ANGALIA LIVE NEWS

Monday, May 9, 2011

Mkulo-Zitto muongo, anapotosha, mzomeeni

WAZIRI wa Fedha, Mustafa Mkulo amewataka Watanzania ikibidi kumzomea Naibu Kiongozi wa Upinzani Bungeni, Kabwe Zitto kwa kuzungumza uongo na uzushi bila kuwa na uzalendo kwa Taifa lake huku akisisitiza kwamba Serikali ina fedha za kutosha kuendesha nchi. 

Akizungumza na waandishi habari mjini Dodoma jana, Mkulo alimshangaa Zitto kwa kudai hadharani kuwa Serikali imeshindwa kulipa mishahara na posho za wabunge, wakati yeye alikuwa mmoja wa waliolipwa tangu Aprili 22, mwaka huu.

"Napenda kuwafahamisha kuwa kwa Aprili mwaka huu, fedha za mishahara ya waheshimiwa wabunge zilitolewa Aprili 22 na fedha kwa ajili ya posho mbalimbali za wabunge nazo zimeshatolewa kwenye Ofisi ya Bunge," alisema Mkulo.
 

Alisema hata Katibu wa Bunge, Dk. Thomas Kashililah ameshangazwa na kauli hiyo. 

Jumamosi iliyopita katika mkutano wa hadhara mkoani Mbeya, Zitto alinukuliwa akisema Serikali ya Rais Jakaya Kikwete imefilisika, na kwamba, sasa inakopa katika benki kwa ajili ya kulipa mishahara ya watumishi, wakiwemo wabunge na posho zao. 

Kwa mujibu wa vyombo vya habari vilivyomkariri, Zitto ambaye ni Mbunge wa Kigoma Kaskazini (Chadema), alidai kuwa hata yeye alikuwa hajapata posho zake kama Mbunge kwa kuwa Serikal ilikuwa ikihangaika katika benki za ndani kupata fedha hizo. 

Lakini Mkulo jana alisema: "Napenda kukanusha vikali madai hayo, ni uongo mtupu na upotoshaji unaofanywa kwa makusudi kwa lengo la kujitafutia umaarufu wa kisiasa.” 

"Taarifa hizo si sahihi. Serikali inalipa watumishi wake mishahara kwa kutumia mapato yake ya ndani na pia ina uwezo wa kugharamia shughuli zake nyingine pamoja na gharama za kuendesha Bunge," alisema Mkulo aliyefuatana na Kamishna Mkuu wa Mamlaka ya Mapato Tanzania (TRA), Harry Kitilya ili kuthibitisha kuwa madai ya Zitto ni 'siasa chafu', Mkulo alieleza mapato ya Serikali tangu Desemba mwaka jana mpaka Aprili na kiwango kinachobakia baada ya kulipa mishahara ya watumishi wote. 

Kwa mujibu wa Mkulo, Desemba mwaka jana, Serikali ilikusanya Sh bilioni 594 na kati ya hizo, Sh bilioni 243.8 zilitumika kulipa mishahara na Serikali ikabakiwa na Sh bilioni 350.20 kwa ajili ya matumizi mengine. 

Mkulo alisema Januari mwaka huu, Serikali ilikusanya Sh bilioni 433.50, mishahara Sh bilioni 240 na baki Sh bilioni 193; Februari makusanyo Sh bilioni 430.40, mishahara Sh bilioni 266.70, ziada Sh bilioni 163.70; Machi makusanyo Sh bilioni 567, mishahara Sh bilioni 249 na ziada Sh bilioni 317.60. Alisema kwa utaratibu wa Serikali, mapato ya Machi ndiyo yaliyolipia matumizi ya Aprili na katika mwezi huo, baada ya kulipa mishahara, Serikali ilibaki na Sh bilioni 317 za matumizi mengine. 

Kwa Aprili, Mkulo alisema, tayari Serikali imeshakusanya Sh bilioni 432 zitakazotumika kulipa mishahara ya mwezi huu iliyo tayari, itakayoigharimu Serikali Sh bilioni 246.70 na baki kwa matumizi mengine itakuwa Sh bilioni 185.40. 

Kuhusu mabadiliko ya matumizi ya fedha za mishahara, yaliyoonekana kuongezeka kuwa makubwa na kupungua mwezi hadi mwezi, Waziri Mkulo alifafanua kuwa inatokana na malimbikizo ya madeni ya watumishi. 

Alitoa mfano wa matumizi ya mishahara ya Februari iliyokuwa Sh bilioni 266.70, ambayo ni kiwango kikubwa na kuongeza kuwa kilitokana na malipo ya malimbikizo ya nyongeza ya mishahara iliyotolewa mwishoni mwa mwaka jana. 

Mkulo alihoji uzalendo wa Zitto kwa Taifa na kufafanua kuwa kauli yake hiyo ni kubwa na gharama yake ni pamoja na kutishia wafadhili kusitisha misaada kwa ajili ya maendeleo ya wananchi wakidhani kuwa itatumika kulipia mishahara na kuendeshea magari. 

Alipohojiwa kuhusu kauli ya Shirika la Fedha la Kimataifa (IMF) iliyotolewa hivi karibuni kuwa Serikali inapaswa kulipa mishahara kwa ajili ya matumizi yake ya kawaida, kama ilisababisha Zitto kutoa kauli hiyo, Mkulo alisema IMF walitoa tahadhari kwa kuwa Tanzania imekopa kwa ajili ya shughuli za maendeleo. 

Alifafanua kuwa IMF yenyewe ilishafanya uchambuzi wa mikopo ya Tanzania na kubaini inadhibitika na kutoa taarifa kuwa Serikali inayo fursa ya kuendelea kukopesheka hata katika taasisi zinazotoa mikopo ya kibiashara. 

Alibainisha kuwa, mkopo wa Tanzania ni chini ya asilimia 30 ya pato la Taifa wakati katika nchi nyingine mkopo ni asilimia 70 ya pato la Taifa. 

Alisisitiza Serikali inakopa kuchochea uzalishaji ambao utaongeza mapato na kuijengea uwezo zaidi wa kulipa madeni. Kuhusu mkopo huo wa Benki ya Dunia, alisema Tanzania imekopa dola milioni 525 ambazo baadhi zimeshapatikana na zitatumika katika ujenzi wa barabara, kununua mtambo wa umeme wa megawati 100 wa Dar es Salaam na mwingine wa megawati 60 wa Mwanza.


CHANZO:HABARI LEO

No comments: