ANGALIA LIVE NEWS

Wednesday, May 18, 2011

Wasomi Chuo Kikuu Dodoma wapinga mgawo wa umeme

Baada ya Shirika la Umeme Tanzania (Tanesco), kutangaza kuwepo kwa mgao mkubwa wa umeme nchini kuanzia kesho hadi Mei 26, wanafunzi wa vyuo vikuu mkoani Dodoma, wamepinga mgao huo na kuitaka serikali iingilie kati suala hilo ili kuiepusha nchi kuingia gizani.
Wanafunzi hao wamepinga mgao huo jana wakati wakizungumza na wandishi wa habari mjini hapa, ambapo Mwenyekiti wa wana vyuo hao kutoka Chuo cha Mtakatifu Yohana (St. John’s), John Kyabwe, alisema wanaamini kwamba serikali ina uwezo wa kuzuia.

Alisema wanatoa rai kwa serikali ifanye kila linalowezekana kuepusha nchi kuingia gizani tena kwa kukosa umeme.
“ Iwapo serikali itaruhusu mgao huu uwepo ni wazi nchi inaweza kuingia katika madhara makubwa katika sekta mbalimbali ikiwemo uchumi, biashara, afya, ulinzi na usalama, mzigo ambao utabebwa na mwananchi wa kawaida, tunadhani kuwa serikali itaufanyia kazi ushauri wetu”, alisema Kyabwe.
Alisema kukosekana kwa umeme wa uhakika nchini, kumekuwa kukichangia kwa kiasi kikubwa kupandisha gharama za maisha kutokana na kupanda kwa gharama za uzalishaji na biashara, ikiwa ni pamoja na kushuka kwa kiwango cha elimu nchini.
“Wanafunzi wanashindwa kujisomea usiku kwa kushindwa kutumia vifaa vinavyo tumia umeme hasa vya maabara, kompyuta na projekta”, alisema.
Aidha, alisema mgao huo utalikosesha mapato taifa kupitia Mamlaka ya Mapato (TRA) na Tanesco na mzigo huo kubebeshwa na mwanachi wa kawaida.
Alisema kwa kuwa tatizo la umeme limekuwa sugu na mawaziri katika wizara husika wameshindwa kutekeleza wajibu wao wa kuweka misingi thabiti katika suala hilo, hawana budi kuwajibika.
Wanavyuo hao walisema serikali inapaswa itekeleze mapendekezo ya Kamati ya Bunge ya Nishati na Madini yakiwemo ya kununua mitambo yake yenyewe ya uzalishaji wa umeme na kuiacha Tanesco itekeleze majukumu yake bila ya shinikizo la kisiasa.
CHANZO: NIPASHE

No comments: