.jpg)
Aliyekuwa Kamishna Msaidizi wa Polisi (ACP), Abdallah Zombe
Aliyekuwa Kamishna Msaidizi wa Polisi (ACP), Abdallah Zombe, ameiomba mahakama kutoa hukumu yake katika malalamiko aliyowasilisha dhidi ya serikali na kutupilia mbali ombi la mdaiwa la kutaka shauri hilo kufutiliwa mbali kwa madai kuwa halina hoja za msingi kisheria.
Zombe alifungua kesi hiyo namba 35 ya mwaka 2011, katika Mahakama Kuu ya Tanzania, Kanda ya Dar es Salaam, akiiomba iiamuru serikali imlipe Shilingi bilioni tano.
Katika majibu yake dhidi ya hoja za serikali aliyowasilisha mahakamanihapo juzi, Zombe amedai kuwa kulingana na mwenendo wa kesi hiyo haihusiani na rufaa iliyopo katika Mahakama ya Rufaa na kwamba mdaiwa anapaswa kuwasilisha vielelezo vya kutosha kuthibitisha madai ya hoja zake.
Anadai kuwa kulingana na maudhui ya maelezo ya utetezi, Zombe amedai kuwa anao ushahidi wa kutosha dhidi ya mdaiwa na kwamba kinacholalamikiwa ni mwenendo uliotokea kabla ya mashtaka hayajawasilishwa dhidi yake.
Amedai pia kuwa hoja ya serikali kwamba shauri hilo lifutwe kwa kuwa kuna rufaa iliyokatwa dhidi yake katika Mahakama ya Rufani hayana msingi kwani shauri hilo la madai linaweza kuendelea bila kuathiri rufaa hiyo.
Zombe amepinga madai kwamba aliitwa na kujieleza lakini ukweli ni kwamba hakuulizwa chochote kabla ya kupelekwa mahakamani na hatimaye gerezani.
Amedai kuwa anapinga madai kuwa alipewa nafasi ya kujieleza na kwamba polisi walitekeleza wajibu wao ipasavyo, ukweli ni kwamba hakupewa nafasi ya kujieleza ambapo pia amemtaka mdaiwa kuthibitisha madai hayo kwani Polisi walishindwa kutekeleza wajibu wao kwa kumshtaki bila ushahidi na kumuunganisha katika tuhuma hizo. Kupitia kwa Mwanasheria Mkuu wa Serikali, serikali iliwasilisha majibu ya hoja ya kwenye hati ya madai ya Zombe kupitia kwa wakili wake, Richard Rweyongeza, Machi mwaka huu.
Shauri hilo lilitajwa kwa mara ya kwanza Mei 16, mwaka huu mbele ya Jaji Upendo Msuya.
Katika shauri hilo, Jaji Msuya, aliutaka upande wa mdai (Zombe) ambaye anawakilishwa na Wakili Rweyongeza, kuwasilisha majibu ya serikali Mei 23, mwaka huu kwa njia ya maandishi, na shauri hilo limepangwa kutajwa Juni 20, mwaka huu.
Mwanasheria Mkuu, aliiomba Mahakama kufutilia mbali madai ya Zombe kwa madai kuwa hayana hoja za msingi za kisheria.
Alidai kuwa Zombe alipelekwa mahakamani kujibu mashtaka hayo halafu akapelekwa jela Ukonga ni sahihi lakini si kweli kwamba Mahakama pamoja na Magereza zilikuwa zimetayarishwa kwa ajili yake, ukiachilia mbali dai la kwamba hakukuwa na hati ya kuitwa shaurini ambapo amemtaka kuthibitisha madai hayo.
Aidha, madai ya kwamba serikali ilivunja sheria kwa kumnyima haki ya kusikilizwa si kweli kwani aliitwa na kuhojiwa na tume hiyo kabla ya kupelekwa gerezani Ukonga, na kwamba kutiwa mbaroni kwa mdai hakukutokana na kushindwa kwa Polisi kufanya kazi yao ya kisheria na mdai anatakiwa athibitishe madai hayo.
‘‘Mdai hana madai yoyote dhidi ya serikali na anatakiwa kuthibitisha hivyo, kwa kuongezea kuna rufani ambayo haijasikilizwa katika Mahakama ya Rufani Tanzania, kwa msingi huo mdaiwa anaomba Mahakama itupilie mbali madai hayo na mdai alipie gharama za kesi hiyo,’’ inadai sehemu ya hati hiyo ya majibu ya serikali. Zombe aliachiwa huru pamoja na askari wengine waliokuwa wakikabiliwa na kesi ya mauaji ya wafanyabiashara watatu na dereva wa teksi.
Kwa kupitia hati yake ya madai, Zombe anadai alishtakiwa kimakosa katika kesi ya mauaji ya wafanyabiashara watatu wa madini na dereva wa teksi.
Zombe anadai kiasi hicho cha fedha ikiwa ni fidia kwa adhabu ya kumweka ndani wakati kesi hiyo ilipokuwa ikiendelea, riba na gharama za kesi na kutaka alipwe fidia hiyo kwa madhara aliyoyapata katika kesi hiyo.
Pia anaiomba mahakama itamke alikamatwa na kushtakiwa kinyume cha sheria, akidai kabla ya kukamatwa, alikuwa amehamishiwa katika Mkoa wa Rukwa, alirejeshwa Makao Makuu ya Polisi siku 14 baada ya kuripoti kituo kipya cha kazi.
Katika kesi hiyo ya mauaji, Zombe alipandishwa kizimbani Juni 9, 2006 na kuunganishwa na askari wenzake wengine ambao jumla yao walikuwa 13.
Agosti 17, 2009, mahakama ilimuachia huru yeye na wenzake baada ya kuwaona hawana hatia katika makosa yaliyokuwa yakiwakabili.
Zombe na wenzake, walikuwa wakituhumiwa kuhusika na mauaji ya
wafanyabiashara wa madini Sabinus Chigumbi (Jongo), Ephrahim Chigumbi, Mathias Lunkombe na dereva wa teksi Juma Ndugu, Januari 14, 2006 katika msitu wa Pande mkoani Dar es Salaam.
CHANZO: NIPASHE
No comments:
Post a Comment