ANGALIA LIVE NEWS

Wednesday, May 18, 2011

Tarime wasusia maiti za waliouawa na polisi

Wananchi wanaoishi kuzunguka mgodi wa dhahabu wa North Mara wilayani Tarime mkoani Mara,wamesusia kuchukua maiti sita za watu waliouawa baada ya kupambana na askari walipotaka kuingia mgodi wa North Mara.
Wananchi hao jana waliandamana hadi ofisi ya Mkuu wa Wilaya ya Tarime, walisema hawatachukua miili hiyo hadi wahusika ambao ni polisi watakaposhtakiwa.
Aidha, waliitaka serikali pia kuunda tume ya kuchunguza sababu ya kutokea kwa mauji hayo ya mara kwa mara na kutoa taarifa sahihi  katika kipindi kifupi.

Benard Koroso, mmoja ya wafiwa waliokuwa mbele ya lango la ofisi ya mkuu wa wilaya hiyo, alisema inasikitisha kuona polisi wakitumia nguvu kubwa kuua wananchi kwa kisingizio cha kuwalinda wawezekezaji badala ya kutumia sheria katika jambo hilo.
 Naye Job Chacha,mkazi wa Tarime pamoja na kusikitishwa na mauji hayo, alisema serikali kupitia jeshi la polisi inastahili lawama kutokana na kutumia nguvu kubwa kuliko hatua ambayo imekuwa ikileta madhara makubwa kwa wananchi.
  Kwa upande wake Lucas Ngonko, ambaye pia ni mmoja wa wafiwa,mbali na kukataa kupokea miili ya ndugu zao waliitaka serikali kutoa tamko litakalo sadia kukomesha mauji hayo na kulipa fidia kwa wote walipoteza maisha kwa mauji hayo ya kinyama.
Kwa upande wao baadhi yamadiwani wa maeneo hayo, walisema sababu kubwa ya kuendelea kwa mauji hayo ni kutokana na serikali kushindwa kuwatengea wananchi hao maeneo kwaajili ya uchimbaji. 
Kamanda wa  Mkoa wa  kipolisi wa Tarime na Rorya Kamishina Msaidizi, Constantine Massawe, alisema askari waliua baada ya kuzidiwa nguvu na kundi la watu wanaokadiriwa kufikia 1,000 waliodaiwa kutaka kuvamia mgodi huo kwa lengo la kuiba mchanga na mawe ya dhahabu.
 Kamanda Masawe, aliwataja waliouawa kwa kupigwa risasi na polisi kuwa ni Chacha Mwita (25) Chacha Ngoka (25 )Chawali Bhoke (26) Mwikwabe Marwa (35) na Emanuel Magige(27) ambapo mmoja kati yao mkazi wa wilaya ya Serengeti na wengine wakazi wa wilaya ya Tarime
 Hadi jana saa 12 jioni miili ya marehemu hao ilikuwa bado imehifadhiwa katika chumba cha maiti mjini Tarime, ambapo Mkuu wa wilaya ya Tarime John Henjewele, alipotakiwa kuzungumzia suala hilo alisema bado serikali inafanya uchunguzi.
CHANZO: NIPASHE

No comments: