Advertisements

Friday, April 29, 2011

Si wanawake tu, hata wanaume nao huchezewa na kuachwa!-2

SIKUKUU zimeisha sasa kazi tu! Nimeona hiyo ndiyo salamu nzuri na bora zaidi katika kuhamasishana kufanya kazi. Mimi nipo sawa kwa uwezo wa aliye juu, anayenipa pumzi ya uhai bure.

Mada inayoendelea hapa kwenye Let’s Talk About Love ni namna gani wanaume nao wanavyochezewa na kuachwa na wenzi wao wakiwa na mateso makubwa. Hii ni dhana ambayo kwa baadhi ya rafiki zangu inakuwa ngumu kidogo kuingia akilini mwao.


Kama utakumbuka, wiki iliyopita nilianza kwa kuelezea dhana yenyewe huku nikinukuu baadhi ya maneno aliyotamka msomaji mmoja aliyejitambulisha kwa jina la Moses aliyefika ofisini kwangu kwa ajili ya ushauri.

Ndugu zangu, wanaume nao wana hisia sawa na wanawake, wanapenda, wanaumizwa na wanajisikia vibaya/aibu kutoka katika uhusiano hata kama mwamuzi atakuwa ni yeye. Inawezekana hapo nimekuacha njia panda kidogo, lakini unatakiwa kufahamu kwamba, wakati mwingine mwanaume anaweza kuamua kuachana na mwanamke, si kwa kupenda, kumkomoa au kumuharibia maisha yake ila analazimika kufanya hivyo kwa ajili ya kulinda maisha yake.

Anafanya maamuzi magumu ili aweze kupisha nafasi ya mtu mwingine ambaye atajua na kuthamini mapenzi yake ya kweli, lakini wakati jambo hili linafanyika anasahau madhara ambayo yanaweza kujitokeza na hapo ndipo anapokuja kugundua kwamba amechezewa na kuachwa! Hebu twende tukaone vipengele vingine.
 
MUDA...
Wakati ni mali ndugu zangu, unajua unapokuwa na mtu kwa muda mrefu akiwa anakutegemea kwa kila kitu. Akiwa amefunga milango ya mapatina wengine, halafu ghafla unaanza vitimbi vinavyohitimishwa na kuachana, lazima utamfanya aumie!
Huyu sasa anawaza juu ya muda wake alioupoteza akiwa na wewe, akiwa ameacha mambo mengi kwa ajili yako! Inawezekana kabisa alifikia hatua ya kusitisha mipango yake mbalimbali kwa ajili yako, haya ni maumivu makubwa sana kwa mwanaume ninayemzungumzia katika makala haya.

HESHIMA HUPUNGUA
Kama ilivyo kwa wanawake, wanaume wakibadilisha sana wapenzi, wanaonekana hawana thamani katika jamii. Heshima yao hupungua na huonekana mapepe. Hapa kuna tofauti kidogo; kama ni mwanaume ambaye anajulikana wazi kuwa ana tabia za ovyo, kwake inaweza kuwa sawa.

Lakini sasa vipi kuhusu mwanaume ambaye jamii inamchukulia muungwana, mstaarabu asiye na makuu? Lazima heshima yake itingishike. Hata hivyo, siku zote mwenye kuona tatizo ni mtu mwenyewe, hivyo basi kwa mwanaume huyu ambaye namuelezea hapa, anayejiheshimu huona kama amevuliwa nguo na kukatiza Kariakoo mchana pweupe.


KUJIAMINI
Hapa pia tatizo la kujiamini huweza kutokea kwa mwanaume huyu, pamoja na kwamba amefanya maamuzi ya kukuacha yeye mwenyewe, lakini ndani ya nafsi yake anaanza kupungukiwa na kujiamini.

Mawazo yake yanaweza kwenda mbali zaidi, akihisi labda wanawake wote wanaomzungumza watakumuona mwaname katili, asiye na mapenzi ya kweli na mwenye maamuzi ya haraka. Hapa hofu yake kubwa huwa kukosa mwanamke mwingine wa kuziba nafasi ya aliyeachana naye, lakini kubwa zaidi moyo wake huwa kama umekufa ganzi, maana aliyekuwa akimpenda kwa dhati ameachana naye.

KISAIKOLOJIA
Yapo matatizo mengi kisaikolojia yanayoweza kumuumiza mwanaume huyu, mawazo mengi juu ya yaliyotokea katika uhusiano wake uliopita na jinsi ilivyokuwa hadi kuachana. Akianza kuwaza zaidi juu ya makwazo aliyokuwa akifanyiwa, ndipo matatizo yanapoongezeka.
Hapa atashindwa kufanya kazi sawa sawa, ataogopa kujichanganya, huenda akawa na mawazo mengi na wakati mwingine huamini pombe/ulevi ndiyo kitulizo chake, kumbe anakuwa ameingia kwenye moto.

KWA WANAWAKE
Kuna tatizo la wanaume kujifikiria wenyewe hasa katika hili suala la kuacha/kuachwa/kuachana kwa wapenzi. Lazima mtazamo ubadilike. Epuka kuamini kwamba mwanamke pekee ndiye ambaye anaumizwa na kuachwa.

Usifikiri kwamba maudhi unayomfanyia mwenzi wako hayamuumizi, anaumia sana kama wewe. Unatakiwa kufahamu kuwa, pamoja na kuwa mpenzi wako ameamua kukuacha si kwa kupenda au anafurahia, ana maumivu kama yako.

Naamini mada hii itabadilisha mtazamo wenu wanawake, mtaanza kuwafikiria wanaume kama binadamu sawa na ninyi. Naamini hapo hiyo dhana ya haki na usawa kwa wote itaanza kufanya kazi vizuri zaidi.

KWA WANAUME
Kuachana na mpenzi wako ni jambo linaloumiza sana, lakini kamwe usiruhusu likaingilia maisha yako. Mpenzi ambaye umemuacha leo, hasa kwa sababu za msingi asisababishe upoteze kazi yako, ukosane na marafiki, udhoofu afya n.k.

Ipo njia moja nzuri sana ya kukabiliana na tatizo la maumivu ya kuachana na mwenzi uliyempenda; jaribu kukumbuka zaidi makosa/maudhi aliyokuwa akikufanyia kuliko mema. Hiyo inaweza kuwa msaada mkubwa kwako na kukuacha salama bila kumkumbuka.

Usifikirie kuhusu jamii inayokuzunguka kuhusu itavyokuchukulia, badala yake JIFIKIRIE wewe na MAISHA yako maana ndiyo vitu pekee vyenye umuhimu mkubwa kwako. Bila shaka somo limeeleweka. Nawashukuru sana kwa kunisoma, naweka kituo kikubwa hapa, hadi wiki ijayo kwa mada nyingine nzuri zaidi. USIKOSE!

Joseph Shaluwa ni Mshauri wa Mambo ya Mapenzi ambaye anaandikia Magazeti ya Global Publishers, ameandika vitabu vya True Love na Let’s Talk About Love vilivyopo mitaani. Unaweza kumtembelea kwenye mtandao wake;www.shaluwanew.blogspot.com au jiunge naye kwenye facebook.

No comments: