ANGALIA LIVE NEWS

Wednesday, May 25, 2011

UMIA MARA MOJA UUPE MOYO WAKO FURAHA YA KUDUMU-2

Mambo vipi marafiki? Mpo poa? Ni furaha yangu kama mtakuwa wazima. Karibuni tena katika uwanja wetu maalum kwa ajili ya kupeana darasa la maisha katika mapenzi. Siku zote hapa huwa nazungumza ukweli.

Ukweli ambao, umewasaidia wengi na maisha yao kuwa bora. Wamekuwa na maamuzi sahihi na hawajuti kuwa na wapenzi wao. Mada iliyopo mezani ni kama inavyosomeka hapo juu, ambapo leo tupo katika sehemu ya mwisho.


Tunajifunza jinsi ya kufanya uamuzi mgumu wenye maumivu kwa mara moja, halafu kujiwekea nafasi ya kudumu katika furaha ya uhusiano. Kipengele cha kwanza kilikuwa ni namna ulivyojipanga, leo tunaendelea...

Kuongozwa na hisia
Hapa rafiki zangu, lazima mtulize akili kung’amua hili sawa sawa, maana ndiyo kiini cha mada hii. Kwanza, fahamu kuwa, hisia na mapenzi ni vitu viwili tofauti, ingawa ili uwe na hisia lazima pia uwe na mapenzi.

Kwa maneno mengine, mtu mwenye mapenzi ya dhati ni rahisi zaidi kuongozwa na hisia kuliko mwenye hisia kupanda mbegu ya mapenzi ndani ya moyo wake!

Hisia katika mapenzi, tunaitafsiri kama ile hali ya kuingiwa na mapenzi ndani ya moyo na kupitiliza, pia kuzama katika penzi kiasi cha kuwa mpofu wa kutoweza kuona mbadala wake.

Mtu mwenye hisia kali za mapenzi kwa mwenzi wake, huwa haamini kama kuna mwingine ambaye anaweza kuwa kama yeye (huyo mpenzi wake), hali hii inasababisha kufunika makosa au matatizo yatakayotokea katika uhusiano huo hata kama ni makubwa.

Akibahatika kugundua, basi uulizaji wake unakuwa si wa kujiamini sana, lakini pia ni mwepesi kuyumbishwa au hata kuomba msamaha kwa kosa ambalo ni la mpenzi wake. Huyu tunamwita anayeongozwa na hisia!

Mwenye hisia zaidi kuliko mapenzi, yupo tayari kuishi maisha ya kubahatisha bila kuwa na mipango ya mbele, lakini awe na mpenzi wake. Huu ni ulimbukeni wa hali ya hali juu. Rafiki zangu, kifungo si lazima upelekwe gerezani, hata wewe unaweza kujiingiza katika kifungo cha mapenzi.

Usikubali kuendelea kuwa katika mapenzi na mtu ambaye unajua wazi ana kasoro kibao, kwa sababu eti unampenda! Hata kama unampenda kwa kiwango gani, lakini ndiyo hivyo si mwaminifu, mkorofi, hana heshima; utaendeleaje na mpenzi wa aina hii?

Lakini katika yote hayo, tatizo kubwa zaidi ambalo ni la hatari, ni ile hali ya kuwa na mwenzi ambaye si mwaminifu. Kutokana na kigezo chako cha kuangalia jinsi hisia zako zinavyokuongoza, wakati mwingine unaweza kusalitiwa lakini usijue au ukajua lakini ukaamua kuacha kwa kuhofia kumpoteza. Huu ni ulimbukeni rafiki yangu.

Katika suala la usaliti ni vizuri kuwa makini katika kufanya uchunguzi kwanza kabla ya kufanya maamuzi. Mathalani mpenzi wako amekuja, anaonekana amechoka-choka, hana furaha na uso wake si ang’avu kabisa! Tabasamu lake halipo na kwa kumwangalia tu usoni unagundua kwamba ana alama ya busu kwenye shavu lake! Wakati mwingine ananukia manukato ambayo siyo aliyoyatumia asubuhi.

Au anaweza kuja na furaha ya  kupitiliza, uchangamfu kupitiliza, kukukumbatia kwa muda mrefu zaidi kuliko kawaida yenu n.k.

Hizi ni dalili za wazi kabisa, kwamba kuna uwezekano huko alipotoka, ameharibu! Alama ya busu shavuni mwake, haina haja ya kuwa na maswali mengi maana tayari jibu utakuwa nalo.

Hivyo vingine ni hisia tu, lakini je, unatakiwa kuwa mkali kwake na kuleta ugomvi baada ya kuona dalili hizo? Hapana.....! Kipo kitu unachotakiwa kufanya.

Chunguza...
Ndiyo! Unatakiwa kwenda mbali zaidi ya hisia zako za kawaida zinavyokutuma, mchunguze! Awe mpole sana au mkali sana, lakini unatakiwa kumwambia akae chini na awe makini kukusikiliza!

Anza na sentesi hii: “Unajua mimi nina akili sana kuliko unavyofikiria? Ukifanya jambo lolote lazima nitajua....” ukifika hapo nyamaza kimya, kisha macho yako yatulize katikati ya macho yake bila kuyapepesa.

Utajifunza kitu!
Kama alifanya usaliti au alikuwa na mpenzi mwingine muda mfupi uliopita utajua tu. Uwoga wake, upole zaidi na kutoa macho sana au kuangalia chini kwa aibu ni tiketi yako ya kuelekea kwenye kuujua ukweli zaidi ambao anajaribu kukuficha.

Usiishie hapo, mnuse kama aina ya vipodozi alivyotumia asubuhi ndivyo anavyonukia kwa muda huo. Ni rahisi tu kugundua, maana wengi wao baada ya kumaliza kufanya mapenzi lazima wataingia bafuni, huko watakutana na sabuni nyingine, wakitoka watatumia mafuta mengine na hata manukato mengine. Lazima utaujua ukweli.

Mwamuzi wa mwisho ni wewe
Lazima ufahamu kwamba hisia zinaweza kukuongoza sawa na wakati mwingine kukuangusha, sasa unachotakiwa kufanya zaidi ni wewe kuwa mwangalifu kabla ya kuchukua hatua. Ikiwa baada ya kupitia vipengele vyote hivyo na ukagudua ni kweli penzi lako husalitiwa ni wakati wako wa kufanya uamuzi sahihi.

Uamuzi wa kwanza ambao ni sahihi zaidi ni kuzungumza naye, mweleze hali ilivyo mbaya kiafya na jinsi mnavyokuwa katika hatari ya kuelekea kwenye matatizo.

Kosa hili kama siyo mara ya kwanza litakuwa ni kubwa sana katika uhusiano wenu lakini anayejua thamani ya penzi lenu na jinsi mlivyokutana ni wewe, hivyo basi uamuzi wa kuachana au kuendelea naye upo mikononi mwako.
Upo? Ahsante kwa kunisoma. Hadi wiki ijayo kwa mada nyingine kali, USIKOSE!

Joseph Shaluwa ni Mshauri wa Mambo ya Mapenzi anayeandikia magazeti ya Global Publishers. Ameandika vitabu vya True Love na Let’s Talk About Love. Unaweza kumtembelea kwenye mtandao wake; www.shaluwanew.blogspot.comau jiunge naye kwenye facebook.

No comments: