ANGALIA LIVE NEWS

Wednesday, June 1, 2011

Chenge asaidia Dowans ilipwe

Mwanasheria Mkuu wa zamani wa serikali, Andrew Chenge, ameamua kuitetea kampuni ya Dowans ilipwe na serikali ya Tanzania Sh. bilioni 94 kama ilivyoamriwa na Mahakama ya Kimataifa ya Usuluhishi wa Migogoro (ICC).
Chenge ametoa utetezi kwa niaba ya mlalamikaji kwenye shauri la usuluhishi kati ya walalamikaji wawili ambao ni Dowans Holdings SA akiwa ni mlalamikaji wa kwanza na Dowans Tanzania Limited mlalamikaji wa pili dhidi ya Kampuni ya Umeme nchini (Tanesco) ambaye ndiye mdaiwa.

Mbali ya kuwa mwanasheria mkuu wa serikali, Chenge pia amekuwa waziri katika serikali ya awamu ya nne, akianzia Ushirikiano wa Kimataifa, kisha Ujenzi (wakati huo Miundombinu) ambako alijiuzulu kwa sababu ya sakata la rada.
Katika sakata la rada, Chenge alikuwa mtuhumiwa muhimu, na sakata hili liliisha kwa Kampuni ya BAE ya Uingereza kukubali kulipa fidia kwa uzembe wa kuweka kumbukumbu, na kukwepa kigingi cha rushwa.
Katika maelezo ya Chenge ambayo yameelezwa kuwa ni ushauri wa kitaalam, uliotolewa kwa maandishi Mei 6, mwaka huu katika Mahakama Kuu ya Uingereza, kitengo cha Biashara unalenga kuhalalisha malipo ya tuzo kwa kampuni ya Dowans iliyoamriwa kulipwa na ICC.
Katika maelezo yake hayo yanayorejewa kuwa ni ‘Ripoti ya kitaalamu ya Andrew Chenge’, anaanza utangulizi wake kwa kueleza kuwa yeye ni Andrew Chenge anayeishi katika kiwanja namba 240, Nyumba namba 546, Barabara ya Ghuba, eneo la Oysterbay jijini Dar es Salaam Tanzania Anaendelea kueleza katika maelezo yake kuwa, anatoa maelezo hayo kufuatia ombi la Stephenson Harvard, wakili wa walalamikaji na katika kuitikia barua yao ya Aprili 15, mwaka huu ambayo bila ya viambatanisho vyake imenakiliwa kama ushahidi namba “AJC 1”
Aliendelea kueleza kuwa alipata Shahada yake ya Sheria (LLB) kutoka Chuo Kikuu cha Dar es Salaam mwaka 1972.
Alisema baada ya hapo alijiunga na Ofisi ya Mwanasheria Mkuu wa serikali na baada ya hapo kwa muda wa miaka minne alikwenda Harvard Marekani, Benki ya Dunia na katika kazi za kibinafsi, kisha alirejea kwenye idara ya sheria za kiraia na za kimataifa iliyokuwa katika Ofisi ya Mwanasheria Mkuu wa serikali mwaka 1978.
Chenge alisema aliteuliwa kuwa Mwanasheria Mwandamizi wa serikali mwaka 1988 na Naibu Mwanasheria Mkuu na Katibu Mkuu wa Wizara ya Sheria mwaka 1991.
Alisema aliteuliwa kuwa Mwanasheria Mkuu wa serikali ya Tanzania mwaka 1993 ambapo alishikilia nafasi hiyo hadi Desemba mwaka 2005. Alisema alichaguliwa kuwa Mbunge wa Bariadi Magharibi mwaka 2005 na hadi leo anaendelea kuishikilia nafasi hiyo.
Alisema nakala ya wasifu wake (CV) imetolewa kama kielelezo “AJC2”
“Sasa nitashughulika na hoja na maswali yaliyojitokeza kwenye barua ya Stephenson Harwood. Ninaitoa katika kielelezo“AJC3” taarifa ambayo nimeirejea katika ripoti yangu hii ambayo marejeo yake katika namba za kurasa kwenye AJC 3 zimekolezwa,” anasema Chenge.
Katika maelezo yake ya utetezi ya kuzifafanua hoja na maswali yaliyojitokeza katika barua waliomwandikia walalamikaji, Chenge ameangalia ‘utawala wa kisheria wa kuipinga tuzo iliyotolewa katika Mahakama za Tanzania’ akiitumia sheria ya usuluhishi ya mwaka 2002.
Alisema pamoja na vifungu vyote vilivyoondolewa, vilivyorejewa na vilivyorekebishwa kuhusiana na suala linalohusu tuzo, kanuni ambazo bado zipo lazima zisomwe pamoja na sheria ya usuluhishi ya mwaka 2002 ambapo nakala ya sheria hiyo na kanuni za usuluhishi za Tanzania za mwaka 1957 anaeleza kuziambatanisha.
Chenge alisema sababu pekee zinazoweza kuifanya tuzo hiyo ikapingwa zimeelezwa katika sheria hiyo ya mwaka 2002 na hasa katika kifungu cha 16 ambacho kinaruhusu tuzo kupingwa ikiwa tu limetolewa kutokana na mwenendo mbaya au kama imepatikana isivyo kihalali.
Alisema chini ya kifungu cha 15, tuzo inaweza kurudishwa kwa ajili ya masahihisho katika mahakama iliyotoa maamuzi hayo.
Akizungumzia namna ya kuipinga hukumu ya tuzo chini ya kutolewa kwa mwenendo mbaya (misconduct), Chenge alisema neno hilo halikutolewa maana yake kwenye sheria ya usuluhishi ya mwaka 2002 na kwamba hakuna mamlaka yoyote Tanzania ambayo imetafsiri neno hilo na kwamba kwa maoni yake mahakama za Tanzania zitaliangalia suala hilo kwa ufinyu na kutilia mkazo kama mahakama au mjumbe wake hakutenda haki au isivyo sawa.
Baada ya hapo, Chenge alizungumzia pingamizi dhidi ya tuzo lililowasilishwa na Tanesco na wadau wengine na hasa maswali manne yaliyotolewa katika aya ya 10 iliyotolewa kama kilelezo “AJC 1”
Alisema kwa kuangalia alichopewa yeye, pande hizo mbili katika mgogoro huo zilikubaliana kutumia sheria za Texas katika mgogoro wao na kwamba wakati wanakubaliana Tanesco hawakuhoji uhalali wa kuzitumia sheria hizo, hivyo anaona hoja ya Tanesco ya kuhoji maamuzi yaliyofikiwa kwa kutumia sheria za Texas haina mashiko.
Akizungumzia aya ya sita ya pingamizi la Tanesco, Chenge alisema kwamba ‘ inaonekana aya hiyo inakubaliana na maoni yake kwamba kinachounda mwenendo mbaya ni mapungufu ya taratibu za haki. “Kwa hiyo siamini kama sababu hizo 11 walizotoa zinaunda mwenendo mbaya.”
Akizungumzia pingamizi la Tanesco la aya ya tisa lisemalo kwamba tuzo iliyotolewa ina makosa kisheria katika macho ya kumbukumbu, Chenge alisema hilo ni suala la ushahidi na si la sheria kwa msingi kwamba mahakama ina mamlaka ya kuingilia.
Alisema kesi ya D.P Shapriya imeshalifafanua vizuri sana suala hilo.
Alimalizia kwa kusema kwamba maoni yake kwa aya ya 10 ya pingamizi la Tanesco kwamba tozo iko kinyume cha sera ya umma haina nguvu ya kushinda kwa sababu zilizoelezwa katika aya ya 15.
NIPASHE ilimwuliza Chenge anajisikiaje anapotaka kuibana nchi yake ilipe kampuni hiyo ya kigeni na alijibu kuwa hawezi kuzungumzia mambo yasiyomhusu na alimtaka mwandishi kuendelea na shughuli zake.
“Nimesema siwezi kuzungumza masuala ambayo hayanihusu na naomba uendelee na shughuli zako inamaana hunielewi?” alisema Chenge kwa kifupi na kuhoji kisha akakata simu.
CHANZO: NIPASHE


No comments: