ANGALIA LIVE NEWS

Thursday, May 19, 2011

Tanzania moja bei ya sukari toka Sh. 1,700 hadi 2,500

Baadhi ya wakazi wa vijiji vilivyopo kando kando ya Ziwa Nyasa, Wilaya mpya ya Nyasa mkoani Ruvuma, wameiomba serikali kupitia Wizara ya Viwanda na Biashara kuona umuhimu wa kuwaruhusu wafanyabiashara wa hapa nchini kununua sukari nchini Malawi na kuingiza kuuza nchini.
Wamesema lengo la ombi hilo ni kupunguza tatizo la uhaba wa sukari ambao umesababisha bei ya bidhaa hiyo kupanda kati ya Sh. 2,000 na 2,500 kwa kilo katika vijiji vyao.

Wakizungumza kwa nyakati tofauti na NIPASHE, baadhi ya wakazi wa vijiji vya Kilosa, Ndengere, Chinula, Zambia, Lundo na Liuli, walisema kutokana na sukari ya Tanzania kutopatikana katika maeneo yao, hulazimika kutumia sukari ya kutoka Malawi ambayo huingizwa nchini na wafanyabiashara kwa njia za panya na kusababisha kuuzwa kwa bei kubwa.
Hamis Yusuf, mkazi wa kijiji cha Kilosa, alisema kwa muda mrefu sukari wanayoitumia kijijini kwao hutoka nchini Malawi ambayo kilo moja huuzwa kati ya Sh. 2,000 na Sh. 2,500 wakati serikali hivi karibuni iliagiza bidhaa hiyo iuzwe kwa bei ya Sh. 1,700 kwa kilo moja.
Rehema Challe, mkazi wa mji mdogo wa Mbamba bay, alisema kama mipaka ingeruhusu kuvusha sukari kutoka Malawi, basi bei ya bidhaa hiyo ingeuzwa kati ya Sh. 1,200 na 1,500 kwa kilo moja.
Challe alisema sukari ya Tanzania katika mji mdogo wa Mbamba bay haijawahi kuletwa kwa muda mrefu wala kuonekana na kuimba serikali kupitia Wizara ya Viwanda na Biashara, ichukue uamuzi wa haraka wa kutoa vibali vya kusafirisha bidhaa hiyo kutoka nchini Malawi ili kupunguza kero inayowakabili wakazi wa maeneo ya mwambao mwa Ziwa Nyasa.
Naye John Katumbi, mkazi wa kijiji cha Ndengere, alieleza kuwa sukari imekuwa ikiadimika sana hasa kati ya Desemba na Aprili ambayo ndiyo kipindi cha Kiwanda cha Sukari nchini Malawi kusafisha mashamba ya miwa na kukifanyia ukarabati.
Alisema kutokana na hali hiyo, kiwanda hicho husimamisha uzalishaji wa sukari na kusababisha uhaba mkubwa wa sukari katika vijiji vilivyopo kando kando ya Ziwa Nyasa.
Mwenyekiti wa Serikali ya Kijiji cha Mbamba bay, Fidelis Duwe, alipohojiwa na NIPASHE kuhusiana na kero inayowakabili wakazi wa vijiji hivyo, altihibitisha kuwa sukari huuzwa kwa bei kubwa kutokana na wafanyabiashara kuipata kwa njia zisizo za halali.
Hata hivyo, alisema iwapo sukari hiyo ingeruhusiwa kuingiZwa nchini kwa njia halali, bila shaka itauzwa kwa bei ya chini.
Alisema nafuu hupatikana pale meli ya MV Songea inapofika Mbamba bay ikitokea Itungi Kyela mkoani Mbeya na kuelekea Nkata Bay nchini Malawi.
Alisema meli hiyo hufika Mbamba bay mara mbili kwa mwezi.
Alieleza kuwa wakazi wa kijiji hicho kwa muda wote hutumia sukari ya kutoka nchini Malawi ambayo pia huuzwa kwa bei kubwa.
Baadhi ya wafanyabiashara wa mji mdogo wa Mbamba bay ambao waliomba majina yao yasitahwe, waliiambia NIPASHE kuwa sukari ya kutoka Malawi huletwa Mbamba bay kwa kutumia boti kuwakwepa maafisa forodha wa Mamlaka ya Kodi nchini (TRA).
Kwa upande wake, Mkuu wa Wilaya ya Mbinga, Kanali Mstaafu Edmund Mjengwa, alithibitisha sukari kuuzwa kwa bei kubwa lakini akasisitiza kwamba jambohilo linafanyiwa kazi.
Mbunge wa Mbinga Magharibi, Kapteni John Komba, alisema kilio hicho cha wananchi cha kuuziwa sukari kwa bei kubwa ni cha muda mrefu lakini tayari alifanyia kazi kwa kuwasiliana na Waziri wa Viwanda na Biashara ambaye wakati wowote atatoa majibu ambayo yatakuwa ni faraja kwa wakazi wa vijiji vilivyopo kando kando ya Ziwa Nyasa.
CHANZO: NIPASHE

No comments: