MKAZI wa Kijiji cha Mamba Lekura wilayani Moshi Vijijini, Dorini Shayo (60) ambaye alimsindikiza dada yake katika Kijiji cha Samunge wilayani Loliondo kupata dawa kwa Mchungaji mstaafu, Ambilikile Mwaisapile, amepotea kwa zaidi ya miezi miwili sasa.
Kwa mujibu wa taarifa iliyotolewa na mtoto wake, Deogratias Shayo, mama yake aliondoka nyumbani Machi 19, mwaka huu kumsindikiza dada yake, Ajenta Makundi ambaye alikuwa akisumbuliwa na maumivu ya miguu kwa muda mrefu.
Deogratias alisema, baada ya kupanga safari hiyo waliondoka wao wawili kwenda Samunge na walipofika, kutokana na wingi wa wananchi wanaofika kijijini humo nao walijipanga katika foleni ya kumuona Mwaisapile maarufu kama Babu wa Loliondo.
“Kwa mujibu wa maelezo ya Makundi, walipofika kwanza waliibiwa chakula chote walichokuwa nacho kwa ajili ya siku za kuishi kijijini humo, lakini waliishi kwa msaada wa wananchi wengine,” alisema.
Hata hivyo, alisema baada ya siku saba, Machi 25 saa moja asubuhi, walikaribia kupata kikombe, lakini mama yake aliteremka ndani ya gari walilokuwemo na kuelekea kusikojulikana mpaka sasa hajaonekana.
Alisema, ingawa juhudi kubwa zilifanyika za kumtafuta mama yake kwa kutumia njia mbalimbali kijijini Samunge, lakini hazijazaa matunda hata baada ya kurejea kijijini Mamba Lekura.
Aidha, kijana huyo aliomba wananchi kumsaidia kutoa taarifa katika kituo chochote cha polisi hususan katika Kijiji cha Samunge iwapo watabaini kumuona mama huyo akirandaranda au vinginevyo.
CHANZO:HABARI LEO
No comments:
Post a Comment