ANGALIA LIVE NEWS

Tuesday, May 10, 2011

SUKARI: TAMU LAKINI INA UKWELI MCHUNGU-GPL

Inawezekana kabisa katika maisha yako hujawahi kusikia au kuambiwa kuwa sukari inaua, kwa sababu chakula chochote kizuri kikisifiwa kinaelezwa kuwa kitamu kama sukari. Wengine husema utamu wa chai ni sukari, ikiwa na maana bila sukari chai hainyweki.

Kuna mjadala mkubwa unaendelea hivi sasa katika ulimwengu wa wanasayansi wa masuala ya lishe wakati ushahidi ukiendelea kutolewa kuwa sukari ndiyo chanzo cha msingi cha magonjwa si ya unene tu, bali hata magonjwa mengine hatari kama saratani.


Imeelezwa kuwa, hivi sasa hakuna shaka tena kwamba sukari ni sumu kwa mwili wako, ni suala la muda tu linabaki kutangaza rasmi kuwa sukari nayo inasababisha saratani, kama inavyoelezwa uvutaji wa sigara husababisha saratani ya mapafu na unywaji wa pombe mbaya husababisha ugonjwa wa ini.

Daktari bingwa na mtaalamu wa masuala ya unene kwa watoto, Robert Lusting, ambaye pia ni Profesa wa Chuo Kikuu cha California, San Francisco, nchini Marekani ni miongoni mwa wataalamu wanaoongoza duniani kwa masuala ya watoto. Aidha, daktari huyu ndiye mwanzilishi wa kufanya utafiti kuhusu aina zote za sukari zinavyofanya kazi katika mwili wa binadamu.

Kwa wale wenye fursa ya mitandao ya internet, nawashauri watafute makala ya mtaalamu huyu kwenye mtandao wa You Tube ambako anaelezea kwa njia ya video. Ameeleza kwa kirefu sana kuhusu madhara yaletwayo na sukari katika mwili wa binadamu (search: Sugar: The Bitter truth).

Kwa mara ya kwanza katika historia ya mwanadamu, magonjwa yatokanayo na staili ya maisha, kama vile kisukari, presha, ugonjwa wa moyo na magonjwa ya saratani, ndiyo yanayoua watu wengi hivi sasa duniani kuliko magonjwa ya kuambukiza.

Nchini Marekani, inakadiriwa kuwa kiasi cha dola Trioni moja hutumika kila mwaka kutiba watu wanaosumbuliwa na magonjwa hayo, hii ina maana kwamba fedha hizo zingeweza kuokolewa kama watu wangeweza kujiepusha na magonjwa hayo kwa kubadili staili za maisha yao katika vyakula.

KWA NINI SUKARI NI HATARI KWA AFYA?
Baadhi ya wataalamu wa kisasa wanapingana na utafiti wa Dk. Lustings kwa madai kuwa sukari siyo mbaya katika mwili wa binadamu ikitumiwa kwa kiasi kidogo, hasa kwenye matunda na vyakula.

Lakini ukweli ni kwamba iwe sukari kidogo au nyingi, madhara ni yale yale kwa sababu ndani ya sukari kuna kirutubisho aina ya Fructose ambacho kinaelezwa kuwekwa kwenye sukari katika kiwango kingi kinyume na inavyotakiwa.

Laiti kwenye sukari kungekuwa na kiasi kidogo cha ‘fructose’ ambacho hakizidi gramu 25 kila mara mtu anapokula sukari, isingekuwa tatizo. Lakini inaelezwa kuwa mtu anapokula gramu 150 tu za sukari, (sawa na vijiko vitatu vya chai), huwa amezidisha kiwango cha fructose kinachotakiwa mwilini kwa asilimia 300!

Mahali ambapo ulipewa maelekezo ya kuweka chumvi kwenye chakula kiasi cha vijiko 25 ili iwe sawa, ukaweka vijiko 300, hicho chakula kitalika? Ikiwa kiasi cha sukari tunachotakiwa kuingiza mwilini kisizidi gram 25 kwa siku, sisi tunaweka 300, si ni hatari? Na hayo ni makadirio ya chini kabisa, kwa sababu kuna wengine wanatumia zaidi ya kiwango hicho.

Bila shaka madhara yatokanayo na sukari tunayotumia katika maisha yetu ya kila siku ni makubwa sana kinyume na tunavyofikiria. Tunatumia sukari nyingi mno kwenye chai, juisi, soda na vyakula vingine vingi.

Ikiwa sukari ndiyo chanzo cha matatizo ya unene, presha, saratani, magonjwa ya moyo na ugonjwa wa kisukari, tutawezaje kuyaepuka iwapo hatutaacha tabia ya kula sukari kwa wingi?

Itaendelea wiki ijayo…

No comments: