ANGALIA LIVE NEWS

Wednesday, May 18, 2011

Mageuzi hadi vijijini mpango wa Mungu-Mbowe

Na Tumaini Makene

MWENYEKITI wa wa Chama cha Demokrasia na Maendeleo (CHADEMA), Bw. Freeman Mbowe amesema kuwa kasi ya mabadiliko ya siasa za mageuzi hadi vijijini  si 
matokeo ya nguvu za viongozi, bali ni mpango wa Mungu juu ya ukombozi wa wanyonge. 

Akionekana kuguswa na namna wananchi wanavyokiunga mkono CHADEMA katika harakati zake za kuuhamasisha umma wa Watanzania kutimiza wajibu, kudai haki na uwajibikaji wa viongozi katika suala zima la maendeleo ya watu na taifa kwa ujumla, Bw. Mbowe alisema 'sifa hizi mkinipatia mimi au viongozi wenzangu mtakuwa mnatutwisha mzigo tu, hii ni kazi ya Watanzania wote...ni mpango wa Mungu.


Bw. Mbowe ambaye pia ni Mkuu wa Kambi ya Upinzani Bungeni, aliyasema hayo juzi na jana katika mkutano wa hadhara pamoja na mkutano wa ndani alipokuwa akizungumza na wanachama wa chama hicho wa mjini Njombe, katika mfululizo wa mikutano ya Operesheni Sangara na mikoa ya Nyanda za Juu Kusini.

"Unajua mpaka wakati mwingine unaogopa, unatishika...maana haiwezekani ghafla tu nchi nzima unaona wananchi wanakubali mabadiliko, wanahitaji ukombozi na mabadiliko kwa kasi ya ajabu ambayo haijawahi kuonekana... waanzilishi wa mageuzi kama Mzee Nyimbo (Thomas) wanajua ugumu tuliowahi kupambana nao huko nyuma, lakini sasa ni wazi Watanzania wanadai ukombozi.

"Wananchi wanatuunga mkono kwa ari ya ajabu, demand (uhitaji) ya CHADEMA inakuwa kwa kasi mno, wananchi wako mbali katika kuhitaji mabadiliko kuliko hata ambavyo sisi viongozi tunafikiria...hawasikilizi tena propaganda zozote zile...ndiyo maana nasema huwezi kusema hii ni kazi yangu, wala ya viongozi wenzangu ni mpango wa Mungu.

"Maana haiwezekani ghafla tu CCM wamegeuka kuwa wezi, wanaiba mchana kweupe mpaka kila mwananchi anajua...ghafla ufisadi unaogharimu maendeleo ya watu na nchi unafanyika kila mahali, mchana kweupe, serikali yao haijali, wananchi wanafahamu kwamba nchi yao na wao wenyewe walistahili maendeleo kutokana na rasrimali zao lakini zinaliwa na watu wachache," alisema Bw. Mbowe. 

Katika mikutano yake Jimbo la Njombe Kusini, CHADEMA kilibaini vitendo vya kifisadi, baada ya wananchi kupewa nafasi ya kueleza kero zinazokwamisha maendeleo jimboni humo, ambapo walitoa madai ya 'kutapeliwa' takribani sh. milioni 57 walizochangishwa kwa ajili ya mradi wa maji mwaka 2008 kwa ahadi ya kupata maji ndani ya miezi sita, lakini mpaka leo hakuna chochote na hawajui zilivyotumika.

Wananchi hao, hususan wa Kijiji cha Lugenge walitoa malalamiko ya kwa viongozi wa CHADEMA, juu ya ubovu wa barabara inayoingia kijijini hapo lakini wamesikia mbunge wao, Bi. Anne Makinda (Spika wa Bunge) alijenga barabara mbili usiku ili wageni waliokuwa wakienda katika msiba wa mama yake, waweze kupita kwa uzuri, wakihoji bajeti hiyo imetoka wapi wakati wao 'hawaangaliwi' miaka yote wanayoteseka.

Kwa upande wake, Bw. Nyimbo, alisema watu wa mkoa huo, sasa wamegundua kuwa maendeleo yao na taifa kwa ujumla hayatapatikana kupitia CCM kwani kimefikia ukomo wa uwezo wa kuwaongoza.

Naye Mbunge wa Viti Maalum CHADEMA kutoka Iringa Mjini, Bi. Chiku Abwao, alisema kuwa wao kama wabunge watachukua kero za wananchi hao na kuzifuatilia, kwani wamegundua kuwa wananchi wa jimbo hilo hawana mwakilishi tangu mbunge wao walipochaguliwa kuwa spika wa bunge.
CHANZO:MAJIRA

No comments: