ANGALIA LIVE NEWS

Saturday, July 30, 2011

DPP: Jamhuri kukata rufani kesi ya Richmond



Mkurugenzi wa Mashtaka nchini (DPP), Eliezer Feleshi, amesema msimamo wa serikali kuhusu uamuzi wa Mahakama ya Hakimu Mkazi Kisutu jijini Dar es Salaam wa kumwachia huru Mkurugenzi wa Kampuni ya Richmond Tanzania Limited, Naeem Gire, ni kukata rufaa kuupinga.
Feleshi alisema hayo jana ikiwa ni siku moja, baada ya mmoja wa mawakili walioiwakilisha serikali katika kesi hiyo, Shadrack Kimaro, kueleza kuwa Jamhuri (serikali) haijaridhishwa na uamuzo huo.
Akizungumza na NIPASHE jana, Feleshi alisema msimamo wa serikali hautofautiani na ule uliotolewa na mawakili walioiwakilisha serikali katika kesi hiyo.
“Msimamo wa serikali ni ule uliotolewa na mawakili wa serikali mahakamani jana (juzi),” alisema Feleshi.

Feleshi alitoa kauli hiyo alipotakiwa na NIPASHE kueleza iwapo serikali itaukatia rufaa uamuzi huo wa Mahakama ya Hakimu Mkazi Kisutu au la.
Awali, NIPASHE iliwasiliana na Mwanasheria Mkuu wa Serikali (AG), Jaji Frederick Werema, kutaka kujua msimamo wa serikali kuhusiana na uamuzi huo wa mahakama.
Hata hivyo, Jaji Werema hakuwa tayari kuzungumzia suala hilo, badala yake alimtaka mwandishi kumtafuta DPP.
Uamuzi wa kumwachia huru mtuhumiwa huyo, ulitolewa juzi na Hakimu Mkazi wa Mahakama hiyo, Waliarwande Lema.
Katika uamuzi wake, Hakimu Lema alisema ushahidi na vielelezo vilivyotolewa na serikali katika kesi hiyo ni dhaifu vyenye upungufu unaoacha maswali mengi.
Katika kesi hiyo, Gire alikuwa akikabiliwa na makosa ya kughushi, kutoa taarifa za uongo kwa maofisa wa serikali kuhusu kampuni ya Richmond, yenye makao makuu yake Texas, nchini Marekani.
Alikuwa akitetewa na wakili wa kujitegemea; Alex Mgongolwa na Richard Rweyongeza, wakati serikali iliwakilishwa na mawakili wake, Frederick Manyanda na Kimaro.
Alifikishwa mahakamani hapo Januari 13, 2009 takriban mwaka mmoja baada ya aliyekuwa Waziri Mkuu, Edward Lowassa, Waziri wa Nishati na Madini, Nazir Karamagi na aliyekuwa Waziri wa Ushirikiano wa Afrika Mashariki, Dk. Ibrahim Msabaha, kujiuzulu nyadhifa zao kutokana na mkataba tata wa zabuni ya kufua umeme wa dharura wa megawati 100 uliotolewa kwa kampuni ya Richmond.
CHANZO: NIPASHE

No comments: