
Hali ya hewa inazidi kuchafuka ndani ya Umoja wa Vijana wa CCM (UVCCM), baada ya Mjumbe wa Mkutano Mkuu wa umoja huo kuwataka viongozi wote wa juu wajiuzulu ndani ya siku 21 akidai kuwa wamewekwa madarakani na mafisadi.
Kada huyo, Augustino Matefu, aliyasema hayo jijini Dar es Salaam jana mbele ya waandishi wa habari akiushutumu uongozi huo kuwa uko kwa ajili ya kuwatumikia mafisadi watatu ambao wako katika mbio za kutafuta urais kwa mwaka 2015.
“Ndani ya UVCCM kuna mafisadi 100 ambao wanaongozwa na … ambaye amepewa ajira na mtu asiye raia wa Tanzania au raia kivuli, ambaye ni mmoja wa wezi wa rasilimali za nchi yetu ambaye ni ….,” alisema.
Kwa sababu za kimaadili hatuwezi kutaja majina ya watu hao kwa sababu jana tulishindwa kuwapata kusikia kauli zao.
Matefu alitaja pia kiongozi mwingine wa UVCCM kutoka kanda ya Kaskakani kuwa naye anatumika vibaya. “Sisi kama vijana wa mkoa wa Dar es Salaam, tunawapa siku 21 akina …. wajivue gamba ndani ya siku 90 walizopewa na chama kwa kuwa siku 90 zinafaa kwa mpangaji wa nyumba, tunataka waondoke la sivyo Dar es Salaam patakuwa hapatoshi.
“Tumechoka, hatuna ugomvi na mtu bali tunaangalia maslahi ya mbele ya chama chetu,” alisema.
Aidha, alisema viongozi wa kitaifa wa UVCCM kwa sasa, Kaimu Mwenyekiti Malisa na Katibu Mkuu Shigela wameshindwa kuwasaidia vijana walalahoi ambao ndiyo wapiga kura wakubwa huku wakiendekeza unafiki na upendeleo kwa watu wasomi. Alisema wamepeleka mapendekezo kwa chama wakieleza kuwa jumuiya yao kimuundo haiko sawa kwa kuwa viongozi wengi wameingia kwa rushwa.
Imeandikwa na Raphael Kibiriti, Zuhura Masudi na Mary Geofrey
CHANZO: NIPASHE
No comments:
Post a Comment