Avishwa jezi iliyoandikwa Aden Rage

Mshambuliaji wa kimataifa kutoka Ghana, Keneth Asamoah, aliwasili jana nchini na kuahidi kuipatia Yanga mafanikio katika msimu ujao wa Ligi Kuu ya Tanzania Bara na michuano ya Ligi ya Klabu Bingwa Afrika ambayo Yanga itashiriki mwakani baada ya hivi karibuni kutwaa taji la ligi kuu ya Bara.
Asamoah ambaye aliwahi kuja nchini kabla ya kuanza kwa msimu uliomalizika na kufuzu majaribio ya kuichezea Yang iliyokuwa chini ya aliyekuwa kocha wakati huo, Mserbia Kostadin Papic, alilazimika kurejea kwao baada ya Yanga kushindwa kukamilisha taratibu za uhamisho wake.
Akizungumza jana baada ya kutua kwenye makao makuu ya Yanga, Asamoah alisema kuwa lengo la kurejea klabuni hapo (Yanga) ni kuhakikisha kuwa anashirikiana na wenzake kuipa timu yao mafanikio katika michuano ya Afrika.
Asamoah aliongeza kuwa amefika Yanga kulipa fadhila baada ya kuishi naye vizuri mwaka jana wakati akiwa kwenye majaribio na amewaahidi mashabiki wa klabu hiyo kusubiri matunda yake.
"Nimerejea kuichezea Yanga na ninaamini kwamba tutafanya vizuri msimu ujao na vile vile katika michuano ya Ligi ya Klabu Bingwa Afrika, ninafurahi kuwa tena hapa Tanzania," alisema mshambuliaji huyo kutoka FC Jagodina ya Serbia.
Nyota huyo ambaye katika mechi za maandalizi ya msimu uliomalizika alionyesha kiwango cha juu cha upachikaji mabao, ikiwa ni pamoja na kupachika mabao matatu peke yake katika mechi yao dhidi ya wageni kutoka Malawi, alikana kufanya mazungumzo na Simba kama ilivyotangazwa awali na Mwenyekiti wa ‘Wanamsimbazi’, Ismail Aden Rage.
"Mimi ni mchezaji wa Yanga, ni vigumu Simba kunipata. Nimekuja kuichezea Yanga ili ipate mafanikio, nilifurahi sana niliposikia kwamba imetwaa ubingwa wa ligi," aliongeza.
Mwenyekiti wa Yanga, Lloyd Nchunga, alisema kwamba safari hii watahakikisha kwamba usajili wa mchezaji huyo unakamilika ili apate nafasi ya kuitumikia timu yao.
Nchunga alisema kuwa wameamua kumleta mchezaji huyo kutokana na kuridhishwa na kiwango chake na tayari wameshaanza mawasiliano na klabu aliyokuwa akiichezea na muda wa usajili utakapofika watakamilisha taratibu za usajili wake.
"Mmemuona Asamoah, tuwaache wengine waendelee kupiga kelele," alisema Nchunga wakati akimuonyesha mchezaji.
Mara baada ya kuwasili kwenye Uwanja wa Ndege wa Kimataifa wa Julius Nyerere, Asamoah, alivalishwa fulana ya rangi ya njano iliyoandikwa jina na Rage kifuani.
CHANZO: NIPASHE
No comments:
Post a Comment