Advertisements

Friday, April 29, 2011

Wanafunzi 1,200 Udom watimuliwa

Wanafunzi wa shahada ya kwanza 1,200 wa Chuo Kikuu cha Dodoma (Udom), katika Chuo cha Sayansi, Mawasiliano na Elimu Angavu, wamesimamishwa masomo kwa muda usiojulikana na kutakiwa kuondoka chuoni hapo kwa kile kilichoelezwa wamevunja kanuni za chuo na hivyo kutishia amani.
Akizungumza na NIPASHE, Kaimu Makamu Mkuu wa Udom, Profesa Ludovick Kinabo, alisema wanafunzi hao walikataa kuingia madarasani hata pale uongozi ulipowataka kufanya hivyo mara kadhaa.
Alisema kuwa kamati ya utendaji ya chuo itakutana Jumatatu wiki ijayo kwa ajili ya kujadili jambo hilo.

“Na hivyo hivyo, wale tuliowasimamisha kwa muda usiojulikana 27, walibainika kuwa ni vinara wa kuleta fujo chuoni,”alisema.
Alisema wanafunzi hao walianza mgomo wa kutoingia madarasani Aprili 20 mwaka huu, wakishinikiza Bodi ya Mikopo ya Elimu Juu kuwapatia Laptop.
Hata hivyo, Profesa Kinabo alisema kuwa bodi hiyo ilishawajibu kuwa hawawezi kuwakopesha Laptop (kompyuta ndogo) kwa sababu hakuna utaratibu kama huo.
“Waliambiwa kuwa labda wazazi wao wawanunulie kwa kuwa utaratibu wa bodi hiyo hauruhusu kukopeshwa Laptop lakini wao wakadai ni haki yao na kuandamana wakidai wanakwenda ofisi ya Waziri Mkuu kuwasilisha madai yao,”alisema.
Alisema ili kuhakikisha hali ya usalama katika chuo hicho, chuo hicho kimeandaa mikakati ya kuhakikisha kuwa ulinzi unaimarika.
Hata hivyo, alipoulizwa kama wameomba msaada Jeshi la Polisi, alisema chuo chenyewe kimeaandaa mikakati ya ulinzi na upo wa kutosha.
Profesa Kinabo alisema kuwa utaratibu utakaotumika ni wa kuwarudisha wanafunzi hao mmoja mmoja na kwamba wale ambao watabainika kuwa ndio vinara wa kuchochea migomo hawatawarejesha chuoni.
Kwa mujibu wa matangazo yaliyobandikwa katika mbao za matangazo, wanafunzi hao walitakiwa kukabidhi mali za chuo na kuondoka katika eneo hilo kabla ya saa 10.00 jioni jana.
Tangazo hilo lilisema kuwa mwanafuzi atakayekaidi agizo hilo atakuwa amejifukuzisha mwenyewe masomo.
NIPASHE ilishuhudia wanafunzi hao wakiwa na mabegi wakiondoka katika mabweni hayo katika muda uliopangwa.
Daladala na taksi zilijizolea abiria tele na hivyo kufanya usafiri wa kwenda Udom kuwa mgumu kwa muda wa zaidi ya saa nne tangu agizo hilo litoke.
Madereva taksi walikuwa wakitoza gharama za kati ya Sh. 13,000 hadi Sh. 15,000 kwa kila safari moja.
Baadhi ya wanafunzi walionekana katika makundi wakiwa na mabegi yao wakiondoka katika eneo la chuo hicho.
Wakizungumza na gazeti hili kwa masharti ya majina yao kutoandikwa gazetini, wanafunzi hao wamelalamikia kupewa muda mfupi kuondoka katika eneo hilo bila kujali kama wana nauli.
“Sijui tunakwenda wapi, itabidi tuendelee kukaa hapa mjini kwa kuwa hatuna nauli ya kwenda wala fedha za mikopo bado hazijatoka,”alisema mmoja wa wanafunzi.
Walisema wao waligoma kuingia darasani kushinikiza kuelezwa sababu zilizosababisha wenzao 27 kusimamishwa masomo.
“Sisi tuliandamana hadi katika ofisi za utawala tukidai tuelezwe sababu za wenzetu kusimamishwa masomo kwa maana tukikaa kimya kesho watasimamishwa wengine na hatujui ni lini atasimamishwa mwingine,” alisema mwanafunzi mmoja.
Mwanafunzi mwingine ambaye hakutaka jina lake litajwe, alisema kuwa wanasikitishwa na hatua hiyo kwani uongozi wa Chuo umeshindwa kutatua kero zao na kuongeza kuwa hatua ya kufunga kitivo hicho na kuwaamuru waondoke itawaathiri kimasomo.
Wanafunzi hao waliandamana Aprili 20 mwaka huu, hadi katika ofisi za Waziri Mkuu mjini hapa, wakidai kupatiwa fedha za mahitaji muhimu ya kitivo.
Wanadai stakabadhi za malipo yanayofanywa Bodi ya Mikopo ya Elimu ya Juu na fedha za malazi zilizozidi.
Katika siku za hivi karibuni wanafuzi wa Udom wamekuwa katika mzozo na serikali, wakidai mahitaji mbalimbali.
Mwaka jana walikuwa wanafunzi wa kwanza wa vyuo vya elimu juu kuanzisha mgomo ambao ulisambaa na kuambukiza vyuo vingine vikuu nchini.
Kutokana na mgomo huo, Waziri Mkuu MizengoPinda alifika chuoni hapo kukutana na menejimenti, na kisha aliagiza Mkaguzi Mkuu na Mdhibiti Mkuu wa Serikali (CAG) kukagua hesabu za chuo baada ya kuwapo madai kuwa mishahara ya wahadhiri ilikuwa inachakachuliwa.
Udom ni chuo kipya ambacho kilitoa mahafali ya kwanza mwaka jana na kinatarajiwa kuwa kitakapokamilika kitakuwa na uwezo wa kuchukua wanafunzi 40,000 kwa mpigo.
CHANZO: NIPASHE

No comments: