Wanafunzi wa mwaka wa kwanza katika chuo kikuu kishiriki cha Tumaini kampasi ya Masoka wilayani Moshi mkoani Kilimanjro,wametakiwa
kuondoka chuoni hapo hadi Mei 20, baada ya kudaiwa kugoma kuingia madarasani.
Wanafunzi hao ambao waliandikiwa tangazo katika ubao wa matangazo chuoni hapo, walitakiwa kuondoka chuoni hapo mara moja kutokana kukataa kuingia darasani.
Katika madai yao ya msingi, wanafunzi hao wanadai kufundishwa masomo ambayo ni tofauti na kozi walizotakiwa kusoma sambamba na kutokuwa kwa mkataba(Prospectus)wa masomo chuoni hapo.
Wanafunzi hao wanaosoma Shahada ya Uhasibu na Utalii walitakiwa kuondoka chuoni hapo ambapo tangazo la kutakiwa kuondoka lilibandikwa jana saa 10:00 jioni.
Tangazo hilo liliwataka wanafunzi hao wa mwaka wa kwanza kuhakikisha watakaporudi chuoni hapo wawe wamekamilisha madeni yote wanayodaiwa na katika barua watakayoiandika waeleze sababu zilizowafanya wagome, aliyewaambia wagome na waelezee namna watakavyojiheshimu pindi watakaporudi chuoni.
Baada ya kuondoka chuoni hapo, walikwenda hadi katika ofisi za Askofu wa Kanisa la Kiinjili la Kilutheri Tanzania (KKKT) Dayosisi ya Kaskazini kuzungunza na katibu wa Askofu kuhusiana na suala hilo, lakini mazungumzo yao hayakuzaa matunda.
Uongozi wa chuo hicho haukutaka kuzungumza chochote na waandishi wa habari.
Aidha, uongozi wa dayosisi ulipotakiwa kutoa ufafanuzi kuhusu sababu za kuwapo kwa migomo ya mara kwa mara chuoni hapo, haukuwa tayari kuzungumza.
CHANZO: NIPASHE
No comments:
Post a Comment