ANGALIA LIVE NEWS

Friday, April 29, 2011

Kodi yakwamisha matrekta ya Suma-JKT bandarini

Makontena 364 yenye matrekta ya Shirika la Uzalishaji Mali la Jeshi la Kujenga Taifa nchini (Suma-JKT), yamekwama bandarini kutokana na kudaiwa kodi mbalimbali, ikiwamo ya Mamlaka ya Mapato Tanzania (TRA).
Hali hiyo inadaiwa kusababisha kukwamisha lengo la matrekta hayo kuwafikia wakulima kabla ya msimu.

Mkurugenzi Mtendaji wa Suma JKT, Kanali Ayoub Mwang’ata, alisema hali hiyo ni moja ya changamoto zinazolikabili shirika hilo, ikiwamo ya kilimo na hivyo, kuhitaji msaada kutoka serikalini ili makontena yaweze kutolewa bandarini.
Alisema hadi sasa wamepokea jumla ya makontena 457 kutoka nchini India, lakini ni makontena 93 pekee yaliyokwishatolewa bandarini wakati 364 bado yamekwama.
Waziri wa Kilimo, Chakula na Ushirika, Profesa Jumanne Maghembe, alisema serikali itahakikisha inatoa msaada katika hilo ili kufanikisha azma ya Suma-JKT kwa wakulima nchini.
“Sisi kama serikali tutajitahidi kadri ya uwezo wetu kusaidia shirika hili kufanikisha lengo na azma waliyoiweka kwa wakulima wa nchi yetu. Hivyo, wananchi wajitokeze kuweza kununua matrekta hayo, kwani utakapopewa elimu, basi utaweza kutumia kwa uafanisi,” alisema Profesa Maghembe.
Alisema serikali imetenga dola za Marekani milioni 92 kama mkakati wa kuanza kutengeneza matrekta nchini.
CHANZO: NIPASHE

No comments: