
NIWASHUKURU sana wadau wote wa kona hii ambao kwao siyo burudani bali ni funzo kubwa katika maisha yao ya kimapenzi. Kama wewe ndiyo kwanza umeanza kusoma leo safu hii ya Uwanja wa Huba, nakuhakikishia utakuwa umefanya uamuzi sahihi kabisa, maana hutabaki kama ulivyokuwa.
Katika ndoa wakati mwingine huwa na furaha na amani tele lakini wakati huo huo ndoa inaweza kugeuka kuwa shubiri kutokana na matatizo kadha wa kadha yanayoweza kutokea katika ndoa hiyo. Wakati mwingine inawezekana kukatokea kutokuelewana baina ya wapenzi hivyo kusabisha migogoro.
Pamoja na hayo kero za baadhi ya ndugu wa mume hasa mawifi husababisha ndoa nyingi kuwa mashakani. Huu ni ukweli ambao hakuna pa kuuficha, lakini hata hivyo naomba nisielewe vibaya, si kila wifi ni mkorofi, lakini hapa nazungumzia juu ya mafiwi wakorofi. Tupo sawa eeeh?!!
Nimeamua kuandika mada hii baada ya msomaji mmoja kunipigia simu na kunieleza jinsi mawifi zake wanavyokuwa kero katika ndoa yake kiasi kwamba sasa anatamani kutoka ndani ya ndoa hiyo.
Msomaji wangu huyo aliyesema ana umri wa miaka 35, ndoa yake bado haijapata neema ya mtoto, anahisi ipo mashakani kutokana na ndugu wa mume wake kuingilia kati wakimtukana matusi yote machafu na kumwita majina mabaya kwa sababu hajabahatika kupata mtoto.
Alisema kuwa hiyo ni ndoa yake ya pili baada ya kuachwa na mume wa kwanza aliyeishi naye kwa miaka miwili, baada ya kuona kuwa hana mtoto akafukuzwa! Mama huyo aliendelea kunisimulia kuwa mume wake hana matatizo sana na hali hiyo na anadai kuwa kupata mtoto ni majaliwa ya Mungu na bado anavuta subira lakini tatizo ni ndugu wa mume wake hasa dada zake wamekuwa wakimsonga na kumsema sana kuwa eti anajaza choo hana lolote.
Hata hivyo, alifafanua kwa kusema kuwa hajawahi kupima kuangalia kuwa kweli ni yeye mwenye matatizo au mumewe, katika hali ya kushangaza anasema kuwa alipojaribu kumwambia mumewe kuhusu kwenda kupima, alikataa na kumweleza kuwa anamtegemea Mungu.
Kwa kweli ni kisa cha kusikitisha kidogo, nilizungumza na mama huyo kwa zaidi ya dakika kumi, mwisho nilimuahidi kumshauri kwa kina gazetini. Nataka kumwambia dada yangu huyo kuwa kwa sasa kuna mambo matatu makubwa ya kufanya ili kuweza kukabiliana na hali hiyo.
Nimeamua kuandika gazetini ili marafiki zangu wengine ambao kwa namna moja ama nyingine wanakabiliwa na changamoto hiyo, waweze kupata tiba ya moja kwa moja.
Kitu cha kwanza ambacho mama huyo anaweza kufanya kuweza kukabiliana na matatizo yake ni kwenda hospitalini kwa ajili ya kufanya vipimo ili kuangalia kama ni yeye ndiye mwenye matatizo au ni mumewe, japokuwa napatwa na mashaka kidogo kwa sababu, mume wake wa kwanza pia hakuweza kupata naye mtoto.
Yote yanawezekana maana baada ya kupata majibu ya vipimo kutoka kwa daktari huenda akapata ushauri wenye kumfaa hasa kama atakuwa hajachelewa sana anaweza akapata dawa kwa ajili ya kutibu tatizo lake moja kwa moja!
Kitu cha pili ambacho anaweza kufanya, baada ya kupata majibu yake hospitalini, kama ataambiwa kuwa ni vigumu kupata tiba ya kitabibu, anaweza akafanya utaratibu wa kupata tiba za jadi (siyo ramli wala uchawi) hilo ni la kuzingatia sana, ninaposema tiba za jadi, simaanishi mambo ya kishirikina kama kupiga bao kuangalia kama amelogwa la hasha!
Katika dawa za jadi kuna zingine ambazo huenda zikamsaidia ikiwa ni kweli ataonekana kuwa na matatizo hayo. Jambo la mwisho la kufanya ni kwamba, namuomba dada yangu huyo awe na moyo wa subira, asichukulie hasira kwa haraka, kwa sababu katika ndoa huwa kuna mambo mengi ambayo hutokea yakiwemo mabaya na mazuri.
Kwa faida ya wasomaji wengine wenye matatizo kama hayo, fuatilia mfululizo ufuatao hapa chini ili uweze kujua kitu cha kufanya pindi utakapokumbwa na matatizo kama haya:
KUWA NA BUSARA
Kama nilivyotangulia katika utanguzi huo hapo juu, lazima uwe na busara na moyo wa uvumilivu ili uweze kukabiliana na tatizo hili ambalo kimsingi linaweza kuharibu kabisa ndoa. Wakati mwingine siyo lazima iwe baada ya kuishi muda mrefu na mumeo bila kupata mtoto, inawezekana akawa ana asili ya ukorofi pasipo sababu yoyote.
Mwingine anaweza akawa analala kutwa nzima bila kukusaidia kazi yoyote za hapo nyumbani halafu mumeo anapokuja jioni kutoka kazini anakuwa wa kwanza kumwambia maneno ya ajabu. Kama hutakuwa na busara unaweza ukaharibu ndoa yako kama hutaweza kutumia busara yako ipasavyo.
Hata kama amemwambia kaka yake, kuwa labda hushindi nyumbani, baada ya yeye kuondoka asubuhi kwenda kazini na maneno mengine mengi kutokana na chuki zake binafsi, unapaswa kutumia busara za hali ya juu sana. Kumbuka kuwa hao ni mtu na ndugu yake hivyo ni vigumu sana kuwachonganisha, kama ukitumia maneno makali na kujibizana na wifi yako au mumeo.
Kujibizana naye maneno makali mbele ya mumeo, inaweza kuwa chanzo cha mumeo kuamini aliyoambiwa na dada yake kuwa na ukweli fulani ndani yake.
Msikilize na utulie usiwe na makuu, lakini kama akimuuliza mbele yake unatakiwa kujibu kuwa anayosema siyo ya kweli, lakini inawezekana wifi yako akawa amepandikiza maneno hayo kwa chuki zake binafsi au inawezekana akawa anakuonea wivu jinsi mumeo anavyokununulia nguo kila kukicha akaona kuwa unapendeza wakati yeye kama dada yake hajawahi kumnunulia nguo za gharama kila wakati kama anavyofanya kwako.
Maneno yote hayo na hasira zote atakazokuwa nazo mumeo unatakiwa kumalizia chumbani! Mwache mumeo hasira zake zitulie, baada ya kuoga na kula chakula cha jioni, ataingia chumbani kwa ajili ya kupumzika, usimsumbue, mwache alale mpaka usingizi umpitie.
Hakikisha unakuwa siyo mbishi kwa lolote. Ni vigumu siku hiyo kukutaka unyumba lakini kama akihitaji, usimnyime ni haki yake, kama hataulizia mwache alale. Kama atazungumza maneno makali, usijibizane naye zaidi ya kumuomba samahani, kumbuka kuwa siku hiyo ni kwa ajili ya kuweka sawa mambo yaliyochafuliwa na wifi yako katika ndoa hivyo hupaswi kulala mtoto wa kike!
Ikifika muda wa saa nane na kuendelea unatakiwa kumuamsha na kuzungumza naye kwa lugha tamu, kabisa. Mweleze kuwa maneno ya wifi yako siyo ya kweli lakini kwa lugha nzuri na ya ushawishi ili akuelewe. Kama kuna mazingira yoyote ambayo wifi yako alikuwa ameyatengeneza yanayosababisha kutokuelewana kwenu unapaswa kuweka bayana.
Kwa kutumia lugha nzuri ni wazi kuwa mumeo atakuelewa na kukusamehe ambapo naamini kuwa usiku huo utakuwa wenye kila aina ya furaha na bashasha zilizojaa cheche za mapenzi.
Mada bado inaendelea, lakini kwa kuwa nafasi yangu ni finyu, kwa leo naweka kituo kikubwa hapa, hadi wiki ijayo tena katika sehemu ya mwisho. USIKOSE!
Joseph Shaluwa ni Mshauri wa Mambo ya Mapenzi ambaye anaandikia magazeti ya Global Publishers, kwa sasa ameandika vitabu vya True Love, Secret Love na Let’s Talk About Love vilivyopo mitaani. Unaweza kumtembelea katika mtandao wake; www.shaluwanew.blogspot.com
No comments:
Post a Comment