ANGALIA LIVE NEWS

Friday, April 1, 2011

Vigogo watajwa mtandao wa uchakachuaji mafuta

Januari Makamba
Ramadhan Semtawa na
Patricia Kimelemeta
SAKATA la uchakachuaji mafuta jana lilitikisa kikao cha Kamati ya Bunge ya Nishati na Madini na kusababisha kikao hicho kuunda kamati ndogo ya uchunguzi baada ya kuelezwa kuwa vigogo ndio wanaounda mtandao huo.

Mjadala huo ulianzia katika Kamati ya Bunge ya Fedha na Uchumi, ambako Mjumbe wa Kamati Kuu ya Chama cha Wasafirishaji Mizigo (Tatoa), Fulgance Buba, alieleza kwa undani ukubwa wa tatizo hilo na kutaja maeneo yanakoendeshwa biashara hiyo haramu.


"Vituo vikuu vya uchakachuaji mafuta kwa kiwango cha kutisha hapa nchini ni Igunga (mkoani Tabora) na Gairo(Kilosa, mkoani Morogoro)," alisema Buba na kuwaacha wabunge wakiwa wameduwaa.

Wakati Buba akiendelea kufichua siri za mtandao huo na kueleza kila hatua ya itendaji wake wa kazi, mbunge wa Bariadi Magharibi, Andrew Chenge, alisikika akisema chini chini, "wengine tumo humu humu, eee!"

Buba ambaye alionekana kuwa na dukuduku hilo kwa siku nyingi lakini alikosa jukwaa la kusemea, aliendelea kueleza kuwa ni vigumu kudhibiti tatizo hilo kwa kuwa wahusika wake ni vigogo wenye ushawishi mkubwa na ambao ni vigumu hata kutiwa mbaroni.

Kuonyesha uzito wa tatizo hilo, Buba alitoa mfano wa mkutano kati yao (Tatoa)na Mkuu wa Jeshi la Polisi Inspekta Jenerali (IGP), Said Mwema, ambao aliutumia kuwataja kwa majina vigogo hao lakini, dakika chache alipotoka nje, mmoja wao alimpigia simu na kumwambia, "sawa fitna zako nimezisikia."

Buba ambaye maelezo yake yaliamsha hisia kali kwa wabunge, alisema kitendo hicho kilimshtua lakini, kwa kuwa ni jasiri hakuogopa.

Aliongeza kwamba, taarifa hizi walizipeleka hadi Mamlaka ya Udhibiti wa Huduma za Nishati na Maji (Ewura) lakini hatua zinazochukuliwa ni ndogo.

"Tulisema sana, sasa ndiyo yakaja matukio kama ya Rwanda na gari la mheshimiwa Rais kujazwa mafuta machafu kule Moshi. Baada ya tukio mheshimiwa mmoja akatuita katika ofisi za Wizara ya Nishati na Madini na kutuambia; “ninyi mnasema sana, hebu tuelezeni, wabunge wanasubiri majibu bungeni."

Akielezea majibu walitoa, Buba alisema: "Sisi tulimwambia hivi, tuseme nini tena wakati tayari tulisema sana na kutoa hadi majina lakini, hayakufanyiwa kazi. Sasa leo gari la mheshimiwa Rais limejazwa mafuta machafu ndiyo mnastuka? Waheshimiwa hili ni tatizo kubwa la kitaifa."

Aliweka bayana kwamba, kama tatizo hilo halitafanyiwa kazi kwa haraka, mtandao huo utaua uchumi wa nchi kutokana na TRA kupoteza mabilioni ya shilingi kila mwezi.

"Hili ni janga la kitaifa kwa kweli. Mtandao ni mkubwa umesambaa nchi nzima, hivi vituo mnavyoviona njia nzima kuanzia hapa Dar es Salaam hadi Kibaha mnadhani kuna biashara kubwa, baadhi vinafanya kazi hiyo," alisisitiza.  

Kutajwa kwa mtandao huo kunakuja katika kipindi ambacho Mamlaka ya Mapato Tanzania (TRA) imekuwa ikirushiwa lawama na wadau kuwa ni sehemu ya tatizo kutokana na baadhi ya maafisa wake kuhusika na ulaji rushwa.

Akizungumza katika mkutano huo, Mwenyekiti wa Kamati hiyo, Dk Abdalla Kigoda, alisema tatizo ni kubwa lakini, akaitaka Tatoa waisaidie kamati kwa kufanya uchambuzi wa kina kuona hasara na faida ya kuondolewa kodi ya mafuta ya taa, kama inaweza kweli kupunguza tatizo hilo.

Baadaye mjadala huo ulihamia kwenye kamati ya Kamati ya Kudumu ya Bunge Nishati na Madini, ambako wajumbe walikubaliana kuunda kamati ndogo ya kuchunguza tatizo hilo linalodaiwa kuisababishia Serikali hasara ya Sh35 bilioni kwa mwezi.

Hata hivyo, ndani ya Kamati ya Nishati na Madini, TRA ilivutana na wadau baada ya kujaribu kutoa taarifa zilizodaiwa kuwa za uongo ambazo zilipingwa na wadau, baada ya kupunguza hasara inayotokana na tatizo la uchakachuaji mafuta hadi Sh25 bilioni kwa mwezi.

Mwenyekiti wa kamati hiyo, Januari Makamba, alisema kamati hiyo ndogo itafanya kazi katika kipindi cha mwezi mmoja na itawasilisha ripoti yake kwa wajumbe wa kamati yake ili waweze kuijadili kabla ya Mkutano wa Bunge la Bajeti utakaonza  Juni mwaka huu.

Makamba alifafanua kuwa, kamati hiyo itafanya kazi kwa mujibu wa sheria ikiwa ni pamoja na kuangalia chanzo cha tatizo la uchakachuaji wa mafuta kuanzia yanakotoka hadi yanapomfikia mtumiaji.

“Tatizo la uchakachuaji mafuta ni kubwa na tayari limeisababishia serikali hasara kubwa, hivyo tumepanga kuhakikisha kuwa tunalimaliza. Ili kufanikisha kazi hiyo tumeunda kamati ndogo ya kufuatilia,” alisema Makamba.
Makamba alifahamisha asilimia 10 ya ushuru wa Serikali inatokana na mafuta hayo.

Makamba alieleza kuwa kutokana na hali hiyo kamati hiyo itaanza kuangalia mfumo unaotumika wa kusafirisha mafuta, sehemu yanakohifadhiwa na maeneo mengine ili kuhakikisha kuwa wanajua chanzo cha tatizo hilo.

Kwa mujibu wa Makamba, uchakachuaji mafuta unasababisha hasara si kwa Serikali tu, bali hata watumiaji wa mafuta wakiwemo wafanyabiashara ya usafiri kutokana na kuharibikiwa magari yao na kupanda kwa gharama za uendeshaji.

Kwa mujibu wa mwenyekiti huyo, kamati iliyoundwa itaongozwa na Charles Mwijage (Muleba Kaskazini) akiwa mwenyekiti. Wajumbe wakiwa Khalfan Aeshi (Sumbawanga), Mariamu Kisangi (Viti maalum Dar es Salaam), Yusuph Nassir (Bukene), Seleman Nchambi (Kishapu) na Ally Mbarouk(Wete).

CHANZO:MWANANCHI

No comments: