Asema ni vile vinavyotetea maslahi ya nchi
Awataka wanachama wa Chadema kushawishi
Awataka wanachama wa Chadema kushawishi
Mwenyekiti wa Chama cha Demokrasia na Maendeleo (Chadema), Freeman Mbowe, amesema Chadema inahitaji kuungana na vyama vyote vya siasa vyenye mwelekeo wa kutetea maslahi ya wananchi na kuwataka wana-Chadema kufanya kazi ya kuwashawishi wanachama wa vyama hivyo kuhusu jambo hilo.
Aidha, amesema wabunge wa chama chake wataendelea kutoka katika vikao vya Bunge iwapo vitaendelea kuwa vinajadili na kutaka kupitisha kile alichokiita “uzembe”.
Alisema hayo alipohutubia mkutano wa hadhara mjini hapa jana, ikiwa ni sehemu ya operesheni ya chama hicho katika mikoa ya Nyanda za Juu Kusini, inayolenga kuishinikiza serikali kusikia kilio cha wananchi, ukiwamo umaskini na hali ngumu ya maisha.
Alisema wana-Chadema hawana budi kuhakikisha wanawashawishi wanaCCM kuhakikisha wanalinda maslahi ya nchi, badala ya kupigana, kwani Chadema inawahitaji wanachama wa vyama vyote, kuungana pamoja katika kutetea maslahi ya Watanzania wote.
Mbowe, ambaye pia ni Mbunge wa Hai na Kiongozi wa Kambi ya Upinzani Bungeni, alisema wamekuwa wakifanya kazi ya ziada kuwazuia wana-Chadema kuwashambulia wana CCM ili kufikia lengo hilo.
Alisema sababu kubwa ya Watanzania kuwa maskini, ni sera mbovu.
Mbowe alisema hadi Baba wa Taifa, Hayati Mwalimu Julius Nyerere anaondoka madarakani, serikali yake ilikuwa ikikusanya kodi ya Sh. bilioni saba kwa mwezi.
Alisema baadaye Rais Mstaafu, Ali Hassan Mwinyi, alipoingia madarakani alifungua milango ya biashara na kwa mwezi, serikali yake ilikuwa ikikusanya kodi ya Sh. bilioni 27 licha ya wakati huo wananchi kutozwa kodi ya maendeleo kati ya Sh. 2,000 hadi 3,000.
Mbowe alisema alipoingia madarakani Rais Mstaafu, Benjamin Mkapa, balaa ndipo lilipoanza.
Alisema Mkapa alilitangazia taifa kwamba, kutokana na sera za CCM, uchumi wa nchi (wakati huo) umekua na kwa sababu hiyo, serikali inafuta kodi za manyanyaso (kodi ya maendeleo).
“Watanzania walifurahi, wakaandamana. Lakini Mkapa hakuwaambia kwamba, serikali inapoondoa kodi, huanzisha chanzo kingine cha mapato ya serikali,” alisema Mbowe.
Hata hivyo, alisema serikali ya Mkapa ilibadili mfumo wa kodi kwa kuondoa kodi ya maendeleo na kuanzisha Kodi ya Ongezeko la Thamani (VAT), ambayo wananchi wengi hawajui kuwa ni kitu gani.
Alisema VAT, ambayo wananchi wanalipa katika biadhaa zote zinazouzwa, ndiyo chanzo cha ufisadi, ambapo fedha za walipakodi zimekuwa zikiondoka mikononi mwao (wananchi) na kwenda mikononi mwa vigogo wachache.
“Wanakusanya mabilioni, wanapeleka hazina, wanatumia kifisadi,” alisema Mbowe.
Aliongeza: “Kodi mnazolipa, Mkapa alipomaliza madaraka yake miaka kumi, alikuwa anakusanya bilioni 290 kwa mwezi.”
Alisema katika utawala wa sasa wa Rais Jakaya Kikwete, serikali inakusanya kodi ya Sh. bilioni 420 kila mwezi.
Aliwashangaa Watanzania kwa kuwa waoga wanapopandishiwa bei ya bidhaa tofauti na wenzao wa Zambia, ambao alisema bei ya mkate ikipandishwa wanaandamana kupinga.
“Sasa tunasema wakipandisha kodi, tutaandamana nchi nzima hadi kieleweke. Tunakwenda bungeni, nimemwambia Kikwete mkipandisha kodi tutaandamana nchi nzima,” alisema Mbowe.
Alisema katika uzinduzi wa Bunge, wabunge wa Chadema walipotoka katika kikao hicho cha Bunge wakidai Katiba mpya, serikali iliwabeza, wabunge wa CCM wakawabeza na Spika wa Bunge, Anna Makinda aliwabeza.
Kutoka na hali hiyo, alisema wabunge wa chama chake wataendelea kutoka katika vikao vya Bunge iwapo vitaendelea kuwa vinajadili na kutaka kupitisha kile alichokiita “uzembe”.
Alisema Chadema kama chama siasa, kitaendelea kupiga kelele ndani na nje ya Bunge, ikiwa ni pamoja na kuwashirikisha wananchi kuhakikisha rasilimali za nchi zinasimamiwa na kutumiwa vizuri.
Mbowe alisema miongoni mwa mambo hawataacha kuyapigia kelele ni pamoja kupanda kwa gharama za maisha.
Alisema umaskini wa Watanzania si mapenzi ya Mwenyezi Mungu, bali ni ufisadi, uzembe, uzembe wa baadhi ya viongozi wa CCM kutumia rasilimali za Watanzania kinyume cha matakwa yao.
Mbowe alisema watu wote wana hali ngumu ya maisha na kuhoji ulikotoka umaskini wa Watanzania.
Awali, Mbunge wa Mbozi Magharibi, David Silinde, aliwataka wananchi wa jimbo hilo, kutokubali kutishwa na mtu yeyote katika kipindi cha miaka mitano na kwamba, yuko tayari kufa na Chama Cha Mapinduzi (CCM) hadi dakika ya mwisho.
Alisema kuishi katika shida siyo kigezo cha kuurithi ufalme wa Mungu kama wanavyoamini CCM na kusema Chadema kitahakikisha kinaking’oa chama hicho kwa gharama yoyote.
Makamu Mwenyekiti wa Chadema Zanzibar, Said Issa Mohamed, alisema ujio wa anayedaiwa kuwa ni mmiliki wa kampuni ya Dowans Tanzania Limited, Alawi nchini ulikuwa ni mchezo wa kuigiza uliofanywa na serikali ili kuhalalisha malipo kwa Dowans na kusema Watanzania kamwe hawatakuwa tayari kuilipa kampuni ya Dowans Tanzania Limited.
Alisema siku 100 walizopewa makada wa CCM wanaotuhumiwa kwa ufisadi hazitoshi na kusema kama serikali imeshindwa kuwapeleka vigogo wa ufisadi mahakamani, Chadema ikiingia madarakani itawashughulikia.
Alisema madai kwamba, Tanzania ni nchi maskini, hayana ukweli wowote, kwani hakuna kiongozi wa serikali, ambaye hutibiwa katika zahanati za nchini na pia hakuna, ambaye watoto wake wanasoma katika shule za kata.
Mohamed alisema ufisadi unapokithiri, nchi huingia katika majanga, kwani tatizo hilo halina tofauti na maradhi ya ukimwi, ambao huangamiza.
Alisema serikali iliwahi kusema hakutakuwa na mgawo wa umeme na kushangaa kusikia tena Shirika la Umeme Tanzania (Tanesco) likiutangazia umma kwamba, kuna mgawo mwingine unakuja na kuhoji kama hali hiyo kama si ufisadi ni nini?
Mkurugenzi wa Ulinzi na Usalama wa Chadema, Wilfred Lwakatare, alisema CCM itake isitake ifikapo mwaka 2015 ndiyo itakuwa mwisho wa uhai wake.
Alisema wamedhamiria kuwafikia wananchi katika kila eneo waliko ili kuona jeuri ya CCM inakotoka.
Leo ni siku ya mwisho ya operesheni katika mkoa wa Mbeya. Operesheni hiyo itaendelea katika Mkoa wa Rukwa leo, kabla ya kuendelea katika mikoa ya Ruvuma na kuhitimishwa katika Mkoa wa Iringa.
CHANZO: NIPASHE
No comments:
Post a Comment