.jpg)
Matumaini ya Simba kusonga mbele kwenye Ligi ya Klabu Bingwa Afrika kwa rufaa dhidi ya timu ya TP Mazembe ya JK Kongo yameyeyuka baada ya shirikisho la soka la Afrika, CAF, kutojumuisha malalamiko ya matukio ya nje ya uwanja katika kikao cha 'kamati ya nidhamu' kinachokaa Afrika Kusini keshokutwa.
Kwa mujibu wa taarifa ya CAF, Bodi ya Nidhamu ya shirikisho hilo itakutana jijini Johannesburg, Afrika Kusini keshokutwa Jumanne kujadili rufaa za vyama nane vya soka vya Afrika kwa niaba ya timu za nchi hizo, na TFF si kimojawapo.
Simba ilicheza mchezo wa marudiano dhidi ya Mazembe kwenye Uwanja wa Taifa wiki mbili zilizopita chini ya pingamizi.
Kama pingamizi hilo lingekubaliwa mapema na CAF palikuwa na uwezekano wa kuchukua nafasi ya mabingwa mara mbili mfululizo hao wa Afrika katika raundi ya tatu, ya timu 16 bora.
Lakini taarifa ya CAF ilisema jana Jumamosi kuwa yatasikilizwa malalamiko nane ya uwanjani na Bodi ya Nidhamu kutoka vyama vya nchi za Algeria na Zimbabwe, Tunisia, JK Kongo, Nigeria, Angola, Msumbiji, Nigeria na Misri.
Taarifa hiyo imesema matukio ya nje ya uwanja yatajadiliwa na Kamati ya Uendeshaji wa Michezo Baina ya Klabu jijini Cairo, Misri, Mei 14 wakati Widad Casablanca inaikaribisha TP Mazembe nchini Morocco mwishoni mwa wiki hii na zitarudiana Mei 8 jijini Lubumbashi.
Timu hizo zinakutana katika raundi ya tatu ambapo mshindi ataingia robo-fainali ambayo huchezwa kwa mtindo wa ligi.
Kwa mujibu wa sheria za mashindano za CAF, hata kama pingamizi la Simba litakuja kuwa na uzito katika kikao cha kamati ya mashindano katikati ya mwezi ujao, ni Casablanca itakayosonga mbele kama itakuwa ilitolewa na Mazembe.
Mazembe iliitoa Simba kwa jumla ya mabao 6-3 baada ya kushinda 3-2 mechi hiyo ya marudiano iliyochezwa chini ya pingamizi, ikiwa ilishawafunga Wekundu wa Msimbazi 3-1 mjini Lubumbashi mwezi mmoja uliopita.
Mbali na pingamizi, Simba ilikuwa na matumaini mengine ya kusonga mbele kupitia mezani baada ya waamuzi wa Misri waliochezesha mchezo wa kwanza kudai Mazembe ilijaribu kuwahonga dola za Marekani 10,000 ili waipendelee katika mchezo wa kwanza.
Ni madai ya waamuzi hao yaliyopelekea viongozi wa Simba kuwasilisha pingamizi CAF kupitia TFF wakihofu hata mechi ya marudiano inaweza kuwa 'ilishachezwa' na Mazembe nje ya uwanja.
CHANZO: NIPASHE JUMAPILI
No comments:
Post a Comment