Okwi, ambaye alikuwa akiwania kufunga 'hat-trick', aligongesha mwamba penalti hiyo na kuinyima Simba ubingwa wake wa pili mfululizo, baada ya kuutwaa bila ya kupoteza mechi msimu uliopita.
Yanga waliokuwa na nafasi ndogo ya kutwaa ubingwa huo wakati zilipokuwa zimesalia mechi tatu, walitumia vyema makosa ya Simba kudondosha pointi nne katika mechi mbili zilizofuata dhidi ya Kagera Sugar na JKT Ruvu walizotoka sare, kwa kushinda mechi zao zote tatu dhidi ya Azam FC, African Lyon hadi ya jana dhidi ya Toto African.
Kwa ushindi wa jana mjini Mwanza, Yanga iliyofunga jumla ya magoli 32 na kufungwa 7 msimu mzima, ilitwaa ubingwa wa mwaka 2011 kwa tofauti nzuri ya magoli 25, dhidi ya 24 ya Simba iliyofunga jumla ya mabao 40 na kufungwa 16 msimu huu.
Kutokana na bingwa kusubiri matokeo ya mechi za mwisho wa msimu, mechi hizo mbili zilichezwa kwa wakati mmoja kuanzia saa 10:00 jioni na hadi mapumziko, Simba walikuwa wakiongoza kwa magoli 2-0 wakati mjini Mwanza, Yanga walikuwa wamebanwa mbavu kwa sare ya 0-0.
Simba walipata magoli yao ya mapema kupitia kwa Shija Mkina katika dakika ya saba ambaye aliunganisha vyema pasi ya Okwi na Mganda huyo akafunga goli la pili katika dakika ya 24 akiiwahi pasi fupi ya Ali Ahmed 'Shiboli' akiwa ndani ya 18.
Majimaji walipunguza goli moja kwa njia ya penalti iliyofungwa na Kassim Kilungo, kufuatia madhambi yaliyofanywa na beki wa Simba, Meshak Abel, aliyetolewa kwa kadi ya pili ya njano.
Beki wa Majimaji, Paul Ngalema alitolewa kwa kadi nyekundu katika dakika ya 53 kwa kumkwatua Okwi baada ya kunyang'anywa mpira katikati ya uwanja.
Mshambuliaji Mbwana Samatta alifunga goli la tatu kwa timu yake katika dakika ya 71 kufuatia kazi nzuri ya Okwi, na Mganda Okwi akaongeza goli la nne kwa Simba katika dakika ya 90.
Siku nzuri kwa Okwi aliyeng'aa ikageuka kuwa mbaya wakati alipokosa penalti ya dakika za majeruhi.
Mjini Mwanza mabingwa wapya, Yanga walifungua mvua ya magoli mapema baada ya kipindi cha pili kuanza kupitia kwa Nurdin Bakari aliyefungwa kwa kutumia mpira wa adhabu ndogo.
Yanga walipata goli lao la pili katika dakika ya 63 kupitia kwa Davies Mwape. Wakati mpira ukielekea ukingoni, Toto walimbadili kipa Wilbert Mweta na nafasi yake kuchukuliwa na Hussein Tade, ambaye hakuweza kuzuia goli la dakika za lala-salama la Nurdin Bakari na kuwapa Yanga ubingwa.
Mjini Morogoro, Mtibwa Sugar iliwafunga African Lyon kwa 2-0 kupitia kwa magoli ya Thomas Morris kwenye Uwanja wa Manungu.
Azam ikaibwaga Ruvu Shooting 2-1 kupitia kwa Mrisho Ngasa na John Boko. Kwa goli la jana, Ngassa alifikisha mabao 16 na kutwaa kiatu cha dhahabu akiwaacha Gaudence Mwaikimba (magoli 13) na Bocco (12)
CHANZO: NIPASHE

No comments: