ANGALIA LIVE NEWS

Saturday, May 7, 2011

Mauaji yatikisa

Wanawake watatu wachinjwa mithili ya kuku
  Mwanafunzi anyongwa, wawili wafa bwawani

Wanawake watatu wameuawa kikatili kwa kukatwa katwa kwa mapanga na watu wasiofahamika jana alfajiri karibu na mlima Mbeya, nje kidogo ya Jiji la Mbeya na sehemu zao za maziwa kuchukuliwa.
Kwa mujibu wa shuhuda mmoja, Simon Mwakyombe, wakati anapita eneo hilo, aliishuhudia miili hiyo na kuwataarifu polisi kwa njia ya simu na polisi walifika baadaye katika eneo hilo.
NIPASHE ilifika eneo la tukio na kuwashuhudia polisi wakiondoka na miili hiyo na kuipeleka katika chumba cha kuhifadhi maiti katika Hospitali ya Mkoa wa Mbeya.

Habari zinasema kuwa wanawake hao waliuawa jana alfajiri wakati wakielekea mashambani kulima.
Kamanda wa Polisi wa Mkoa wa Mbeya, Advocate Nyombi, alipotafutwa jana kutoa ufafanuzi wa mauaji hayo, alisema alikuwa na shughuli nyingi za kufuatilia maandamano ya amani ya Chama Cha Demokrasia na maendeleo (Chadema) yaliyokuwa yakifanyika jijini Mbeya pamoja na mkutano wa hadhara.
Kamanda Nyombi, alisema Kamanda wa Polisi wa Wilaya (OCD) alikuwa akilifuatilia tukio hilo na kwamba baada ya kulikamilisha yeye (Nyombi), angetoa taarifa.
Hadi tunakwenda mitamboni, Kamanda Nyombi hakulitolea ufafanuzi.
Katika tukio lingine, mwanafunzi wa darasa la kwanza, katika Shule ya Msingi Ambureni, wilayani Arumeru, Prince Elisaria (7), amekutwa ameuawa na mwili wake kuwekwa ndani ya kiroba.
Kaimu Kamanda wa Polisi Mkoa wa Arusha, Akili Mpwapwa, alisema tukio hilo lilitokea Mei 3, mwaka huu, saa 8:00 mchana katika Kitongoji cha Nguambia, Kijiji cha Nkoandua.
Alisema marehemu aliondoka nyumbani kwa wazazi wake Aprili 29, saa 1:00 asubuhi kuelekea shuleni, lakini hakurejea.
“Lakini cha kushangaza wazazi walisubiri hata baada ya muda wa kurudi nyumbani ulipofika hawakumuona na walipojaribu kuulizia shuleni hakuonekana, ndipo jitihada za kumtafuta zikaanza na kutupa sisi polisi taarifa,” alisema Kamanda Mpwapwa.
Alisema baada ya Polisi kupewa taarifa hizo, walishirikiana kuendesha msako mkali na kufanikiwa kupata mwili wake uliokuwa umewekwa katika kiroba Jumanne wiki hii majira ya mchana.
“Tuliufungua mfuko huo, tukashangaa kuona mwili wa mtoto huyo huku ukiwa umeharibika. Tulichunguza na kubaini aliuawa na watu, hivyo tukaamuru uzikwe,” alisema Kamanda Mpwapwa.
Alisema Polisi bado wanaendelea na uchunguzi ili kubaini wahusika wa tukio hilo na kuomba mtu yeyote mwenye taarifa kuhusu aliyehusika katika tukio hilo atoe taarifa za siri polisi akamatwe na kufikishwa mbele ya sheria.

WATOTO WAWILI WAFA MAJI DAR
Jijini Dar es Salaam, watoto wawili wamekufa maji baada ya kuzama katika dimbwi walilokuwa wanaogelea eneo la Kibamba Hondogo, Wilaya ya Kinondoni, mkoani Dar es Salaam.
Tukio hilo lilitokea juzi saa 11:00 jioni wakati watoto hao wakiogelea na wenzao katika dimbwi lililopo karibu na maeneo wanapoishi.
Watoto hao ambao ni wanafunzi wa darasa la tano na sita, walizidiwa na maji kisha kuzama na kunywa maji mengi, hali iliyosababisha kufariki dunia.
Kamanda wa Polisi Mkoa wa Kinondoni, Charles Kenyela, aliwataja watoto hao kuwa ni Polycarp Mollo (13) darasa la tano na Hamisi Marana (12), ambaye alikuwa anasoma darasa la sita, wote wakiwa wanafunzi wa Shule ya Msingi Kibwegere.
Kamanda Kenyela alisema miili ya watoto hao iliopolewa na Kikosi cha Zimamoto cha Jiji la Dar es Salaam kwa kushirikiana na wakazi wa eneo hilo.
Imeandikwa na Cynthia Mwilolezi, Arusha; Erick Mashafi, Dar na Emmanuel Lengwa, Mbeya.
CHANZO: NIPASHE

No comments: