Advertisements

Thursday, August 11, 2011

MAMBO YA KUZINGATIA KWA WAPENZI MWEZI MTUKUFU

Namshukuru Mwenyezi Mungu kwa kunijaalia uzima na kuniwezesha kuiona siku hii ya leo nikiwa salama salimin. Lakini namshukuru pia kwa kuwa amenipa uwezo wa kuandika mada za kimapenzi ambazo zinawagusa walio wengi.

Wiki iliyopita nilizungumzia faida za mtu kufanya maamuzi ya kumuacha mtu aliyetokea kumpenda lakini akawa hampi raha aliyoitarajia zaidi ya kulizwa kila siku.


Kwa kifupi, kumuacha mtu ni jambo la kawaida na wala usimvumilie mtu ambaye moyo wako unamkataa. Faida za kumuacha ndiyo kama zile nilizozitaja wiki iliyopita, kazi kwako.

Wiki hii nazungumzia suala la mapenzi hasa katika kipindi hiki ambacho Waislam wako katika Mwezi Mtukufu wa Ramadhani. Nimekuwa nikipokea maswali mengi kutoka kwa baadhi ya wasomaji wangu wakiuliza mambo kadhaa kuhusu uhusiano wao. Wapo ambao ni wapenzi na kipindi hiki inaonekana mahaba yamepungua kutokana na mmoja au wote kuwa katika mfungo.

Wapo wanaolalamikia wapenzi wao kutotaka hata kuonana nao kwa maelezo kwamba, wakikutana eti swaumu zitaharibika. Si hivyo tu, wapo wanaosema siku hizi mawasiliano yamekuwa hafifu, hakuna sms tamu, hakuna kupigiana simu kuzungumza mambo matamu.

Katika hili kwanza niseme tu kwamba, kupendana hakuna mipaka. Kila  dakika, kila saa, kila siku na kila sehemu tunatakiwa kuoneshana mapenzi sisi tulio katika uhusiano wa kawaida lakini pia wale walio katika ndoa. Kikubwa cha kuzingatia ni kutii sheria za kidini zilizopo.

Hata hivyo, wiki hii nataka kuzungumzia mambo kadhaa ambayo wapenzi wanatakiwa kuyazingatia hasa kwa kipindi cha mwezi huu mtukufu. 
Nimediriki kuzungumzia mada hii kwa kujua kwamba, mapenzi hayachagua dini, wapo waliopendana wakiwa katika dini tofauti, namaanisha Muislam na Mkristo.

Katika mazingira haya, ni lazima kutakuwa na matatizo kama mambo kadha wa kadha hayatazingatiwa na hili litakuja kama kila mmoja ataheshimu imani ya mwenzake na kuwa tayari kuvumilia kwa kila jambo.
Kukutana, kuongea ruksa! Jamani nani kasema ukiwa umefunga usikutane na mpenzi wako? Kuna tatizo gani kama mtakutana na kubadilisha mawazo kuhusiana na maisha yenu?

Kinachokatazwa hapa ni kutegana kimahaba kiasi cha kumfanya mpenzi wako afikie hatua ya kuiharibu swaumu yake.
Cha kuzingatia katika hili ni kuhakikisha humpi mpenzi wako vishawishi, zungumza lugha nzuri na pia mavazi yako yawe ya kujisitiri hasa kwa wanawake.

Fahamu kama mpenzi wako kafunga au mmefunga wote, ni kipindi cha kutubu dhambi zenu lakini pia kama hamjaoana basi ni wakati wa kumuomba Mungu awajaalie muweze kuoana haraka.

Hata hivyo, katika suala la kukutana, isiwe mara kwa mara. Nasema hivyo kwa kuwa najua sisi ni binadamu, unaweza kukutana na mpenzi wako fikra zako zikakupeleka kusikotakiwa na ukatamani kuonja na utakuwa umefanya kosa kubwa.

Sms na kupigiana simu kuwe na mipaka. Meseji zile za chumbani hazina nafasi kipindi hiki na ukimtumia mpenzi wako sms za kingono, ni matatizo kwako na kwa mwenzako, sasa kwa nini umuingize matatizoni mtu unayempenda?

Haya yote si kwa mchana tu, ni kwa saa 24 maana kuna ambao mchana wanafunga, usiku mahaba kama kawa wakati hawajaoana. Waliooana ndiyo walioruhusiwa kufanya mapenzi na tena ni baada ya kufuturu, wao wana haki hiyo.

Tukumbuke tu kwamba, zinaa imekatazwa, si kipindi hiki tu bali katika siku zote za maisha. Kwa maana hiyo basi, tujizuie kumkera Mungu lakini pia muombe dua ikiwezekana mwezi mtukufu ukiisha, muoane kabisa ili muweze kuyafurahia maisha yenu ya kimapenzi.

Ni hayo tu kwa leo, tukutane tena wiki ijayo kwa mada nyingine.

www.globalpublishers.info

2 comments:

Anonymous said...

Ustaadh Dullah, kwanza namshukuru Mola kwa kuniwezesha leo hii kufunga mwezi huu mtukufu. Makala yako imenifurahisha sana kuuona kijana kama wewe umemuweka Mola wako mbele. Si kazi yetu kumhukumu mtu nani kafunga na hakufunga. Sote tunafahamu funga za Marekani zimetawaliwa na mushkeli wa hapa na pale. Tupo kwanye nchi yenye maadili tofauti na tuliyokulia inshallah Mola atatuondolea kila kipingamizi ili funga zetu ziwe za heri. Ustaadh Dullah labda kwa kumalizia umesahau kidogo Mtume(S.A.W) amesema "HAKIKA KILA MWENYE KUOA AMEKAMILISHA NUSU YA DINI YAKE." Mimi nakuombea DUA kubwa na ndogo ndogo Mola akufungulie, mwenye HUS'DA na wewe na Bi Zainabu basi HUS'DA hizo zimrudie mwenyewe, Mola awape NURU YA MAISHA. Kwa baraka za Ramadhani hii mungu awafungulie kila la heri mnalolikusudia.
AMEN.

Anonymous said...

Jazakallah kheiran!