ANGALIA LIVE NEWS

Wednesday, May 11, 2011

Mmeachana, unataka kurudiana naye? – 2

NAWASHUKURU wote mlionitumia meseji za pongezi baada ya kuandika sehemu ya kwanza ya mada hii wiki iliyopita. Naamini somo lilieleweka vyema. Mlioomba ushauri, baadhi yenu niliwajibu na nitaendelea kufanya hivyo kwa kadiri muda utakavyoniruhusu.

Karibuni katika sehemu ya mwisho, ambayo naamini itakuacha na kitu kipya katika ufahamu wako wa mapenzi. Nazungumzia juu ya kurudiana na mpenzi uliyeachana naye.

Kama utakumbuka vizuri, wiki iliyopita nilianza kwa kueleza kwanza kuchunguza mahali mwenzi wako alipo na kupeleleza historia yake kiuhusiano. Sasa tunaendelea na vipengele vingine muhimu zaidi.

MAWASILIANO
Ukishachunguza mahali alipo na ukaridhika na historia yake ya kimapenzi baada ya kuachana na wewe, sasa unatakiwa kutafuta mawasiliano yake. Kama unayo ni vyema, lakini kama huna unatakiwa kusaka.

Kuwa na mawasiliano naye ni hatua ya kwanza, kingine kitakachofuata baada ya hapo ni kujenga mawasiliano. Hapo sasa inategemea na namna mlivyoachana, lakini kama hamkuwa na ugomvi mkubwa sana, basi unaweza kumtumia meseji za ‘kichokozi’ mara nyingi uwezavyo kwa siku.

Majibu yake ndiyo yatakayokupa mwanga wa kuendelea na kipengele kingine. Kikubwa hapa ni kutozungumzia kabisa mambo ya mapenzi, badala yake iwe ni kumjulia hali na utani wa hapa na pale.

MWALIKE
Baada ya kutengeneza mawasiliano naye, sasa unatakiwa kumwalika katika shughuli mbalimbali za kifamilia na binafsi. Mathalani umepata mwaliko wa kwenda kwenye sherehe au hafla fupi ya usiku, omba kampani yake.

Kama mtu mzima atagundua kitu kilichopo moyoni mwako. Hata kama atakuwa mwenye moyo wenye kutu, kutoka naye mbele za watu, kutamfanya akumbuke ‘enzi zile’ mlipokuwa mkitoka pamoja, hivyo kufikiria kurudi tena kwako.

Ikiwa yeye mwenyewe ataamua kukuambia kwamba anaona mrudiane litakuwa jambo zuri zaidi, maana atakuwa amekurahisishia, lakini akinyamaza, basi njia inayofuata hapa chini ni muafaka kwake.

MSOGEZE KARIBU
Sasa unatakiwa kumsogeza karibu zaidi na wewe. Lazima afahamu kwamba, kuna kitu fulani kipo ndani ya moyo wako. Meseji zako zibadilike, kama ulikuwa unamwandikia, “Salama Juma?” au “Mambo vipi Suzan?”,  sasa unatakiwa kubadilisha hadi “Niambie sweetie, uko poa?”

Meseji za aina hiyo zitamfanya aone tofauti na inawezekana kabisa akagundua kwamba upo kwenye mawindo ya kumrudisha tena kwako. Katika hatua hii katu hutakiwi kufungua mdomo wako kumwambia kuwa unataka kurudiana naye na badala yake unatakiwa kuacha vitendo vizungumze vyenyewe.

MTOKO MAALUM
Kutokana na ukaribu wenu, kumwalika katika mtoko maalumu kama wa chakula cha mchana au usiku, haitakuwa vigumu kwake. Hiyo itakuwa njia nyingine ya kumfanya awe karibu yako zaidi.

Mkiwa katika mtoko huna haja ya kuzungumza chochote kuhusu uhusiano wenu, labda kama yeye ataanzisha mjadala huo. Ongelea mambo mengine ambayo ni maarufu zaidi labda katika duru za siasa, sanaa n.k lakini si mambo yanayohusu mapenzi kabisa.

Kama kichwani mwake alikuwa amekufanya kama rafiki yake wa kawaida, mtazamo utaanza kubadilika taratibu na kuanza kutamani kurudi tena mikononi mwako. Jaribu kufikiria, kama umetoka naye, akiamini labda unataka kumuomba msamaha na kurudiana naye, wewe unaanza stori za Ligi za Ulaya!
Bila shaka atajiona kama mpumbavu kichwani, si ajabu akaamua kujifunga mwenyewe kwa kuomba urudi tena kwake.

ZUNGUMZIA UHUSIANO WENU
Hatua hii ndiyo muhimu zaidi hapa; sasa unatakiwa kuanza kuzungumzia juu ya uhusiano wenu. Mwambie jinsi ulivyokuwa ukifurahishwa na mapenzi yenu. Msifie alivyokuwa anajua majukumu yake na kukuonesha mapenzi ya dhati.

Si vibaya kama utamweleza pia sababu ambazo unahisi zilisababisha wewe na yeye kuachana. Kwa kauli hizo, utampa nafasi ya kuchambua/kumjua mwenye makosa na mahali pa kurekebisha.

JUTIA MAKOSA YAKO
Ikiwa kuna mahali unaamini ulienda kinyume na yamkini ndiyo sababu kuu iliyosababisha muachane, tujia makosa yako mbele yake. Mweleze kwamba wewe ndiyo chanzo cha matatizo na huenda kama si kukosea, msingeachana.

Kujutia hasa kama uso wako utawakilisha vyema kilicho moyoni mwako, kutamfanya akuone muungwana ambaye unatambua ulipojikwaa na sasa unataka kurekebisha makosa yako. hapo utakuwa na nafasi kubwa ya kumnasa kwa mara nyingine.

OMBA USAJILI MPYA
Hapa huna haja ya kuendelea kujitesa, FUNGUKA! Sema moja kwa moja kilichopo moyoni mwako. Kwamba unahitaji nafasi nyingine kwake, maana umeshajua makosa yako.
Kama utakuwa umefuata kwa makini vipengele vyote hapo juu, lazima urudi tena mikononi mwake. Pumua kwa kasi, kisha jipongeze, lakini chunga sana, usiharibu tena!

Joseph Shaluwa ni Mshauri wa Mambo ya Mapenzi anayeandikia magazeti ya Global Publishers, ameandika vitabu vya True Love na Let’s Talk About Love. Unaweza kumtembelea kwenye mtandao wake;www.shaluwanew.blogspot.com au jiunge naye kwenye facebook.

No comments: