Advertisements

Thursday, August 11, 2011

Kiiza kiza kinene Yanga

Image
MSHAMBULIAJI Yanga, Mganda Hamisi Kiiza amezua kiza kinene ndani ya klabu hiyo baada ya kuondoka nchini bila kuutaarifu uongozi wake.

Mshambuliaji huyo mpya wa Yanga maarufu kama ‘Diego’, aliondoka nchini Agosti 10 kwenda kwao Uganda mara baada ya timu hiyo kuwasili Dar es Salaam ikitokea Khartoum, Sudan, ambako ilienda kujipima nguvu na Al Hilal.

Ofisa Habari wa Yanga, Louis Sendeu amekiri kuwa nyota wao huyo aliondoka kwenda kwao kwa kile kinachoelezwa kuwa anakabiliwa na matatizo ya kifamilia.

Hatahivyo Sendeu alipoulizwa endapo mchezaji huyo aliwasiliana na viongozi wake kwa ajili ya kuomba ruksa kabla ya kuamua kuondoka, alikataa kuzungumzia suala hilo na kusema uongozi wa Yanga ulitarajiwa kukutana jana jioni kujadili suala lake. 



“Ni kweli Kiiza hayupo kambini na wenzake, kwani aliondoka jana(juzi) kwenda kwao Uganda na uongozi umepanga kukutana kujadiliana kuhusiana na jambo hilo na itazungumzia suala lake baada ya kukutana,”alisema Sendeu.

Hii ni mara ya pili kwa mshambuliaji huyo wa Yanga kuzua kizaazaa katika klabu hiyo, mara ya kwanza ilikuwa wakati aliposhindwa kuripoti kambini kuanza mazoezi ya pamoja ya kujiandaa na msimu wa ligi na kuwasili Dar es Salaam siku chache kabla timu haijaenda Sudan.

Wakati huohuo, Kocha Mkuu wa Yanga, Mganda Sam Timbe anatarajiwa kuzungumza na waandishi wa habari kuhusiana na ziara ya timu hiyo nchini Sudan, ambako ilicheza mechi mbili dhidi ya Al Hilal na kufungwa zote, ambapo kila mchezo ilifungwa mabao 3-1.


Habari Leo

No comments: