Advertisements

Friday, April 29, 2011

Kama hakuridhishi mueleze, usitoke nje ya ndoa-GPL

NITAKUWA si muungwana kwa kutotanguliza salamu, ni matumaini yangu wote mu wazima wa afya njema. Tunaendelea kukumbushana mambo muhimu katika mahaba ili ufurahie mapenzi kila siku.
Nimepata maswali mengi juu ya matatizo ndani ya ndoa au ndani ya uhusiano. Imeonyesha pande zote zikifikisha lawama zao huku wakiwa tayari wamekwisha tafuta tiba mbadala kabla ya swali.


Ni matatizo gani hayo?
Moja, kukosekana uaminifu kwenye ndoa, pili ni mtu kushindwa kupatiwa penzi kamili. Katika maswali haya mwanamke mmoja alidiriki kusema kuwa anakuwa mbali na mpenzi wake na wanakuwa na muda mchache wa kukutana bado amekuwa hakidhi haja zake na kufikia hatua ya kuwa matesoni.

Siku chache anazokuwa yupo nyumbani amekuwa akimuacha njiani, wazo lake kubwa lilikuwa ni kutafuta mtu wa pembeni awe akimsaidia pale mume wake anapokuwa nje kwa kipindi cha mwezi mmoja mpaka miwili.

Kwa upande wake aliona ule ndiyo utatuzi wa tatizo lake, lakini uamuzi ulikuwa mgumu na kuomba ushauri kabla hajatekeleza kwa vitendo uamuzi wake huo. Mwanamke huyo aliamua kuweka ukweli wote kwa kusema amempata ‘kidumu’ lakini alitegemea majibu yangu.

Baada ya kumjibu moja kwa moja kwa njia ya simu na kunielewa, sasa nageukia kwako mwenye wazo kama hilo pale unapokuwa mwepesi wa kutoa uamuzi bila kuangalia hasara zake ni kubwa kuliko faida.

Pale unapoikosa haki yako ndani, unapotokewa na tatizo la mwenzio kushindwa kukufikisha au mpenzi wako kuwa mtu wa kusafiri. Kwanza napenda kukuomba uwe mvumilivu na kulilinda penzi lako, najua unakuwa kwenye hali mbaya.

Siku zote unapokuwa kwenye wakati huo jiepushe na mawazo ya ngono au kuangalia picha za aina hiyo ambazo lazima zitakupa kishawishi cha mapenzi.
Mawazo ya mtu huelekea pale unapoyaelekeza, pia moyo una haki ya kutamani lakini wewe ndiye unayetakiwa kuuzuia. Ukiuendekeza utakupeleka kubaya.

Kingine ambacho ndicho muhimu kwenye mada yetu ni kutokuwa bubu, kushindwa kumweleza ukweli mwenzako kuwa siku hizi ushibi. Unatakiwa kuwa mkweli kwa mwenzako, kumueleza jinsi unavyoteseka kwa yeye kukuacha njia panda ili utafutwe utatuzi wa tatizo hilo. Huenda yeye huamini wewe hufurahia.

Hata wewe mwanaume lazima uelewe hakuna kitu alichokifuata kwako zaidi ya mijeledi. Nani alikuambia punda au farasi anakufa kwa mijeledi? Kupigwa kwake ndiko kunakomfanya aongeze mbio.

Pamoja na kufanya kazi nzito ambazo huchosha mwili  lakini unatakiwa upate muda wa kumpanda punda wako na kumpiga mijeledi ya maana.
Usikae kimya penye tatizo, zungumza ili kuwekana wazi kila mmoja ajue kitu gani mwenzie amepunjwa hasa katika mapenzi. Ili kumnyima nafasi shetani ambaye kishawishi chake kikubwa ni wewe kutoka nje ya ndoa.

Namalizia kwa kusema hakuna suluhu ya matatizo nje ya ndoa yako zaidi ya kujidhalilisha kwani penzi la kweli limo ndani ya ndoa nje ya hapo ni kupotea njia.

Kama una wazo la kuisaliti ndoa yako jiulize mara kumi faida na hasara zake kwa jambo unalotaka kulifanya. Kila tatizo kaa chini na mwenzako mtafute suluhisho ambalo ndiyo kinga thabiti ya ndoa yenu.
Kwa hayo machache tukutane wiki ijayo.

No comments: