ANGALIA LIVE NEWS

Monday, April 11, 2011

Unahitaji mwenzi wa kufa na kuzikana? Soma muongozo huu – 2

Karibu msomaji wangu. Nashukuru tunakutana tena leo kwenye sehemu ya pili ya makala haya. Tumshukuru Mungu kwa miujiza anayoendelea kututendea kila siku.

Wiki iliyopita nilikutaka kutambua kuwa uhusiano wa kimapenzi ni suala binafsi. Kwanza kabisa ni sanaa inayokutaka uangalie mahitaji yako mwenyewe.
 

Je, unahitaji nini kwa mtu ambaye ungependa awe mwenzi wa maisha yako? Hilo ni jambo ambalo unatakiwa utembee nalo unapokuwa kwenye hatua ya kumsaka mwandani wako.

Yale unayotaka kutoka kwa mtu ambaye unapenda awe mwenzi wa maisha yako, unapaswa kuyapa kipaumbele. Hata siku moja, usithubutu matamanio ya mwili na moyo yakupe mwongozo wa kumwona umpendaye.

Ikiwa unataka mwenye umbo namba nane, kiuno kama dondora, hizo zinapaswa kuwa alama za kukuongoza kufikia kwenye kufanya uamuzi sahihi, lakini vipi kuhusu kesho?
Tabia ni kigezo muhimu ambacho kinaweza kukufanya uishi na mwandani wako kwa muda mrefu bila kuchokana. Hivyo basi, unatakiwa kutambua alama za msingi na za nyongeza.

Wakati ukiishi kwa kuheshimu alama hizo za muhimu na zile za nyongeza, unahitaji kuwa na nidhamu binafsi. Pointi hapa ni moja kwamba inawezekana ukamkosa unayemtaka kwa sababu ya kutojiheshimu.

Utamtaka unayedhani anakufaa lakini mwisho wa mchezo atakukataa kwa sababu huna sifa njema kwenye jamii. Unaonekana mhuni, kicheche, macho juu na kadhalika, hivyo hawezi kupata ujasiri wa kuwa na wewe.

Kuna pointi tatu ambazo nilikupa wiki iliyopita. Kitu cha kwanza nilitaka utambue “Nani Mwenzi wa Maisha”, cha pili “Nani Mwenzi Wako wa Maisha”, tatu nilikutaka “Ujenge Imani”.

4. ANAKUKUBALI?
Usikubali maisha yaende mbele bila kupata jibu hili. Ni sawa na kuendelea kuinua ghorofa wakati msingi bado ni tatizo. Kuna siku jengo litakuangukia. Itakuwa hasara ya kuumiza moyo.

Bora jengo pengine uliweka bima, kwa hiyo unaweza kupata malipo ambayo yatapoza maumivu lakini mapenzi hayana bima. Yakiharibika ndiyo mwisho. Ogopa mno mapenzi kuharibika wakati mmeshapotezeana muda.

Mwanasaikolojia mmoja, huyafananisha mapenzi katika muunganiko wa wawili kama picha na fremu. Kwamba vyote vinapaswa kuwa na ukubwa sawa ili viweze kuoana.

Picha ikiwa kubwa zaidi, haiwezi kuenea kwenye fremu, kama ambavyo fremu ikiwa kubwa, picha haitapendeza. Hivyo, kujua kama anakukubali au wote mnakubaliana, ni jambo linalohitaji majibu mapema.

5. THAMANI BINAFSI
Mtu ambaye anatosha kuwa wako wa kufa na kuzikana anaonekanaje kwako? Je, ni yule ambaye unaweza kwenda naye kitandani mara tatu kwa siku au moja tu kwa wiki nzima?
Je, ni yule ambaye unaweza kuketi naye sofani, mkashikana mikono na kupiga stori za hapa na pale? Ni yule ambaye mtatoka naye mitaani kwa ajili ya matembezi, huku ngono ikiwa na nafasi ndogo katika muundo wa uhusiano wenu?

Pengine kwako mwenzi wa maisha yako ni yule mwenye uelewa mkubwa wa mambo, kiasi kwamba ukianzisha mada kuhusu sura ya nchi mnaweza kuelewana kwa sababu mtajadili pamoja kwa mapana na marefu.

Lengo la kukutaka ujiulize maswali haya ni kwamba, wewe mwenyewe ndiye unayepaswa kujua ni kwa namna gani unayatafsiri mapenzi pamoja na sura ya uhusiano wako wa kudumu.

Majibu yako unatakiwa uyaweke mbele katika kuangaza yule ambaye ungependa awe mwenzi wa maisha yako. Usithubutu kumchagua ambaye haendani na kile unachokiamini.

Itaendelea wiki ijayo.

No comments: