ANGALIA LIVE NEWS

Thursday, May 19, 2011

Mechi ya Simba, Wydad kupigwa Misri

Mechi ya raundi ya tatu ya michuano ya Ligi ya Klabu Bingwa Afrika kati ya wawakilishi wa Tanzania Bara, Simba dhidi ya Wydad Casablanca ya Morocco itachezwa kwenye uwanja wa PetroSport Mei 28 jijini Cairo, Misri.
Kwa mujibu wa taarifa iliyotolewa jana na Shirikisho la Soka la Afrika (CAF), kila timu itatakiwa kujigharamia usafiri wa kwenda na kurudi nchini kwao pamoja na malazi wakiwa nchini humo, ambapo matokeo ya mechi hiyo moja tu kati yao ndiyo yatakayoamua nani atinge hatua ya 8-Bora ya ligi ya klabu bingwa Afrika.

Taarifa ya CAF imeeleza zaidi kwamba endapo dakika 90 zitamalizika na mshindi hatapatikana, timu hizo zitaenda katika hatua ya matuta.
Iliongeza kwamba wenyeji wa mechi hiyo ambayo ni Chama cha Soka cha Misri (EFA), watakuwa na jukumu la kuwaandalia hoteli za kufikia.
CAF imeeleza vilevile katika taarifa yake kwamba, gharama za waamuzi na kamisaa wa mechi hiyo zitabebwa na timu hizo mbili kupitia vyama vya soka vya nchi zao, Shirikisho la Soka Tanzania (TFF) na wenzao wa Morocco (FRMF).
Taarifa hiyo iliongeza kuwa gharama zozote ambazo EFA itaingia, zitarejeshwa na vyama vya nchi zinazotoka Simba na Wydad Casablanca huku mapato ya mechi hiyo pia yatagawanywa kwa klabu hizo mbili na yatapokelewa kupitia vyama vyao.
Simba ilikuwa imeshatolewa katika mashindano hayo ya kimataifa kwa kufungwa jumla ya mabao 6-3 na waliokuwa mabingwa watetezi, klabu ya TP Mazembe ya Jamhuri ya Kidemokrasia ya Kongo huku Wydad wakilizwa pia na Mazembe kwa kipigo cha jumla ya mabao 2-1. Hata hivyo, CAF ilizirejesha Simba na Wydad kwenye michuano hiyo baada ya Simba kushinda rufaa waliyokata dhidi ya Mazembe waliomchezesha bila kufuata utaratibu mchezaji Janvier Besala Bokungu waliyemtwaa kutoka klabu ya Esperance ya Tunisia.
Katika kujiandaa na mechi hiyo ambayo mshindi atacheza hatua ya makundi ya michuano hiyo, Simba ilianza mazoezi Jumatatu ikiwa chini ya kocha wake mpya, Mganda Moses Basena na wachezaji 18 walijitokeza katika siku ya kwanza.
Makamu Mwenyekiti wa Simba, Geofrey Nyange 'Kaburu', alisema jana kuwa kwa upande wa uongozi, kila kitu kiko tayari na watakachosikiliza ni maelekezo ya kocha wao.
Alisema kuwa kama walivyokwenda mjini Lubumbashi kuivaa TP Mazembe, hivi sasa wanatarajia pia kukodisha ndege ya serikali ili kuelekea Cairo katika siku ambayo kocha wao ataipanga.
Mara ya mwisho Simba kufika hatua ya 8-bora ya michuano hiyo ilikuwa mwaka 2003 wakati walipokuwa chini ya kocha wa kimataifa kutoka Kenya, James Siang'a na kuwang’oa waliokuwa wakitetea ubingwa, klabu ya Zamalek ya Misri.
CHANZO: NIPASHE

No comments: