ANGALIA LIVE NEWS

Thursday, June 2, 2011

Zitto awashika wabunge pabaya

Mwenyekiti wa Kamati ya Bunge ya Hesabu za Mashirika ya Umma, Zitto Kabwe, akisisitiza jambo wakati wa kikao cha kamati hiyo katika ofisi ndogo za Bunge jijini Dar es Salaam jana. Kushoto ni Makamu
   Ataka posho zote za vikao ziondolewe
  Ataka panga pia lielekezwe serikalini
Mbunge wa Kigoma Kaskazini (Chadema), Zitto Kabwe, kwa mara nyingine ameibua hoja nzito iliyowahi kutaka kuligawa Bunge vipande vipande ya kutaka wabunge wasiwe wanalipwa posho za vikao akisema kuwa kazi wanayoifanya ni sehemu ya majukumu yao ya kila siku.

Akizungumza jana jijini Dar es Salaam katika Ofisi Ndogo ya Bunge jijini Dar es Salaam, Zitto alisema haoni sababu mbunge kuendelea kulipwa posho nono kwa ajili ya kuhudhuria vikao kwa kuwa hiyo ni sehemu ya kazi yao ya kila siku.
Alisema anataka sheria ya Bunge inayotoa mwanya kwa wabunge kulipwa posho hizo ibadilishwe haraka ili kiasi hicho cha fedha kitumike kwa ajili ya kuwasaidia Watanzania wengine wenye matatizo.
Zitto alisema ingawa suala hilo ni gumu, lakini ataliwasilisha katika mkutano wa Bunge la bajeti wakati atakapowasilisha bajeti yake kama Waziri Kivuli wa Fedha na Uchumi.
Alisema ana imani wabunge wenzake watakubali pendekezo hilo na kumuunga mkono kubadilisha sheria hiyo ili posho hizo zisiwe zinatolewa.
Katika Bunge lililopita aliyekuwa Mbunge wa Karatu, Dk. Willibroad Slaa (Chadema), aliwahi kutoa wazo kama hilo pamoja na kupendekeza mshahara wa wabunge upunguzwe kwa kuwa ni mkubwa, lakini wabunge wenzake walipinga hoja hiyo kwa nguvu zote.
Dk. Slaa alishindwa kupitisha hoja yake katika Bunge lililopita baada ya wenzake kukataa kumuunga mkono huku baadhi yao wakitoa kauli za kumkejeli na kumuona kama mtu aliyekuwa akitafuta umaarufu wa kisiasa.
Kiutaratibu wabunge wote hulipwa posho ya vikao ya Sh. 80,000 kwa siku, na posho ya kujikimu kwa kuwa ya nje makazi Sh. 70,000 hivyo kwa siku moja tu wabunge hulipwa wastani wa Sh. 150,000 siku za kazi, wakati mwishoni mwa wiki hulipwa Sh. 70,000, kwa maana hiyo kati ya wabunge wote waliopo ambao ni 350 kama posho hizo zitaondolewa serikali itaokoa kiasi cha Sh. milioni 52.5 kwa siku.
Mkutano wa Bunge la Bajeti unatarajiwa kuanza Juni 7, mwaka huu hadi Agosti 15, mwaka huu, kwa maana hiyo kutakuwa na siku za kazi 48 ambazo zitaigharimu serikali Sh. bilioni 2.52 kama posho ya vikao kwa wabunge.
Kiasi hicho kikiongezwa Sh. milioni 490 za posho ya kujikimu ya mwishoni mwa wiki ambazo ni sawa na siku 20, serikali itakuwa inatumia jumla Sh. bilioni 3.01 ambazo ni posho za wabunge bila mshahara.
Kiasi hicho kama hakitalipwa wabunge kinaweza kuelekezwa kutunisha bajeti ya elimu, barabara au afya, ambako kuna upungufu mkubwa wa fedha.
Mshahara wa mbunge kwa sasa ni Sh. milioni 2.5, kiasi hicho kikichanganywa na posho ya mafuta, kuendesha ofisi mapato yake ya ubunge yanafika kiasi cha Sh. milioni 7.19.
Mbali na wabunge, watumishi wengi wa serikali nao wanaishi kwa posho ya vikao na mikutano ya ndani zinazoigharimu serikali mabilioni ya shilingi kila mwaka.
Wakati huo huo, Kamati ya Kudumu ya Bunge ya Hesabu za Mashirika ya Umma (POAC), imeshangazwa na hatua ya kitengo cha kupakia na kupakua kontena bandarini (Ticts), kupuuza agizo la Rais Jakaya Kikwete na kukaidi kulipa Dola za Marekani milioni 261 ambazo ni gharama za kuhamisha makontena bandarini kwenda bandari kavu.
Kamati hiyo jana ilizidi kuyabana mashirika ya umma ambapo ilibaini madudu ndani ya Mamlaka ya Bandari nchini (TPA) ambako Sh. bilioni 1.7 zimetumika kwa ajili ya manunuzi bila kuzingatia sheria na taratibu za serikali.
Rais Kikwete mwaka jana alipotembelea Bandari ya Dar es Salaam aliagiza makontena yaliyokuwa yamerundikana hapo yahamishwe na kupelekwa bandari ya nchi kavu na alisema gharama za kazi hiyo zilipwe na Ticts.
Hata hivyo, tangu wakati huo, Titcs wamekaidi agizo hilo na huwa hawafiki kwenye vikao mbalimbali vilivyoitishwa na Wizara ya Uchukuzi ili kujadili suala hilo kwa pamoja.
POAC iliambiwa hayo jana jijini Dar es Salaam ilipokutana na TPA ambako uongozi wa Mamlaka hiyo ulithibitisha kutolipwa na Ticts gharama hizo ilizotumia kuhamisha makontena hayo ikiwa ni sehemu ya utekelezaji wa agizo la Rais Kikwete.
Kaimu Mkurugenzi Mkuu wa TPA, Idd Mkwata, aliiambia kamati hiyo kuwa Ticts imegoma kulipa kwa madai kuwa hakuna mkataba wa maandishi unaowataka kufanya hivyo.
Kutokana na hatua hiyo ya Ticts, Mwenyekiti wa Kamati hiyo, Zitto Kabwe, aliagiza kampuni hiyo iitwe kwenye Kamati ya Maadili ya Bunge ili kutoa maelezo ni kwa nini imekaidi agizo la Rais Kikwete.
Mkwata alisema Ticts wamekuwa na kiburi cha kupindukia kila walipofuatwa na kuambiwa kuhusu malipo ya fedha hizo na kuongeza kuwa uongozi wa TPA uliiandikia barua Ikulu kulalamikia hatua hiyo, lakini bado hawajapata ufumbuzi wa suala hilo.
Zitto alionyesha kukerwa na kitendo cha Ticts kukaidi agizo la Rais Kikwete na kusema kuwa "wazungu hawa wa Ticts wanadharau sana na wanatudharau Watanzania wote mpaka Rais Kikwete,"
Kuhusu manunuzi yasiyozingatia sheria, kamati hiyo iliagiza TPA kurekebisha makosa hayo na kwamba itaitwa tena mara ya pili.
Zitto alisema kiasi hicho cha fedha ni kikubwa na kwamba lazima hatua zichukuliwe na kamati ili kuhakikisha mahesabu ya TPA yanakaa vizuri.
CHANZO: NIPASHE

No comments: