ANGALIA LIVE NEWS

Thursday, April 21, 2011

Shule walipokufa chekechea 4 haijasajiliwa



Image
Sehemu ya ukuta ulioanguka na kusababisha vifo vya watoto wanne wa shule ya awali ya Nia iliyopo Kimara B mjini Dar es Salaam. (Picha na Yusuf Badi)
SHULE ya chekechea waliyokuwa wakisoma watoto wanne waliokufa kwa kuangukiwa na ukuta, ni nyumba ya makazi iliyogeuzwa kuwa mradi wa shule kwa ajili ya watoto wa jirani na haijasajiliwa.

Mmiliki wa shule hiyo, Jacqueline Sarungi (42), mkazi wa Kimara B Matosa, Dar es Salaam amekiri kwamba, alikuwa katika mchakato wa kuisajili shule hiyo, huku akiwa na wanafunzi 22 wa mwanzo.

Akizungumza na gazeti hili eneo la ajali hiyo, Sarungi amesema, siku ya ajali akiwa na wanafunzi wake, alimsikia fundi akigonga ukuta na alipomuuliza alimwambia usalama upo, hivyo asihofu, lakini baadaye aliona tofali moja likiangukia upande wake.

“Nilipoona tofali limeangukia upande wangu, nilikosa amani nikatoka nje, nikamwuliza fundi akaniambia nisihofu, baadaye likafuata lingine akaendelea kuniambia nisijali,” alisema Sarungi.

Alisema, baadaye akiendelea kuwavisha watoto, akiwaandaa warudi nyumbani, wengine walipenya na kwenda kubembea na ghafla akasikia mshindo mkubwa na alipotoka nje akaona nguo zikipepea kwa juu na kupiga kelele za kuomba msaada.

Jirani wa shule hiyo, Zabibu Zuberi, alisema siku hiyo akiwa ndani, alisikia kishindo kikubwa akatoka nje akifikiri ni mabomu.

Alisema alipotoka nje, alisikia vilio na kukimbilia zilikokuwa zikitokea na alipofika eneo hilo, alikuta watoto wameangukiwa na ukuta na kupiga kelele za kuomba msaada.

Hata hivyo, alisema baadaye walijitokeza majirani na kusaidia kuopoa miili hiyo na majeruhi na kutoa taarifa Polisi.

Shuhuda mwingine wa ajali hiyo, Juma Abdallah, amesema, ukuta huo umekuwa ukiwakera majirani wa eneo hilo kwa sababu ulikuwa ukionekana dhaifu na wenye nyufa nyingi kwa kuwa ulijengwa chini ya kiwango.

Abdalla mkazi pia wa Kimara, alisema ukuta huo, ulijengwa bila nondo na uliwekwa mchanga mwingi kuliko saruji, hali iliyochangia kushindwa kuhilimi maji mengi hasa katika kipindi hiki cha mvua.

“Huu ukuta ulikuwa dhaifu sana na majirani wawili walishamfuata na kumwambia mwenye nyumba, huo ukuta ni hatari maana uko kilimani na maji yanaingia chini bila kutoka na ni hatari maana hauna nondo, unaweza kuanguka muda wowote, lakini hakusikia,” alisema.

Akizungumza jana wakati wa maziko ya Gladness Shimwela (5), mjumbe wa shina namba mbili tawi la Mji Mpya, Kimara B, Abdalla Mandwanga, alisema msiba huo umegusa wakazi wa eneo hilo kwa kuwa waliofiwa kuwa ni wa familia jirani.

Alisema mwanafunzi mwingine aliyezikwa Dar es Salaam pia ni Devotha Living ambaye alizikwa juzi na waliosafirishwa kwenda Kilimanjaro ni Ludacris Lawrence (3) na Isaack Ndosi (5), wote wa Kimara B Matosa.

Baada ya maziko hayo ambayo yalitawaliwa na vilio na simanzi kubwa, wananchi walielekea eneo la tukio na kushirikiana kuubomoa ukuta huo ambao ulikuwa umeshaweka nyufa wakihofia madhara mengine.

Mjomba wa Gladness, Dunia Somba, aliiomba Serikali kuhakikisha inaangalia ujenzi holela unaoendelea sasa kutokana na kukosa viwango na kuhatarisha maisha ya watu.

“Bila Serikali kuingilia kati, ujenzi unaoendelea sasa, hali itakuwa mbaya maana nyumba nyingi zinajengwa bila viwango, hebu angalia huu ukuta ulivyo mzito na hauna nondo walitarajia utaacha kuanguka? Ujenzi kama huu ni hatari sana,” alisema.

CHANZO:HABARI LEO

No comments: