Mwalimu wa Shule ya Msingi Maleza iliyopo wilayani hapa mkoani Mbeya, Martin Ilonga, amewekwa ndani kwa zaidi ya masaa sita katika kituo kidogo cha polisi Mkwajuni kwa amri ya Naibu Waziri wa Elimu na Mafunzo ya Ufundi, Philipo Mulugo, baada ya kukutwa akiwa amelewa pombe chakari muda wa saa za kazi.
Mwalimu huyo amekumbana na mkasa huo juzi majira ya saa 4 asubuhi katika mji mdogo wa Mkwajuni wilayani hapa ambapo alikamatwa karibu na baa moja ya mjini Mwakajuni huku akiwa amelewa pombe chakali na kupepesuka wakati akiongea na Naibu Waziri wa Elimu na Mafunzo ya Ufundi.
Mulugo ambaye pia ni Mbunge wa jimbo la Songwe wilayani Chunya yupo katika ziara ya kikazi kukagua miradi jimboni mwake ambapo wakati akielekea kukagua Shule ya Sekondari ya Maweni akiwa na watendaji kadhaa wa serikali akiwemo Diwani wa kata ya Mkwajuni, Ngailo ghafla alimuona mwalimu na kumwambia dereva wake asimamishe gari.
Baada ya gari hilo kusimama alimwita mwalimu huyo ambaye alifika na kuanza kumuuliza kuwa ni kwanini hajaenda kazini wakati siku hiyo (ijumaa) ni siku ya kazi naye kajibu kuwa anaumwa ndiyo sababu hajaenda kazini.
Hata hivyo, Naibu Waziri wa Elimu na Mafunzo ya Ufundi alimshtukia mwalimu huyo baada ya kubaini kuwa alikuwa akinuka pombe na hivyo wakati akiendelea kumhoji walipita askari wawili ambao aliwaagiza wamkamate mwalimu huyo na kumpeleka kituo cha polisi cha Mkwajuni.
Baada ya Mwalimu huyo kukamatwa, Naibu Waziri wa Elimu na Mafunzo ya Ufundi aliwaagiza askari hao waendelee kumuweka rumande hadi atakapo maliza ziara siku hiyo ambapo atafika kituo hicho cha polisi na kuangalia hatua gani zaidi zinazofaa kumchukulia.
Akizungumza na wananchi wa vitongoji vya Chudeko, Majengo na Kaloleni vilivyopo kijiji cha Mwakajuni, alisema kuanzia sasa atakuwa makini kufuatilia mienendo ya walimu na wale watoro wanaokimbilia kwenda kunywa pombe nyakati za saa za kazi watachukuliwa hatua kwa mujibu wa sheria ili kutoa fundisho kwa wengine .
Mulugo ambaye pia ni Mbunge wa Jimbo la Songwe, alisema hawezi kukubali kuona walimu wanakuwa watovu wa nidhamu kwa kuendekeza utoro na kuthamini pombe kuliko kazi waliyoajiriwa na inapofika mwisho wa mwezi wanachukua mishahara ya bure ambayo hawajaitolea jasho.
Aidha katika kitongoji cha Majengo alitoa zaidi ya Sh.700,000 kwa ajili ya kusaidia wanawake kuanzisha mradi wa maendeleo na nyingine kwa mabalozi Sh.150,000.
Kukamatwa kwa mwalimu huyo kumekuja siku chache tu baada ya Naibu Waziri huyo kutembelea Shule ya Msingi ya Maleza anayofundisha mwalimu huyo ambapo alielezwa na Mwalimu Mkuu wa Shule hiyo kwamba walimu katika shule hiyo wamekuwa watoro ambapo hawahudhurii kabisa vipindi darasani.
Alisema mfano yupo mwalimu mmoja ambaye anaishi mji wa Makongorosi ambako ni zaidi ya kilometa 50 hadi shuleni hapo na mwalimu mwingine Martin Ilonga aliyekamatwa anaishi Makongorosi ambako ni zaidi ya kilometa 20 kufika shuleni hapo.
Hali hiyo imetokana baada ya Naibu Waziri kugundua kuwa katika mtihani wa taifa wa mwaka jana shule ya msingi Maleza haikufaulisha hata mwanafunzi mmoja kwenda sekondari kutokana na utoro wa walimu katika shule hiyo.
CHANZO: NIPASHE JUMAPILI
No comments:
Post a Comment