Mussa Juma, Samunge
MAMIA ya watu ambao walikuwa wakisafiri kwenda katika Kijiji cha Samunge, wilayani Ngorongoro kupata kikombe cha tibaya magonjwa sugu, wanadaiwa kutumia nguvu kuvunja kizuizi cha barabara inayoingia kijijini hapo.
Hata hivyo, licha ya kufika Samunge hawataweza kupata dawa leo kutokana na tiba hiyo kusitishwa kwa siku za Ijumaa Kuu na keshokutwa ambayo ni Siku Kuu ya Pasaka.
Idadi kubwa ya watu hao, waliopo kwenye magari zaidi ya 100 ni kutoka mikoa ya Kanda ya Ziwa na nchi jirani ya Kenya, wanatuhumiwa kuvunja kizuizi cha barabarani Katika Kijiji cha Soitsambu kilichopo mpakani mwa Wilaya za Bunda na Serengeti juzi usiku.
Mkuu wa Wilaya ya Ngorongoro, Elias Wawa Lali jana alithibitisha kuvunjwa kwa kizuizi hicho na kueleza ni jambo la kusikitisha kwani huenda watu hao wakalazimika kukaa Samunge hadi Jumatatu wakati mchungaji Ambilikile Mwasapila atakapoanza kutoa tiba.
"Ni kweli wamevunja kizuizi cha barabara na kwenda Samunge, sasa hao wanajitakia shida kwani sasa watakaa hadi Jumatatu bila huduma,"alisema Lali.
Masikitiko ya Mchungaji Mwasapila
Akizungumza na Mwananchi, msaidizi wa mchungaji, Mwasapila, Fredrick Nisajile alisema mchungaji huyo amesikitishwa na watu kutozingatia taratibu na kwenda Samunge kwa nguvu.
"Tumepata taarifa watu wa kutoka Kanda ya Ziwa kuvunja kizuizi cha barabara na kuja Samunge, mchungaji amesikitishwa sana na watu hao wasiofuata taratibu,"alisema Nisajile.
Alisema kama ambavyo Mchungaji Mwasapila alitangaza, leo hakutakuwa na tiba na kwamba hata dawa hazitachemshwa kabisa hadi kesho Jumamosi na Jumapili ya Pasaka pia hakutakuwa na tiba.
"Watu wanapaswa kufuata taratibu, mchungaji alitangaza watu wasije huku kwani Ijumaa Kuu na Pasaka hatafanya kazi, sasa wamekuja tena kwa wingi kupitia njia za panya, mchungaji hatatoa huduma siku hizi,"alisema Nisajile.
Alisema mchungaji wakati wote amekuwa akiomba taratibu zilizowekwa zifuatwe na suala la kusitisha huduma alitangaza mapema.
"Leo (jana) hata dawa ya kesho hatuchemshi na hii inamaanisha kesho (leo) kutakuwa hakuna huduma hapa tunaomba watu waelewe hivyo,"alisema Nisajile.
Katibu Tawala wa Wilaya ya Bunda, Selevine Lalika alisema jana kuwa juzi jioni alipata taarifa za kuwapo magari eneo la kizuizi cha Bunda, lakini walipewa taarifa ya kusitishwa safari.
"Sina taarifa kamili kama walipita, ila ni kweli kulikuwa na magari kwenye kizuizi na huko maeneo ya Ikoma ila watu wa hifadhi ya Serengeti nao walizuia,"alisema Lalika.
Alisema magari ambayo yalianza jana mchana kuingia Samunge, yatakuwa yamepita njia za panya na sio katika vituo ambavyo vimekuwa vikitumika.
CHANZO:MWANANCHI
No comments:
Post a Comment