ILIKUWA ikijulikana kama Uwanja wa Huba, sasa ni All About Love, ikiwa ni maboresho madogo ya kona hii, lengo likiwa ni kukuongezea ‘taste’ katika kukupa kile unachokipenda. Karibuni sana marafiki.
Yes! Leo naongea na wenzi ambao walikuwa pamoja kwa muda mrefu wakaachana, lakini sasa mmoja wao anahisi kurudiana na mwenzake. Ndugu zangu, kuachana ni sehemu ya uhusiano (hasa ule usio na ndoa).
Yes! Leo naongea na wenzi ambao walikuwa pamoja kwa muda mrefu wakaachana, lakini sasa mmoja wao anahisi kurudiana na mwenzake. Ndugu zangu, kuachana ni sehemu ya uhusiano (hasa ule usio na ndoa).
Kugombana ni kawaida kabisa kwa wapenzi, inawezekana ulikuwa na mpenzi wako, lakini kwa bahati mbaya kukatokea kutoelewa, mwisho mkaishia kuachana. Baada ya kuwa nje ya uhusiano huo kwa muda mrefu, sasa unahisi kwamba unamuhitaji, lakini hujui pa kuanzia.
Wengi hushindwa namna ya kufanya ili kuweza kumnasa tena mpenzi wa zamani. Baadhi yao huenda mbali zaidi, wakifikiria kuwa huenda wakaonekana hawana thamani au hawana ujanja ndiyo maana wanataka kurudi, jambo ambalo si la kweli.
NI SAHIHI KURUDIANA?
Mawazo mgando ya baadhi ya watu huamini kwamba kurudi kwa mara nyingine kwa mpenzi wa zamani ni kujidhalilisha, kujishusha na kujisalimisha. Kwamba hakuna mwanaume wala mwanamke mwingine yeyote atakayeweza kuwa naye tofauti na huyo anayemrudia.
Jambo hilo si la kweli hata kidogo, kikubwa cha kuzingatia hapa ni moyo; je, unahisi bado unampenda? Ni kweli naye anakupenda? Kama sifa hizi zipo, hayo mambo madogo ambayo mmetofautiana ni ya kawaida kabisa ambayo mnaweza kurekebishana taratibu.
Kwa msingi huo basi, hakuna tatizo lolote katika kurudiana na mpenzi wako wa zamani, maana tayari unakuwa umeshamjua vya kutosha, hivyo kukupa urahisi wa kufanya yale anayoyapenda na kuepuka asiyopenda jambo litakalozidisha umri wa uhusiano wenu, si ajabu mkaingia kwenye ndoa.
FAIDA ZA KURUDIANA
Katika utafiti usio rasmi nilioufanya wakati naandaa mada hii, niligundua kwamba zipo faida za kurudiana na mpenzi mliyeachana, lakini kikubwa ni awe moyoni mwako.
Asbert Ndesanjo (32), mfanyakazi wa kampuni moja jijini Dar, alisema kurudiana na mpenzi wa zamani ni jambo jema, kwani linakomaza uhusiano.
“Unajua kaka Shaluwa, kumrudia mtu wako wa zamani maana yake ni kwamba umekubaliana na udhaifu wake wote. Unajua anachopenda na anachochochukia, hapo lazima mtadumu. Bila kudanganya, mke wangu wakati wa urafiki wetu, tukiwa na miaka miwili kwenye uhusiano tulitibuana tukaachana.
“Kila mmoja alikaa kivyake kwa miezi kama sita au saba hivi, nikakutana naye Dar, nikiwa nimeachana naye Arusha, nikamwita tukakaa na kuzungumza, miezi minne mbele yake tukapanda madhabahuni kufunga ndoa, mimi naona sawa tu,” alisema Ndesanjo.
UNATAKA KURUDIANA NAYE?
Je, wewe ni mmoja kati ya walioachana na wapenzi wao? Bado unapenda na unatamani kurudiana naye? Rafiki yangu si ngumu kama ambavyo unaweza kufikiria.
Baadhi ya watu huanza kufikiria namna ya kurudi kwa mpenzi wake wa zamani wakiwa na woga mkubwa ndani ya mioyo yao. Hapa kwenye All About Love ipo dawa. Unaijua? Soma hapo chini.
CHUNGUZA ALIPO
Kitu cha kwanza kabisa ambacho unatakiwa kuchunguza ni mahali anapopatikana kwa wakati huo, nasema hivyo kwa sababu yawezekana alihama makazi, kikazi n.k. Kujua anapopatikana ni mwanzo wa kuelekea kwenye mafanikio ya kumkamata katika himaya yako.
HISTORIA YAKE KIUHUSIANO
Lazima ujue kuhusu historia yake kiuhusiano baada ya kuachana na wewe ilivyokuwa. Hapo unatakiwa kufanya ‘ushushushu’ wako kimya kimya bila yeye kujua. Ikiwa ameshafanya ‘vurugu’ sana, maana yake ni mtu asiye na msimamo na huenda anaongozwa zaidi na tamaa za kimwili na si mapenzi.
Katika kipengele hiki, ni muhimu sana kujua kama muda huo ambao wewe unahitaji kurudi tena mikononi mwake kama ana uhusiano mwingine. Kimsingi kama atakuwa ndani ya uhusiano, itakubidi uhairishe kurudi kwake.
Kwanini? Kwa sababu kwanza, anaweza kukubali kuwa na wewe wakati akiwa bado hajaachana na mpenzi aliyenaye kwa muda huo, hivyo kuwa kama mwizi tu kwa mwenzako. Kubwa zaidi ni kwamba, utakuwa katika mapenzi ya kushea, jambo ambalo si zuri kisaikolojia na hata kiafya.
Bado kuna mengi ya kujifunza rafiki zangu, wiki ijayo tutaendelea ambapo tutaona kwa mapana njia za kutumia ili uweze kurudi mikononi mwa mpenzi wako wa zamani.
HADI WIKI IJAYO
Joseph Shaluwa ni Mshauri wa Mambo ya Mapenzi anayeandikia Magazeti ya Global Publishers, ameandika vitabu vya True Love na Let’s Talk About Love. Unaweza kumtembelea kwenye mtandao wake; www.shaluwanew.blogspot.comau jiunge naye kwenye facebook.
No comments:
Post a Comment