ANGALIA LIVE NEWS

Friday, May 13, 2011

Mameya watatu wamvaa Magufuli

 Wasema sasa anapuuza wakubwa wake
  Wasikitika kudhalilishwa na kauli zake
  Mmoja atoboa siri `ana ugomvi binafsi`
Waziri wa Ujenzi, Dk. John Magufuli
Wamiliki wa mabango na mameya wa manispaa za jijini Dar es Salaam, wamemjia juu Waziri wa Ujenzi, Dk. John Magufuli, wakimtaka aache ubabe katika utekelezaji wa majukumu yake na afuate maagizo yaliyotolewa na bosi wake, Rais Jakaya Kikwete.
Wakizungumza na NIPASHE jana, wamiliki hao walisema wameshtushwa na kauli ya Magufuli kuwa fedha za mabango zinatumika kulipana posho.
Wa kwanza kuponda kauli ya Magufuli ni Meya wa Manispaa ya Ilala, Jerry Silaa, ambaye alimtaka Magufuli kuacha ubabe na asikilize maagizo ya bosi wake, Rais Jakaya Kikwete, aliyoyatoa juzi mjini Dodoma wakati akifungua semina elekezi kuwa watekeleze wajibu wao kwa kutumia busara.

Alisema anafahamu fika kuwa Magufuli ana ugomvi na mmoja wa wamiliki wa makampuni yanayojihusisha na mabango, hivyo alimuasa kuwa makini ili ugomvi wake huo usiwasababishie wengine hasara na usumbufu.
“Yeye ana ugomvi na mtu mmoja, lakini anasahau kuwa wanaotangaza kwenye mabango ni wengi, yeye tunajua anachofanya ni kumkomoa mtu mmoja ambaye ana ugomvi naye, lakini hiyo si aina ya utendaji kazi ambayo Rais Kikwete anataka na ndiyo maana juzi Dodoma kawaambia watumie busara na hekima waache ubabe, labda hakumsikia vizuri bosi wake wakati anasema waache ubabe,” alisema Silaa.
Alisema kauli ya Magufuli kuwa fedha za mabango zinatumika kwa kulipana posho kwenye halmashauri ni dhihaka ya hali ya juu ambayo haivumiliki.
“Kwa mujibu wa sheria, udiwani ni kazi ya kujitolea maana haina mshahara, hii si kazi ya mshahara kama yeye, kwa hiyo sisi tunaona si bure huyu ndugu yetu labda anatafuta umaarufu wa kuwania urais, lakini sisi tunamwambia kama anautaka urais autafute kwa njia zingine sio kuharibu mipango ya maendeleo ya nchi hii,” alisema.
“Kutuambia sisi tunalipana posho fedha za kodi ya mabango ni utovu wa nidhamu wa kupindukia, mwambieni aache na asirudie tena kutudhihaki, ingawa hatupendi malumbano naye, lakini asituvunjie heshima,” alisema.
Alisema bajeti ya posho kwa mwaka katika manispaa hiyo ni Sh. milioni 48 tu wakati fedha zinazokusanywa kutokana na mabango zinafikia Sh. bilioni mbili.
Alisema miongoni mwa walipa kodi wakubwa na wazuri nchini ni wenye mabango hivyo kutaka kuyaondoa ni sawa na kuhujumu maendeleo.
“Kawaulize TRA kuhusu hawa wenye mabango namna wanavyotoa fedha nyingi serikalini kwa kodi, makampuni ya simu yote yanatangaza kwenye mabango, Tume ya Kudhibiti Ukimwi, (Tacaids), TRA wenyewe wanatangaza kwenye mabango, sisi tunachukua kodi maana mikataba tuliyoingia nao ni halali sasa mwenzetu sijui anatafuta nini labda umaarufu,” alisema.
Alisema watu wenye mabango wana mikataba halali na halmashauri na wale wanaotangaza kwenye mabango hayo wana mikataba halali na wenye mabango hivyo kuyaondoa ni kusababisha usumbufu usio wa lazima katika mikataba hiyo.
“Mwambieni hapa ni mjini asidhani yuko Chato, aliyemwajiri yeye Magufuli na wenzake juzi kawaambia Dodoma watumie busara katika maamuzi yao na tunadhani wamemwelewa,” alisema.
Mwingine ni Meya wa Kinondoni,Yusuf Mwenda, ambaye alisema kauli ya Magufuli kuwa fedha za mabango hazina msaada wowote kwa serikali si ya kweli.
Mwenda alisema fedha hizo zimekuwa msaada mkubwa kwa maendeleo ya manispaa hiyo tofauti na madai ya Magufuli.
Alisema hata katika bajeti ya mwaka huu wamepanga kutumia bilioni mbili kutoka kwenye mabango hayo, ambazo zitasaidia kuendesha miradi mbalimbali.
Alisema fedha hizo hutumika kuwalipa wakandarasi wanaozoa taka na kusafisha barabara, madawati shuleni na katika hospitali za manispaa hiyo.
“Mabango ni chanzo chetu muhimu sana cha mapato, fedha tunazitumia kwa miradi ya maendeleo kama shule, barabara na hospitali anaposema kuwa fedha hizo zinatumiwa kulipana posho anadanganya na ni uongo wa hali ya juu, madiwani wanalipwa Sh. 120,000 kwa mwezi, sasa inawezekana vipi bilioni mbili ziwalipe madiwani posho, ushahidi kwamba fedha hizi zinatumika kwa maendeleo upo na Mkaguzi na Mdhibiti Mkuu wa Hesabu za Serikali (CAG) huwa anakagua,” alisema Mwenda.
Alisema manispaa hiyo ina vyanzo vingi vya mapato ambayo mwaka huu wamepanga kukusanya bilioni 23 na mabango ni chanzo kimojawapo.
Kuhusu mpango wa Magufuli kubomoa mabango, Mwenda alisema walimwandikia Waziri Mkuu kuelezea namna watakavyoathirika iwapo yataondolewa na wanasubiri awajibu.
“Waziri Mkuu alituambia tumwandikie kuonyesha ni namna gani tutaathirika iwapo mabango yataondolewa na tumeshafanya hivyo na tunasubiri atujibu,” alisema.
Mkurugenzi Mwendeshaji wa kampuni ya matangazo ya A1 Outdoor, Edwin Sanda, alisema anashangazwa na kauli ya Magufuli kuzungumzia suala hilo wakati likiwa mahakamani.
Alisema mahakama ilishatoa katazo kwa serikali kupitia Wakala wa Barabara Nchini (Tanroads) kuvunja mabango hayo, hivyo kauli ya Magufuli ni ya ubabe tu.
“Mahitaji ya wananchi wa Tanzania si barabara tu kama anavyotaka Magufuli watu waamini, watu wanahitaji huduma nyingine muhimu kama za afya, elimu na usafi wa mazingira, fedha za mabango zinafanya kazi hiyo, sisi tunaona anatafuta ugomvi usio wa lazima na serikali za mitaa ambazo zinanufaika sana na fedha za mabango,” alisema.
“Hata hivyo suala hili tulishaliwasilisha mahakamani na ikatolewa amri ya zuio la kuvunja mabango, na kwa kawaida jambo likiwa mahakamani hutakiwi kulizungumzia sasa hatumwelewi mwenzetu anataka nini,” alisema Sanda.
Alisema walishawasilisha suala hilo kwenye ngazi za juu ili kuomba busara itumike katika mchakato huo, lakini alisema walishangaa wakati wanasubiri Magufuli anaibuka na madai mapya.
“Kuna kikosi kazi kiliundwa kwa ajili ya kuangalia na kushauri kuhusu suala hili na tunachosubiri kwa sasa ni mrejesho wa kile kikosi kazi,” alisema Sanda.
Kwa upande wake, Meya wa Manispaa ya Temeke jijini Dar es Salaam, Maabad Hoja, alisema kauli ya Magufuli imewadhalilisha madiwani kwa kiwango kikubwa.
Akizungumza na NIPASHE jana, alisema kauli kwamba pesa za mabango zinawanufaisha madiwani kwa kugawana posho haina hata chembe ya ukweli.
“Kama posho hata bungeni wanalipwa hii kauli inashangaza sana, kwa kweli Waziri ametusononesha sisi madiwani tumeona tumedhalilishwa,” alisema. Alisema halmashauri zote tatu za Ilala, Kinondoni na Temeke zimeungana katika kutetea mabango yasiondolewe na wameandika barua kwenda katika ngazi za juu kuomba uamuzi huo usitekelezwe.
Alisema hakuna sababu ya Magufuli kufanyakazi kwa mabavu kwani tayari suala hilo lilishaundiwa kikosi kazi na kinachosubiriwa ni majibu.
“Hatuwezi kumzuia kufanya hivyo, hata leo anaweza kuyaondoa, lakini tunaomba busara itumike hadi majibu ya maombi yetu huko ngazi za juu yajibiwe,” alisema.
Alifafanua zaidi kuwa kodi inayotokana na mabango hayo imesaidia kwa kiasi kikubwa katika maendeleo ya halmashauri zote ambapo nyingi zimeingizwa katika mafungu ya ujenzi wa miradi mbalimbali.
Juzi akihojiwa na kituo cha televisheni cha ITV, Magufuli alisema hakuna wa kumzuia kuvunja mabango ya biashara ambayo yako pembezoni mwa barabara kuu zote nchini.
Magufuli alisema kuwa mabango hayo yanawanufaisha tu madiwani kwa kulipana posho kwani fedha zinazotokana na ukodishwaji wake hazifanyi kazi yoyote ya maana.
Magufuli pia alikwisha kusema kuwa kokote kwenye barabara zinazosimamiwa na Tanroads mabango ni lazima yaondolewe, na kama halmashauri zinataka mabango basi yawekwe hata katikati ya barabara.
Akifungua semina elekezi Jumatatu wiki hii kwa mawaziri, manaibu waziri, makatibu wakuu na manaibu katibu wakuu, Rais Kikwete pamoja na mambo mengine aliwataka viongozi hao kuacha ubabe na dhuluma.
Hii ni mara ya pili viongozi wakuu, yaani Rais na pia Waziri Mkuu, Mizengo Ponda, kutoa maelekezo juu ya utendaji wa mawaziri, yakimlenga moja kwa moja Magufuli.
Akiwa ziarani Kagera, Pinda alisitisha amri ya kubomoa nyumba zote zilizojengwa kwenye hifadhi ya barabara akitaka ifanyike kwanza tathmini ili kubaini athari zake na kuangalia ni kwa jinsi gani serikali ingeweza kusaidia wananchi dhidi ya madhara hayo. Wakuu wa mikoa walipewa kazi hiyo.
Akiwa katika ziara ya Wizara ya Ujenzi, Rais Kikwete alimtaka Magufuli kuacha ubabe katika kuendesha kazi ya kubomoa nyumba kwenye hifadhi ya barabara na kutaka bomoa bomoa hiyo iwe na utu ikiwa ni pamoja na kuwapa muda wa kutosha wananchi kuhamisha mali zao.
Pia Rais Kikwete alisema pale mabadiliko ya sheria ya barabara yaliposababisha kuguswa kwa maeneo ya watu na mali zao ni lazima serikali iwape fidia.
CHANZO: NIPASHE

No comments: