ANGALIA LIVE NEWS

Thursday, May 19, 2011

Kero za Muungano zitakuwa historia: Dk. Bilali

Kero za Muungano wa Tanganyika na Zanzibar zitabakia kuwa historia kwa vile serikali ya awamu ya nne ya Muungano imekusudia kumaliza kero hizo.
Hayo yameelezwa na makamu wa Rais, Dk. Mohammed Gharibu Bilali alipokuwa akizungumza na wanachama wa CCM katika viwanja vya Micheweni Mkoa wa Kaskazini Pemba.

Alisema serikali imedhamiria kuzipatia ufumbuzi kero zote za Muungano katika muda mwafaka ili kuondoa malalamiko yanayojitokeza katika pande mbili za Muungano.
Dk. Bilali alifafanua kwamba Muungano wa Tanganyika na Zanzibar umeleta faida nyingi kwa wananchi ikiwemo kujenga umoja wa kitaifa licha ya kukabiliwa na changamoto katika miaka 47 ya Muungano huo.
Alisema kwamba kero nyingi tayari zimeshapatiwa ufumbuzi na kwamba zilizobakia zinaendelea kufanyiwa kazi ili kuhakikisha kasoro zote za Muungano zinabakia kuwa historia katika taifa la Tanzania.
“Serikali ya awamu ya nne imedhamiria kuzipatia ufumbuzi kero zote lengo ni kuona zinabakia historia kwa sababu muungano wetu unafaida nyingi kwa wananchi wa pande zote za muungano,” alisema.
Kuhusu hali ya kisiasa Zanzibar, Dk. Bilali amewataka wanachama wa CCM Zanzibar kujenga umoja na kujiepusha na malumbano na migogoro ili kuhakikisha chama hicho kinaendelea kukamata hatamu ya dola Zanzibar na Tanzania bara.
Alisema kwamba viongozi na wanachama kazi yao kubwa hivi sasa ni kuongeza wanachama wapya ili chama kiweze kuwa na nguvu hasa kisiwani Pemba kabla ya kufanyika kwa uchaguzi mkuu mwaka 2015.
“Wakati huu si wakati wa kusherehekea ushindi uliopatikana katika uchaguzi uliopita bali ni muda wa kukiimarisha chama kuelekea uchaguzi ujao,” alisema Dk. Bilali katika ziara yake ya kukagua miradi ya maendeleo na uhai wa chama Zanzibar.
CHANZO: NIPASHE

No comments: