.jpg)
Wachezaji wa timu ya soka ya Tanzania, Taifa Stars, Nizar Khalfan kutoka Vancouver White Caps ya Canada, Abdi Kassim na Danny Mrwanda wanaocheza Vietnam hawatakuja kwa ajili ya mechi ya kirafiki ya Jumamosi dhidi ya Afrika Kusini 'Bafana Bafana' kwenye uwanja wa Taifa jijini Dar es Salaam.
Akizungumza jana, Afisa Habari wa Shirikisho la Soka Tanzania (TFF), Boniface Wambura, alisema kuwa Nizar amekataliwa na timu yake kutokana na kukabiliwa na mechi muhimu Jumapili huku pia Mrwanda na Kassim nao timu yao inawahitaji katika kuhakikisha wanapambana ili wasishuke daraja.
Wambura alisema kuwa taarifa kutoka katika timu hizo mbili zimewafikia juzi na jana asubuhi na wamezipokea kwa sababu wote wamejenga hoja kwamba mechi hiyo ya kirafiki ya kimataifa inachezwa siku ambayo haitambuliwi katika kalenda ya Shirikisho la Soka Duniani (FIFA).
Alisema kwamba bado TFF inasubiri majibu ya maombi ya wachezaji wengine ambao ni Idrissa Rajab wa Sofapaka ya Kenya, Henry Joseph (Norway) na Athumani Machuppa anayecheza soka la kulipwa nchini Sweden.
Alisema pia maandalizi ya mechi hiyo yanaendelea vizuri na tiketi kwa ajili ya mashabiki zitaanza kuuzwa kesho katika vituo mbalimbali jijini Dar es Salaam.
Alisema kwamba Bafana Bafana itawasili nchini kesho saa 1:30 usiku kwa ndege ya Shirika la Ndege la Afrika Kusini ikiwa na wachezaji 20 pamoja na viongozi 10.
Aliwataja wachezaji watakaokuja kuivaa Stars wakiongozwa na nahodha wao, Siphiwe Tshabalala wa klabu ya Kaizer Chiefs na kocha Pitso Mosimane, kuwa ni makipa Itumeleng Khune na Wayne Sandilands na mabeki Morgan Gould, Siyanda Xulu, Eric Matoho, Mzivukile Tom, Prince Hlela, Siyabonga Sangweni, Tefu Mashamaite na Siyanda Zwane.
Wachezaji wengine ambao ni viungo wanaokuja ni Hlompho Kekana, Thanduyise Khuboni, Reneilwe Letsholonyane, Thandani Ntshumayelo,Thabo Matlaba, Erwin Isaacs na Sifiso Myeni wakati washambuliaji ni Bernard Parker, Vuyisile Wana, Lehlohonolo Majoro na Katlego Mphela.
Stars itatumia mchezo huo kujiandaa na mechi yake ya kufuzu kwa fainali za Kombe la Mataifa ya Afrika dhidi ya Jamhuri ya Kati huku Bafana Bafana nao wakijiandaa na mchezo wao dhidi ya Misri, mechi zote zikifanyika Juni 3.
CHANZO: NIPASHE
No comments:
Post a Comment