.jpg)
Kamanda wa Polisi wa Mkoa wa Mbeya, Advocate Nyombi (Kushoto), akiwa pamoja na askari wapelelezi mkoani humo, wakionyesha bunduki inayodaiwa kutumika kumuua aliyekuwa Mwenyekiti wa halmashauri ya Rungwe
Watu 11 wametiwa mbaroni kwa tuhuma za mauaji ya aliyekuwa Mwenyekiti wa Halmashauri ya Rungwe, mkoani Mbeya, marehemu John Mwankenja.
Kukamatwa kwa watuhumiwa hao ni utekelezaji wa agizo la Rais Jakaya Kikwete, aliloligiza Jeshi la Polisi mkoani hapa kuhakikisha linawasaka na kuwakamata watuhumiwa wote wa mauaji hayo na kufikishwa mbele ya vyombo vya haki.
Marehemu Mwankenja aliuawa kwa kupigwa risasi Mei 19, mwaka huu na watu wasiofahamika, wakati akiegesha gari nyumbani kwake, akitokea jijini Mbeya.
Alikwenda Mbeya kumjulia hali mkewe aliyekuwa amelazwa hospitali akisubiri kufanyiwa operesheni.
Kamanda wa Polisi wa Mkoa wa Mbeya, Advocate Nyombi, aliwaambia waandishi wa habari jijini hapa jana kuwa, polisi walifanikiwa kuwakamata watuhumiwa hao pamoja na bunduki iliyotumika katika tukio hilo.
Alisema watuhumiwa hao wamekamatwa kwa nyakati tofauti ndani ya siku kumi tangu mauaji yalipotokea.
Kamanda Nyombi, alisema watuhumiwa walikamatwa wakiwa na bunduki aina ya SMG yenye namba 786474, pamoja na risasi 37, funguo 27 za milango mbalimbani, kofia moja aina ya mzura na jaketi moja likiwa na kofia maalum yenye uwezo wa kuficha uso.
Alisema wakati watuhumiwa hao wakishikiliwa na polisi, polisi wanaendelea ma uchunguzi juu ya mauaji hayo na kwamba watuhumiwa wote watafikishwa mahakamani uchunguzi utakapokamilika.
CHANZO: NIPASHE
No comments:
Post a Comment