ANGALIA LIVE NEWS

Tuesday, July 19, 2011

Kwa kashfa hii lazima pia Ngeleja atimuliwe

Waziri Nishati na Madini,William Ngeleja
Muda mrefu kabla ya Wizara ya Nishati na Madini kuwasilisha bungeni makadirio ya matumizi yake kwa mwaka 2011/12  mwishoni mwa wiki iliyopita, gazeti hili lilipata habari kutoka kwenye vyanzo vyake mbalimbali vya habari ndani na nje ya Bunge zilizosema kwamba, wizara hiyo ilikuwa imetenga mabilioni ya fedha kuwahonga wabunge kwa lengo la kuwashawishi wakubali kupitisha bajeti ya wizara hiyo.

 
Vyanzo vyetu hivyo vya habari vilituhakikishia kwamba, hakika fedha hizo tayari zilikuwa zinagawiwa kwa wabunge na kwamba kampuni mashuhuri inayohusika na masuala ya mahusiano yenye makao yake makuu jijini Dar es Salaam, ambayo tunahifadhi jina lake kwa sasa,  ilikuwa imepewa zabuni ya kusambaza fedha hizo za hongo.
 
Habari zilisema fedha hizo zilielekezwa kwa wabunge ambao wangekubali kupokea fedha hizo na kuisaidia wizara hiyo kupitisha bajeti yake ambayo ilikuwa imekamiwa na idadi kubwa ya wabunge wa CCM na wabunge wote wa upinzani kwa kutokuwa na mikakati yoyote ya kumaliza tatizo kubwa la umeme ambalo limekuwa linalikabili taifa kwa muda mrefu sasa.
 
Lakini katika kufuatilia kashfa hiyo, gazeti hili lilidokezwa  kuwa, fedha hizo awali zilielekezwa kwa baadhi ya wajumbe wa Kamati ya Nishati na Madini inayoongozwa na Mbunge wa Bumbuli, Januari Makamba ambaye inasemekana alisimama kidete kuikataa bajeti hiyo ilipojadiliwa na kamati yake, huku baadhi ya wabunge wakiiunga mkono. Habari zilidai kuwa baadhi ya wajumbe wa kamati hiyo walipokea fedha hizo zinazosemekana zilikuwa “nyingi”.
 
Pengine wasomaji wetu na wananchi kwa jumla watashangaa kwanini gazeti hili, pamoja na kupata dokezo hizo nzito, halikuchapisha habari za kashfa hiyo hadi zilipoibuliwa jana bungeni na Mbunge wa Kilindi, Beatrice Shelukindo na kuthibitishwa na Waziri Mkuu, Mizengo Pinda?
 
Tunakiri kabisa kwamba baadhi ya wananchi wanaweza kuibua  dukuduku kuhusu suala hilo, ingawa tungependa waelewe kwamba kutochapisha habari hizo kulitokana na ukweli kwamba wizara husika ilikanusha tuhuma hizo na ndiyo maana gazeti hili lilizingatia weledi kwa kuendesha uchunguzi na kutafuta ushahidi ambao hatimaye ungewezesha kupatikana ukweli usiotiliwa shaka.
 
Ndiyo maana hatukushangazwa hata kidogo na Mbunge Shelukindo alipoibua kashfa hiyo bungeni na pia hatukushangazwa na kauli ya Waziri Mkuu Pinda alipokiri kuwa wizara hiyo ilitoa rushwa kwa baadhi ya wabunge na kusema Serikali ingemfukuza kazi Katibu Mkuu wa wizara hiyo, David Jairo ambaye ushahidi umeonyesha kwamba, hakika ndiye aliyechangisha fedha za kuwahonga wabunge ili bajeti ya wizara yake ipitishwe na Bunge.
 
Pamoja na ukweli kuwa kashfa hiyo ni nzito na ni moja ya kashfa za aina yake tangu nchi yetu ipate uhuru, bado tunampongeza Waziri Mkuu Pinda kwa kuwasikiliza wabunge waliotaka kiongozi huyo mtoa rushwa afukuzwe kazi. Kama ambavyo tumekuwa tukisema na kusisitiza mara kwa mara kupitia safu hii, unyenyekevu na usikivu wa kiongozi huyo siku zote umeepusha shari na kuleta maridhiano miongoni mwa makundi katika nchi yetu, likiwamo Bunge.
 
Tunachokisisitiza hapa ni kwamba, Serikali isiishie tu kumtoa kafara Katibu Mkuu huyo pekee wakati ukweli usiopingika unajulikana, kwa maana  kwamba mtoa rushwa huyo asingeweza kutenda kosa kubwa kama hilo pasipo kupata maelekezo na baraka za bosi wake, Waziri William Ngeleja. Ni aibu iliyoje kwa Serikali iliyo madarakani kwamba wizara inaweza kuziamuru taasisi zote zilizo chini yake zichange fedha za kutoa hongo ya kupitisha bajeti yake bungeni.
 
Sisi tumefadhaishwa na kusikitishwa na kashfa hiyo ambayo bila shaka imethibitisha kwamba, hakika ufisadi na rushwa vimejikita ndani ya Serikali. Tunamshauri Rais Jakaya Kikwete afanye maamuzi magumu kwa kuvunja Baraza la Mawaziri na kuwafukuza kazi Waziri Ngeleja na Katibu Mkuu wake, David Jairo. Tunadhani pia kwamba sasa Takukuru haitakuwa na kisingizio cha kutowafungulia mashtaka  wote waliohusika na kashfa hii, wakiwamo baadhi ya wabunge na watendaji wengine serikalini.


Mwananchi

No comments: