.jpg)
Waziri Kivuli wa Fedha na Uchumi, Zitto Kabwe
Waziri Kivuli wa Fedha na Uchumi, Zitto Kabwe, amesema ameelekezwa na chama chake kuwasilisha bungeni bajeti mbadala itakayopunguza bei ya mafuta ya petroli na dezeli kwa asilimia 50 na misamaha ya kodi kutoka asilimia 2.5 za sasa hadi asilimia moja, ili kumsaidia mwananchi wa kawaida kumudu gharama za maisha.
Alisema bajeti hiyo mbadala, ambayo itawasilishwa katika Mkutano ujao wa Bunge la Bajeti unaotarajiwa kuanza mwezi ujao, pia itahakikisha inapunguza gharama za usafiri, kusafirisha chakula na itapunguza kodi.
Zitto, ambaye pia ni Naibu Katibu Mkuu wa Chama cha Demokrasia na Maendeleo (Chadema) Tanzania Bara, alisema hayo katika mkutano wa hadhara uliofanyika katika Uwanja wa Rukwa High School (Msakila), katika kilele cha maandamano yaliohudhuriwa na maelfu ya wafuasi wa chama hicho mjini hapa jana.
Zitto alisema kazi ya Chadema hivi sasa, ni kuhakikisha wanapiga kelele kila wanapoona mambo hayaendi vizuri serikalini. Alisema kuanzia sasa watahakikisha bajeti mbadala ya kambi rasmi ya upinzani bungeni inaangalia namna gani itawezekana kupunguza gharama za maisha ya wananchi.
Alisema gharama za maisha, huchangiwa na kupanda kwa bei ya mafuta.
“Nimeelekezwa na chama changu kwamba, bajeti mbadala iwe ni kupunguza bei kwenye mafuta kwa asilimia 50, gharama za usafiri, kusafirisha chakula ili mwananchi wa kawaida aweze kumudu maisha yake,” alisema Zitto, ambaye pia ni Mbunge wa Kigoma Kaskazini na Naibu Kiongozi wa Kambi ya Upinzani Bungeni.
Zitto, alisema misamaha ya kodi kwa mwaka ni Sh. bilioni 630, ambayo ni sawa na asilimia 2.5, hivyo alisema wanataka katika bajeti hiyo wapunguze ifikie asilimia moja tu ya pato la taifa.
“Wanaopata misamaha ya kodi si maskini bali ni makampuni makubwa, kama vile ya madini,” alisema Zitto.
Alisema katika bajeti hiyo mbadala watahakikisha pia kila kodi inayotakiwa kulipwa nchini inalipwa.
Alisema maisha yamekuwa magumu baada ya bidhaa muhimu, kama vile sukari kupanda bei kati ya Oktoba mwaka jana na Mei mwaka huu, huku kipato cha mwananchi wa kawaida kikizidi kushuka.
Alitoa mfano kuwa mwaka jana mahindi yalikuwa yakiuzwa kwa Sh. 500 kwa kilo, lakini mwaka huu yanauzwa Sh. 300, wakati sukari ilikuwa ikiuzwa kwa Sh. 1,200, lakini hivi sasa imefikia Sh. 2,000 kwa kilo.
Zitto alisema lazima yawekwe mazingira, ambayo kila Mtanzania atapata haki yake ya kimsingi ya maisha bora na si bora maisha.
Katibu Mkuu wa Chadema, Dk. Willibrod Slaa, aliwataka wananchi wa Jimbo la Sumbawanga Mjini kujiandaa kwa marudio ya uchaguzi katika jimbo hilo.
Mgombea wa Chadema, Norbert Yamsebo, amefungua kesi mahakamani kupinga matokeo ya uchaguzi yaliyompa ushindi Mbunge wa sasa wa jimbo hilo, Hilali Aeshi, katika Uchaguzi Mkuu wa mwaka jana.
Dk. Slaa alisema ingawa Chadema haijaingia Ikulu, lakini watapambana bungeni kuhakikisha ahadi walizotoa za elimu, huduma za afya bure zinatekelezwa.
Alisema nchi itatawalika iwapo tu watu watakula, kuvaa vizuri, kulala katika nyumba za hadhi ya binadamu.
Alifichua waraka wa siri wa CCM unaokiri kwamba, chama hicho kimepoteza ladha kwa Watanzania, wamepoteza tunu ya uadilifu na uaminifu na wananchi wameikataa kwa sababu imeshindwa kutekeleza sera ya ujamaa na kujitegemea.
Mwenyekiti wa Chadema, Freeman Mbowe, alisema iwapo uchaguzi katika jimbo la Sumbawanga Mjini utarudiwa ‘CCM watajua muziki wa Chadema’.”
Maandamano hayo, yalianzia katika eneo la Nambogo nje kidogo ya mji wa Sumbawanga majira ya saa 8 mchana na yalipita katika Barabara ya Mpanda hadi katika uwanja huo, ambako viongozi wakuu ngazi ya taifa, wilaya na mkoa pamoja na wabunge walihutubia mkutano wa hadhara.
Vibwagizo vya nyimbo za waandamanaji waliokuwa wamebeba mabango yenye ujumbe mbalimbali, huku wakiwa wamevalia mavazi rasmi ya chama na kubeba bendera za chama, vilijikita zaidi katika kumkejeli Mbunge wa Sumbawanga Mjini, Hilal Aeshi.
Baadhi ya mabango yalisomeka: “CCM hata mkijivua gamba bado sumu ipo”, “Ukitaka tisheti na kofia muone Aeshi ukitaka maendeleo muone mbunge wa wananchi Yamsebo.”
Maandamano hayo yaliongozwa na msururu mrefu wa magari, pikipiki, baiskeli na watembea kwa miguu.
Wabunge wengine waliohutubia mkutano huo wa hadhara jana, ni Raya Ibrahim Khamisi (Viti Maalum-Pemba), Joyce Mkya (Viti Maalum-Arusha), Mallac (Viti Maalum-Rukwa), Naomi Kaihula (Viti Maalum-Mbeya), Regia Mtema (Viti Maalum-Morogoro), David Silinde (Mbozi Magharibi), Suzan Kiwanga (Viti Maalum-Morogoro) na Mchungaji Peter Msigwa (Iringa Mjini).
Pia walikuwamo Grace Kiwelu (Viti Maalum-Kilimanjaro), Chiku Abwao (Viti Maalum-Iringa), Joseph Mbilinyi “Mr. Sugu” (Mbeya Mjini), Ofisa Mwandamizi katika Kurugenzi ya Sera na Utafiti, Mwita Mwikabe Waitara, Mkurugenzi wa Organaizesheni na Mafunzo, Benson Kigaila, kada mwandamizi wa Chadema, Fred Mpendazoe na Makamu Mwenyekiti wa Chama hicho Zanzibar, Said Issa Mohamed.
Mpendazoe alisema CCM iliyoachwa na Mwalimu Julius Nyerere, ambayo ilikuwa ni chama cha wakulima na wafanyakazi, kutetea wanyonge na kupigania usawa ni tofauti na ya sasa.
Alisema CCM ya sasa ni ya matajiri na wafanyabiashara.
Alisema vita dhidi ya ufisadi vinavyoendeshwa na CCM, si vya dhati kwani licha ya Dk. Slaa kutaja orodha ya vigogo mafisadi mwaka 2007, hakuna hatua zozote zilizochukuliwa dhidi ya vigogo hao.
CHANZO: NIPASHE
No comments:
Post a Comment