ANGALIA LIVE NEWS

Monday, May 2, 2011

Moto wawaka Chadema, NI VITA YA KAMBI ZA MBOWE, ZITTO

Mbunge wa Kogoma Kaskazini na Naibu kiongozi wa Kambi ya Upinzani Bungeni Zitto Kabwe
Ramadhan Semtawa
VITA vya makundi vimezidi kuviandama vyama vikubwa vya siasa nchini, ambapo sasa hali si shwari ndani Chadema, ambako kunadaiwa kuwepo mkakati wa kumng'oa Naibu Katibu Mkuu wa chama hicho, Zitto Kabwe.
Kabwe ambaye pia ni Mbunge wa Kigoma Kaskazini na Naibu Kiongozi wa Upinzani Bungeni, anadaiwa kuponzwa na msimamo wake kupinga ununuzi wa magari mitumba yenye thamani ya Sh480 milioni ya Chadema.

Hali hiyo ilijitokeza katika kikao cha Kamati Kuu ya Chadema kilichoketi juzi Jumamosi chini ya Mwenyekiti wa Chadema Taifa, Freeman Mbowe, kikao ambacho pia kilimg’oa John Shibuda katika nafasi ya kukaimu uenyekiti mkoa wa Shinyanga.Shibuda ambaye ni mbunge wa Maswa Magharibi ameondolewa baada ya kukalia nafasi hiyo takriban kwa siku nne tu tangu ateuliwe, kufuatia kifo cha aliyekuwa mwenyekiti wa Chadema mkoani Shinyanga Philip Shelembi ambaye alizikwa April 27, 2011.


Chanzo cha mvutano
Habari kutoka ndani ya kikao hicho cha Kamati Kuu na kuthibitishwa na baadhi ya wajumbe wa kikao hicho zinasema kuwa mbunge wa Arusha mjini, Godbless Lema, ndiye alianzisha mvutano wa kutaka Zitto ang'olewe kutokana na kupinga wazo la kununua magari chakavu kutoka India.

Chanzo chetu cha uhakika kilidokeza kuwa mashambulizi dhidi ya Zitto yalianza pale alipounga mkono hoja ya Profesa Mwesiga Baregu na Dk Kitila Mkumbo ambao walinukuliwa wakisema kwamba, isingekuwa sahihi kwa chama hicho kinachopinga ufisadi kufanya ufisadi kwa kununua magari chakavu wakati wamekuwa wakiibana serikali isifanye hivyo.

Baada ya Zitto kuunga mkono hoja hiyo, vyanzo hivyo nifafanua kuwa ndipo vurugu zilipoanza kwani Lema alianza kumrushia vijembe akisema kwamba Zitto ni tatizo na kwamba amekuwa akimtetea Shibuda.

Habari zinasema baadhi ya wajumbe walisema hoja ya Lema haikuwa na nguvu ya kumshutumu Zitto kwani Shibuda ni mbunge halali wa Chadema.

Duru zaidi za kisiasa kutoka ndani ya kikao hicho  zinasema wakati mvutano huo ukiendelea, Katibu Mkuu wa Chadema, Dk Willibrod Slaa alikuwa kimya huku kwa mara ya kwanza Mbunge wa Ubungo, John Mnyika akiwa mmoja wa wajumbe waliomtetea Zitto.

"Wakati Lema akisema hivyo, Dk Slaa wakati wote alikuwa kimya na hakusema chochote. Mnyika alisimama na kumtetea Zitto kwa mara ya kwanza, na katika utetezi pia alikuwepo Grace Kiwelu," kiliweka bayana chanzo hicho.

Katika majibizano hayo inadaiwa  ulifika wakati Zitto alisimama na kumwambia mwenyekiti wa chama hicho, Freeman Mbowe, kwamba mpango mkakati wake huo wa kujenga mtandao utakuja kumgharimu katika siku za usoni."Zitto alimwambia Mbowe mpango wake huo wa kujenga mtandao ungekuja kumletea matatizo hapo baadaye, "kilisema chanzo hicho kikimnukuu Zitto ndani ya kikao. 

Kung’olewa kwa Shibuda
Mbali ya Zitto, Kamati Kuu hiyo pia iliazimia kutengua nafasi ya Shibuda, kukaimu nafasi ya uenyekiti ya Chadema mkoa wa Shinyanga.Vyanzo hivyo viliongeza kwamba, kabla ya mpango huo genge linalompinga Zitto lilimshutumu kwamba alikwenda Shinyanga na kushirikiana na baadhi ya wanachama kumweka Shibuda ili kutimiza ajenda zao.

Mvutano huo unaondelea ndani ya Chadema unazidi kukiweka chama hicho kinachokua na kuwa na malengo ya kukamata dola katika wakati mgumu kutokana na makundi mawili, huku moja likimuunga mkono Zitto na jingine Mbowe.

Zitto na Shibuda ni viongozi ambao wamekuwa wakikumbwa na misukosuko ndani ya Chadema na mara kadhaa Zitto amenusurika kung'olewa katika nafasi zake za uongozi kutokana na kile kinachodaiwa ni hulka yake ya kutofautina na wenzake hata katika mambo yenye maslahi kwa chama hicho kikuu cha upinzani nchini.

Kauli za Zitto, Shibuda
Zitto alipoulizwa na Mwananchi jana jioni kuhusu tafrani hiyo alisema “….tafadhali sana, naomba nisiongee chochote kwa sasa, hiki ni kipindi cha kukijenga chama, si kipindi cha kuonyesha umma kwamba Chadema kuna mgogoro”.

Pale mwandishi alipomhoji zaidi alisema “…tafadhali naomba nikupigie baadaye” kisha kukata simuKwa upande wake Shibuda alikiri kusikia taarifa hizo na kuongeza kwamba, anasubiri apate taarifa rasmi kwani yeye alipewa heshima hiyo na wanachama wa Shinyanga kupitia vyombo vyao vya maamuzi.

CHANZO:MWANANCHI

No comments: