
Ilipoishia wiki iliyopita:
Ikawa mke huyo akienda kuwaona watoto wake anakaribishwa na msichana wake wa kazi, anamuandalia chumba cha kulala ambacho awali alikuwa akilala yeye. Mama hakawa hana chake.
Haya yote ni madhara ya kuwaachia wasichana wa kazi wafanye kila kitu kwa waume ndani ya nyumba. Ni hatari kuliko inavyofikiriwa.
SASA ENDELEA…
Ikawa mke huyo akienda kuwaona watoto wake anakaribishwa na msichana wake wa kazi, anamuandalia chumba cha kulala ambacho awali alikuwa akilala yeye. Mama hakawa hana chake.
Haya yote ni madhara ya kuwaachia wasichana wa kazi wafanye kila kitu kwa waume ndani ya nyumba. Ni hatari kuliko inavyofikiriwa.
SASA ENDELEA…
DALILI YA TANO
Hii ndiyo dalili yetu ya mwisho ya kufungia jamvi hili la Mashamsham kabla ya wiki ijayo kuangalia mada isemayo KWENYE USALITI; MUDA, GIZA SI KIGEZO.
Katika dalili hii ya tano, mara nyingi hausigeli ambaye ana uhusiano wa kimapenzi na baba ndani ya nyumba huanza kuwa jeuri, kiburi na asiyetaka kusikia maelekezo kama zamani.
Utakuta mke unamuita msichana wako huyo wa kazi ili umpe maelekezo ya kufanya, lakini atachukua dakika hata tano kufika kukusikiliza.
Na hata utakapokuwa ukiongea naye, uso wake hauweki kama zamani katika hali ya kujali, ataonesha dalili za dharau kama moyoni anayesema; ‘utanifanya nini? Mumeo nalala naye.’
Msichana wa kazi akiwa hivi tambua kuna kitu kama hicho, huna budi wewe mama kufuatilia kwa makini ili kuujua ukweli, ingawa pia wapo wasichana ambao hubadilika tabia kutokana na kunasa katika mapenzi kati yake na muuza duka jirani au muuza genge.
Kinachotokea sasa, wanawake wengi huichukulia tabia hii kuwa, hausigeli ‘amelijua jiji’ ndiyo maana amebadilika.
Katika dalili hii ya tano, wakati mwingine hausigeli huwa jeuri kutokana na maneno anayoongea na baba. Wako wa-baba ambao wanapokuwa na uhusiano wa kimapenzi na wasichana wa kazi huongea mambo mengi ya siri kuhusu wake zao. Mfano…
Baba: We Jane…
Hausigeli: Abee …
Baba: Njoo…kaa hapo…
Msichana anakaa, kisha baba anaendelea…
“Mama yako jana alirudi saa ngapi kutoka kazini?”
Hausigeli: Mh! Kama saa moja na nusu usiku.
Baba: Huyu mwanamke huyu, anachelewa wapi lakini?
Hausigeli: Sijui, labda kuna mahali anapitia.
Baba: Dawa yake ipo jikoni, kuna siku ataondoka hapa nyumbani, wanawake wapo wengi bwana…ala!
Msichana wa kazi akitoka hapo anachoamini yeye ni kwamba, mke huyo anaishi kwa kushikilia nyuzi nyembamba sana ambapo siku yoyote itakatika na ndoa kuvunjika.
Sasa kwa sababu naye ni mwanamke na ameshaanza kulala na mume huyo, anaamini anaweza kuolewa yeye badala yako.
Hapo ndipo kiburi huanza, ukiongea naye anakuangalia kwa dharau kwa sababu nyuma ya akili yake kuna mazungumzo kati yake na baba kuhusu wewe ambayo anaamini hujui na ni siri yao wawili.
Wapo wanaume wanaotembea na wasichana wao wa kazi na kuwaponda wake zao mbele yao jambo ambalo pia huongeza dharau.
Lakini pia kuna suala la matumizi. Wewe mama kama utamfuatilia kwa makini msichana wako wa kazi na kugundua ana vitu vyenye gharama inayopita mshahara wake ni sehemu ya dalili hii ya tano.
Utakuta mshahara wake ni shilingi elfu ishirini (20,000) kwa mwezi, lakini kwa mwezi huo uliomlipa ananunua simu ya elfu thelathini na tano, anaweka vocha ya buku, ananunua sendozi za elfu kumi na tano na anaweka dawa nywele.
Kama utapiga hesabu ya haraka haraka utagundua ametumia kama shilingi elfu hamsini na tano! Hapo ndipo penye maswali kibao.
Kwa wa-mama wengine hawana haja ya kuhoji. Ni sawa lakini nasema kuwa, unaliwa mwanamke bila kujijua. Dunia ya sasa kama wewe si mwelewa utajikuta pale unapogundua tukio mambo yameshamwagika.
Ndiyo maana hata serikali humtafakari mtumishi wake kulingana na kipato, kama kwa mwezi analipwa shilingi laki moja na nusu (150,000) halafu anamiliki gari na hana mradi wowote, wasiwasi husababisha upelelezi.
Utafiti wangu wa kina umejiridhisha kuwa, wasichana wa kazi kwa miaka ya karibuni wamekuwa wakiingia kwenye nyumba za watu kwa lengo la kutafuta njia ya kutongozwa na wa-baba wenye nyumba ili wajiongezee kipato na ikibidi kupindua ndoa.
Mikasa hii ipo na watu wanakumbana nayo kila kukicha. Kikubwa ni ‘taiming’ ambazo wa-mama wengi wanakosea na kujikuta wenyewe wanagawa nafasi ya kusalitiwa.
Mwanamke huwezi ukamwachia msichana wako wa kazi afue ‘sing’lendi’ za mumeo. Kwa wasiojua ni zile nguo zinazovaliwa kabla ya shati.
Sasa kama ‘kufuli’ huvaliwa kabla ya suruali, kwanini sing’lendi nayo isiheshimiwe kwa vile inavaliwa kabla ya shati? Kumpa msichana afue nguo kama hii ni sawa na kumruhusu pia afue ‘makufuli’ ya mumeo. Kama upo hivi badilika.
Nilipata bahati ya kuongea na wanaume ambapo baadhi yao walidai kuwa, huwa hawana mawazo ya kufanya mapenzi na wasichana wa kazi lakini wanawake wenyewe huchangia kwa sababu huwa wanaunganisha urafiki kati ya mfanyakazi na baba mwenye nyumba.
Nimefika mwisho wa makala yangu haya, lakini kama nilivyosema, wiki ijayo nitakuwa na mada ya KATIKA USALITI; MUDA, GIZA SI KIGEZO.
1 comment:
Duh!
Dalili hizi pia huashiria kuwa msichana wa gazi ana kibuzi, yaweza kuwa sio mume, bali jirani au mtu mwingine hapo hapo nyumbani!
Post a Comment