ANGALIA LIVE NEWS

Wednesday, June 1, 2011

Baadhi ya wanaotumia ARVs hawawezi kuambukiza VVU

UTAFITI kuhusu tiba ya kukabiliana na makali ya virusi vya Ukimwi (VVU), umebaini kuwepo kwa watumiaji wa dawa hizo, ambao hawawezi kuambukiza virusi hivyo kwa watu wengine. 

Kwa mujibu wa Chama cha Kimataifa cha Ukimwi (IAS), hatua hiyo inaonesha mafanikio katika safari ya kutafuta tiba ya ugonjwa huo ambao umeendelea kuua watu wengi duniani. 

Akikaririwa na Shirika la Utangazaji la Uingereza (BBC), Mkuu wa IAS, Bertrand Audoin, alisema kazi iliyopo ni kutafuta tiba ya kufanya virusi viwe butu mwili, visimdhuru muathirika na visiambukize watu wasio na virusi.
 

Audoin anakiri kwamba, inaweza kuchukua hata miaka 25, lakini anasema tiba ndiyo njia pekee ya kukabiliana na maambukizi ya VVU kwa muda mrefu wakati huu wa matatizo ya kifedha duniani. 

“Ni wakati muafaka sasa – kimtazamo wa kisayansi na kifedha - kuwekeza muda na fedha zaidi katika kufanya utafiti wa tiba. 

“Tayari kuna ugunduzi fulani wa kisayansi katika eneo hilo. Tunajua kwamba baadhi ya watu wanaoendelea na matibabu ya VVU wanaweza kuwa na virusi, lakini wasiweze kuambukiza wengine sasa. 

“Hivyo, tunadhani kazi zaidi itasaidia kupata tiba, ambayo sasa itaruhusu virusi kuwa butu mwilini, bila mtu kuhisi anaumwa au kuhitaji matibabu. Hilo ndilo lengo hasa.” 

Jumapili yatashuhudiwa maadhimisho ya miaka 30 ya taarifa ya kwanza ya kitabibu ya ugonjwa huu mpya. 

Baadhi ya wataalamu wameonya kwamba kuzungumzia tiba kunaweza kusababisha matumaini potofu na badala yake ni vema kutafuta chanjo yake. 

Audoin alipata kuongoza Shirika la Kupambana na Ukimwi la Ufaransa lililojulikana kama Sidaction, kabla ya kuongoza IAS – shirika lenye wataalamu na wanaharakati 18,000. 

Alisema: “Kwa sasa, kwa kila mtu anayeanza matibabu katika nchi zilizoathirika sana katika Afrika, watu wawili wanaambukizwa VVU wakati huo. 

“Hivyo matibabu kwa vidonge vya kurefusha maisha – ARVs - si suluhisho pekee la muda mrefu. 

“Itaweza kuchukua miaka 25 kabla ya kupata tiba – na ugumu utakuwa katika kushawishi nchi wahisani na mashirika mengine ya misaada kuwekeza fedha katika utafiti huo. 

“Lakini tusipowekeza katika sayansi, maambukizi yataendelea kwa kasi kuliko kazi tunayoifanya – na hali ya kifedha itasababisha ugumu zaidi katika kutibu watu.” 

IAS imekutanisha kikosikazi cha watafiti wa kimataifa ili kuja na mkakati ambao unaweza kupata tiba. Inatarajia kuwasilisha rasimu ya taarifa yake mwishoni mwa mwaka huu. 

Kikosi hicho kinaongozwa kwa pamoja na Profesa Francoise Barre-Sinoussi, ambaye ni mshindi wa Nishani ya Nobel ya mwaka 2008 kwa ugunduzi wa VVU. 

Mtaalamu wa magonjwa yatokanayo na virusi wa Chuo Kikuu cha London, Profesa Robin Weiss, alisema: “Sitaki kuamini kwamba mnaweza kuponya maambukizi ya VVU, lakini mnaweza kupunguza kiwango kilichoko mwilini. 

“Mimi ningependa kuona chanjo ili tuweze kuzuia watu kuambukizwa kwanza. Lakini bado tuna safari ndefu ya kupata tiba ya VVU.”


CHANZO:HABARI LEO

No comments: