ANGALIA LIVE NEWS

Saturday, April 23, 2011

Simba wamtema rasmi Phiri

Wamnyatia kocha Mnyarwanda
  Kaseja ndani ya kikosi
Kocha Mkuu wa Simba, Patrick Phiri
Sasa ni rasmi kwamba Kocha Mkuu wa Simba, Patrick Phiri, hatakinoa kikosi cha timu hiyo kwenye msimu ujao na badala yake klabu hiyo imeanza mazungumzo na makocha watatu, akiwamo Jean Marie Ntagwabira kutoka Rwanda, anayesema wamefikia pazuri katika mazungumzo.
Kadhalika, kipa namba moja wa klabu hiyo, Juma Kaseja, ameponea tundu la sindano kutemwa katika kikosi hicho.

Habari za ndani ya klabu hiyo yenye makao makuu mtaa wa Msimbazi, hayo ni sehemu tu ya maamuzi ambayo yalifikiwa na Kamati ya Utendaji ya Klabu iliyokutana Jumatano wiki hii jijini Dar es Salaam chini ya Mwenyekiti wake, Ismail Rage.
Ingawa kulikuwa na uvumi wa kutemwa kwa Kaseja, uamuzi huo umeshindikana kwa sababu imekuwa ni vigumu kupata kipa hodari wa kuchukua nafasi yake kwa sasa, licha ya kudaiwa kuwa kiwango chake kimeshuka.
Kocha Ntagwabira anayeinoa timu ya Kiyovu ya Rwanda inayocheza ligi kuu ya Rwanda na ikiwa nafasi ya pili katika msimamo wa ligi hiyo, akizungumza na NIPASHE jana kutoka Kigali, Rwanda alisema yuko tayari kuinoa Simba na uwezo wa kuipa mafanikio anao ikiwa ni pamoja na kuiwezesha kucheza fainali ya Kombe la Shirikisho mwakani.
Alisema kuwa tayari amekwisha kutuma wasifu wake (CV) kwa uongozi wa Simba na mahitaji yake anayoyataka na kwa kiasi kikubwa wamekubaliana nao.
Ntagwabira alisema kuwa ana uwezo mkubwa wa kuipa Simba mafanikio kutokana na kuifahamu vyema soka la Tanzania na ukanda wa Afrika Mashariki na Kati baada ya kufundisha klabu ya APR, Atraco zote za Rwanda na timu yao ya taifa, Amavubi. “Kwa sasa mimi (Ntagwabira) nimepata ujuzi zaidi ya nilivyokuwa na APR, waniamini ninaweza, niko tayari kutua Dar es Salaam," alisema kocha huyo.
Aliongeza kuwa kwa sasa hana mkataba wowote na Kiyovu na anafanya kazi kutokana na mapenzi yake ya kuendeleza soka nchini kwao baada ya APR kuajiri kocha wa kigeni.
Amewataka viongozi wa Simba kutohofia kumpa ajira hiyo kwa sababu uwezo wa kuwapatia mafanikio wanayoyahitaji anao.
"Kwanza nitahakikisha Simba inachukua ubingwa wa Kombe la Kagame huko Sudan, nimeshawahi kufanya hivyo na hata kuwafunga Simba nikiwa na APR mwaka 2004, nafahamu ninachotakiwa kukifanya, ninaweza," aliongeza kocha huyo ambaye akiwa na Amavubi walifuzu fainali za Kombe la Mataifa ya Afrika mwaka 2004.
Mbali na kocha huyo, habari kutoka ndani ya klabu ya Simba zinasema kuwa jina la kocha Mganda, Moses Basena, ndilo lililopitishwa na Kamati ya Utendaji ili kuwa kocha msaidizi huku nafasi ya kocha mkuu bado ikiwa inaendelea kufanyiwa kazi.
Taarifa nyingine zinasema kwamba kikao hicho kiliamua nafasi ya kocha kwa kupiga kura jambo ambalo ni kinyume cha taratibu za kiufundi.
Leo Rage anatarajia kuzungumzia mambo mbalimbali yaliyotolewa maamuzi kwenye kikao hicho cha Kamati ya utendaji kilichofanyika Jumatano jioni.
Hata hivyo mapema mwaka huu, Rage aliwahi kutangaza kwamba klabu hiyo imeingia mkataba wa miaka miwili na kocha Phiri.
Mbali na hatma ya Kaseja kuwa wazi, wakali wengine wa timu hiyo waliokalia kuti kavu ni mshambuliaji Mussa Hassan Mgosi, Mohammed Banka (kiungo), Salum Kanoni (beki), Juma Jabu (Beki), Salim Gilla (beki).
Taarifa za ndani zinasema kuwa wacheza hao mbali ya kudaiwa kushuka kiwango, pia kuna tetesi kuwa walishiriki kwa njia moja au nyingine kuhujumu timu yao wakati Ligi Kuu Bara ikikimbilia ukingoni, hivyo kuikosesha Simba ubingwa.
Simba inakabiliwa na mashindano ya kimataifa yakiwamo ya Kombe la Kagame yatayoanza Juni mwaka huu jijini Khartoum, Sudan.
Mashindano ya Kagame mwaka huu yanatarajia kuwa na msisimko zaidi hasa kutokana na kuongezeka kwa zawadi kutoka Dola za Marekani 60,000 (Sh. milioni 90) hadi kufikia Dola za Marekani 100,000 (Sh. milioni 150).
CHANZO: NIPASHE

No comments: