.jpg)
Afisa Habari wa Shirikisho la Soka (TFF), Boniface Wambura
Shirikisho la Soka la Afrika (CAF) limewazuia wachezaji Mbwana Samatta na Patrick Ochan kuichezea klabu yao ya zamani ya Simba katika mechi ya raundi ya tatu ya michuano ya Ligi ya Klabu Bingwa Afrika dhidi ya Wydad Casablanca ya Morocco takayochezwa Jumamosi jijini Cairo, Misri.
Akizungumza jana jijini Dar es Salaam, Afisa Habari wa Shirikisho la Soka (TFF), Boniface Wambura, alisema kuwa wachezaji hao hawana uhalali wa kuchezea Simba kwa sababu tayari klabu yao ya zamani (Simba) na ya sasa, TP Mazembe ya Jamhuri ya Kidemokrasia ya Kongo, wameshafikia makubaliano ya kuuziana.
Wambura alisema kuwa awali, Simba ilitaka kufahamu kama wanaweza kuwatumia wachezaji hao katika mechi dhidi ya Wydad na nyingine zitakazofuata na juzi, CAF ilituma taarifa ya kuwajulisha kwamba wawakilishi hao wa Tanzania hawaruhusiwi kuwatumia nyota hao ambao hivi sasa ni mali ya Mazembe.
"Simba kupitia TFF ilitaka kufahamu kama inaweza kuwatumia wachezaji hao kwa vile hati za uhamisho wa Kimataifa (ITC) za kuichezea TP Mazembe zilikuwa hazijatolewa, jana (juzi) usiku, CAF ilitujibu kwamba hawawezi kuichezea Simba kwa vile tayari wameuzwa, hivyo kutokuwa na sifa ya kuwa wachezaji wa timu hiyo kwa mujibu wa ibara ya 26 (1) ya kanuni za Ligi ya Klabu Bingwa Afrika," alisema Wambura.
Aliongeza kuwa Samatta na Ochan wanabanwa na sifa za kuendelea kuichezea Simba kwa sababu baada ya kuuzwa, sasa wanahesabika kwamba wanaishi Jamhuri ya Kidemokrasia ya Kongo na CAF inataka mchezaji achezee klabu ambayo iko katika nchi anayoishi.
Hata hivyo, Samatta na Ochan wasingeweza pia kuichezea TP Mazembe endapo ingekuwa haijatolewa katika mashindano hayo kwa sababu kanuni za CAF haziruhusu mchezaji mmoja kuchezea klabu mbili tofauti ndani ya msimu mmoja wa michuano yake.
Ochan alirejea nchini wiki iliyopita na yuko Visiwani Zanzibar katika kambi ya Simba kujiandaa na mechi hiyo ya Jumamosi wakati Samatta yuko na klabu yake ya Mazembe mjini Lubumbashi, Kongo baada ya kukataliwa kuja kujiunga na ‘Wekundu wa Msimbazi’.
Simba walilamizika kutaka ufafanuzi kutoka CAF ili kuepuka matatizo yaliyowakuta mabingwa watetezi, Mazembe, ambao walimchezesha beki Janvier Besala Bokungu aliyekuwa hajakamilishiwa taratibu za uhamisho kutoka klabu yake ya zamani ya Esperance ya Tunisia na mwishowe wakajikuta wakiondolewa katika michuano hiyo na nafasi yao kutwaliwa na atakayeshinda mechi ya Jumamosi baina ya Wydad na Simba ambao ndio walioshinda rufaa dhidi ya Bokungu.
CHANZO: NIPASHE
No comments:
Post a Comment