ANGALIA LIVE NEWS

Thursday, May 19, 2011

Mbunge apigwa mawe

  Sare za CCM zachanwa
  Magari nayo yapopolewa
Mbunge wa Tarime, Nyambari Nyangwene (CCM)
Hali katika kitongoji cha Nyamongo ni tete ikichangiwa na hisia kali za vifo vya watu watano waliouawa na Polisi kwa madai ya kutaka kuvamia mgodi wa North Mara, na sasa Mbunge wa Tarime, Nyambari Nyangwene (CCM) na viongozi wengine wa halmashauri ya wilaya ya Tarime wameshambuliwa kwa mawe na magari yao kuharibiwa vibaya.
Tukio hilo lilitokea jana wakati Nyangwene akiwa na msafarawake wakiwasili Nyamongo katika mkutano uliokuwa umeitishwa kuzungumzia tukio la mauaji hayo, lakini miongoni mwa waliokuwamo kwenye msafara huo ni makada wa CCM waliokuwa wamevaa sare za chama hicho,
hali iliyoamsha taharuki kubwa.
Wananchi hao kwa mamia walianza kupiga kelele kama vile kuomba msaada kutokana na kuvamiwa na wezi, huku wakilalamika kuwa waliokuwa wamevaa sare hizo walikuwa wanawakasirisha kwa kuwa serikali ya CCM imeshindwa kutatua kero zao.
Katika kadhia hiyo, kada mmoja wa CCM ambaye jina lake halikupatika mara moja, shati lake la chama lilichanwa chanwa, huku Mwenyekiti wa Halmashauri ya Tarime, Amos Sagana, akivua sare ya shati na kofia za CCM na kubaki na fulana tu.
Makada wengine wa CCM aliokuwa wamevaa sare hizo, walilazimika kuzivua na kujisalimisha kwenye ofisi ya serikali ya mtaa katika eneo hilo.
Magari yaliyoharibiwa kwa kuvunjwa vioo ni la mwenyekiti wa halmashauri ya Tarime, Toyota Land Cruiser namba STK 8411 na la waandishi wa habari T299 ASW aina ya Toyota Land Cruser Prado mali ya mbunge huyo.
Yote yalipigwa kwa mawe yaliyokuwa yakirushwa mfululizo na wananchi jambo lilisababisha mbunge huyo na msafara wake kukimbia huku wakiendelea kushambuliwa.
Wananchi hao walieleza pia kwamba kitendo cha serikali kushindwa kuwapatia maeneo ya wachimbaji wadogo wadogo pamoja na kushindwa kuchukua hatua za haraka katika kudhibiti mauaji ya mara kwa mara ambayo yamekuwa yakifanywa na polisi katika mgodi wa dhahabu wa North Mara ni moja ya sababu za kufanya hivyo.
“Sisi hatuna kosa na mbunge wetu kwanza yeye hakuua, lakini hatuwezi kumsikiliza kwa vile serikali yake ndio inayotumia polisi kulinda Wazungu na kutuua sisi kinyama kila kukicha,” alisema mwananchi mmoja.
Mwananchi mwingine alijitambilisha kwa jina la Chacha Keresa, alisema viongozi wa serikali katika ngazi ya wilaya wamekuwa wakishindwa kutatua matatizo yao, lakini wamekuwa wakijitokeza hadharani pindi tu wanaposikia wananchi wanakusudia kuwafanyia fujo wawekezaji.
“Siku zote sisi tunasema hatuna eneo la kulima tunataka tupewe sehemu ya kufanya uchimbaji mdogo, lakini umekuwa wimbo sasa leo wameuawa vijana wetu tena hata maiti zikiwa bado hazijazikwa wanakuja na nguo za CCM kufanya nini,” alisema.
Naye Yahana Chacha, alisema endapo serikali haitachukua hatua za haraka za kutatua tatizo la umaskini linalowakabili wananchi wa maeneo hayo hakuna amani itakayopatikana daima.
“Tunachosema hakuna jambazi anayekwenda kuiba mawe haya yote tunayafanya kwa umaskini sasa hapa si kutumia polisi bali serikali itafute njia ya kumaliza umaskini kwa wananchi bila hivyo wataleta hata JWTZ lakini hakuna watakachosaidia,” alisema.

NYANGWENE: KUVAA SARE SI KOSA
Akizungumza na NIPASHE baada ya kuokolewa na walinzi wake binafsi kutoka katika kundi hilo la wananchi, Nyangwene pamoja na kulaani kitendo hicho, alisema hatua iliyofanywa na wananchi hao inatokana na uchochezi wa kisiasa.
Alisema si jambo la busara wananchi kuwashambulia wananchi wengine kwa kosa la kuvaa sare za chama cha siasa na hivyo kuwaomba viongozi wanaotumia matatizo kujitafutia umaarufu wanaweza kuhatarisha amani wilayani Tarime.
“Hawa walikuja na sare hizi baada ya kumpokea katibu mkuu wao wa CCM, sasa niliposema nakwenda kuzungumza na wananchi wangu hasa kwa kuwapa pole baada ya yale mauji waliniunga mkono cha kushangaza kabla ya kutoa pole tukaanza kushambuliwa,” alisema.
Hata hivyo, pamoja na magari hayo kuharibiwa vibaya, viongozi waliokuwemo walitoka salama.
Kufuatia hali hiyo, mbunge huyo wa Tarime, alimetoa tamko kwa kuitaka serikali kuchukua hatua za haraka za kuwapatia wananchi hao maeneo ya uchimbaji mdogo huku akiutaka uongozi wa mgodi huo kutekeleza kwa vitendo mikataba ya vijiji vinavyozunguka mgodi huo.
“Natumia nafasi hii kuitaka serikali licha ya kuchukua hatua kwa wote waliohusika na mauji haya ya wananchi, lakini pia serikali kupitia Wizara ya Nishati itekeleze kwa vitendo mpango wa kuwapatia wananchi maeneo ya kuchimba na wawekezaji watekeleze kwa vitendo makubaliano yaliomo katika mikataba,” alisema Nyangwine.
Kamanda wa Polisi Kanda Maalum ya Polisi, Tarime/Rorya, Costantine Massawe, amethibitisha kutokea kwa vurugu hizo.
Kamanda Massawe alisema tayari serikali imeanza kuunda tume itakayochunguza tukio la kuvamiwa kwa mgodi huo kabla haijaanza kuchukua hatua zaidi.
Alisema katika tukio la jana, mtu mmoja alijeruhiwa ambaye alitibiwa kwenye hospitali ya wilaya ya Tarime na kuruhusiwa.
Kamanda Massawe alisema hali mjini Tarime ni tete na kuwataka wananchi kuheshimu sheria na taratibu za serikali katika kushughulikia tukio la North Mara.

WAKUSANYIKA CHUMBA CHA MAITI
Naye Samson Chacha, anaripoti kwamba umati mkubwa zaidi ya watu 200 umekusanyika nje ya chumba cha maiti katika hospitali ya wilaya Tarime wakitokea maeneo ya Nyamongo huku wakikataa kuchukua miili ya marehemu waliouawa na polisi.
Kufuatia hali hiyo, Kamanda Massawe amewataka wananchi kuchukua miili ya marehemu hao na kwenda kuwazika wakati serikali ikiendelea kuunda kamati maalum.
Mei 16 mwaka huu watu watano kutoka katika kundi la watu wanaodaiwa kutaka kuvamia mgodi wa North Mara waliuawa kwa kupigwa risasi na askari polisi huku wengine zaidi ya watatu wakijeruhiwa jambo ambalo limesababisha kutoelewana huko kati ya wananchi na viongozi hadi sasa.
Baada ya kutokea kwa hali hiyo NIPASHE imeshuhudia vikosi mbalimbali vya askari wa jeshi la polisi kutoka mkoa wa kipolisi wa Tarime na mkoa wa Mara vikipelekwa katika eneo la mgodi huo ili kuimarisha ulinzi.
Hadi kufika jana miili ya wananchi hao waliouawa na polisi ilikuwa imehifadhiwa katika chumba cha maiti katika hospitali ya serikali ya wilaya Tarime.

KAGASHEKI
Naibu Waziri wa Mambo ya Ndani ya Nchi, Balozi Khamisi Kagasheki, amekemea vikali tabia ya baadhi ya wanasiasa nchini kuingiza siasa katika matatizo yanayotokea kwenye jamii.
Akizungumza na waandishi wa habari, jana jijini Dar es Salaam, Kagasheki alisema wanasiasa hao wamekuwa wakijiingiza katika matukio mbalimbali ambayo yanachochea migogoro kati ya serikali na wananchi badala ya kuwaelimisha juu ya haki zao.
Alisema kwa kuthibitisha kauli hiyo, kuna wanasiasa ambao waliandaa maandamano katika Mgodi wa Nyamongo wilayani Tarime, sehemu iliyotokea fujo kati wananchi waliovamia mgodi na askari polisi waliokuwa wakipambana nao.
“Kuna watu kutoka katika chama kimoja cha siasa walikuja kuomba kibali cha kufanya maandamano na mkutano, lakini kiukweli kwamba kibali walinyimwa kutokana na maandamo hayo kuashiria wazi kuwa ni ya shari kwa serikali,” alisema Balozi Kagasheki.
“Kama unavyojua kuwa polisi kazi yao ni kulinda mali na usalama wa wananchi, basi walipambana na wahalifu hao waliokuwa na silaha za jadi ambazo ni mapanga, shoka na visu ndipo polisi walilazimika kutumia mabomu ya machozi ila chakushangaza walizidisha mapambano,” alisema Kagasheki.
Alieleza kuwa hakuna serikali inayopenda kuwaua wananchi wake ila inaonyesha wazi watu hao waliuawa kutokana na kufanya kitendo cha uovu.
Alisema wamesikitishwa na vifo hivyo na serikali imejitolea kufanya shughuli za mazishi kutokana na wahalifu hao kuwa ni Watanzania hata kama walifanya mambo maovu.
Alifafanua kuwa katika familia zote tano ni familia moja tu ambayo imekubali kufanyiwa mazishi ya ndugu yao na nne zikikataa kufanyiwa shughuli hiyo mpaka maandamano yatakapofanyika.
Alisema hiyo inaonyesha kuwa ndugu hao wamepewa vishawishi na chama hicho ndio maana wamekinyima kibali cha kufanya maandamano na kusema labda wangekubali kuzika ndipo wafanye.
Balozi Kagasheki ametoa pole kwa familia za Watanzania 16 waliofariki na 45 kujeruhiwa katika ajali ya gari zilizogongana juzi, wilayani Geita.
CHANZO: NIPASHE

No comments: