

Freddy Macha
Habari zilizotanda Uingereza wiki mbili zilizopita zimehusu gazeti maarufu la News Of The World. Lilifungwa wiki iliyopita baada ya mashtaka ya uhalifu. News of the World ilikuwa ikipata habari kwa kuingilia barua pepe na simu za watu maarufu ili kuwaiba.
Miongoni mwa waliokuwa wakifanyiwa wizi huo ni Malkia Elisabeth, mwanaye Prince Charles, Waziri Mkuu wa zamani Gordon Brown, viongozi mbalimbali na wacheza mpira mashuhuri.
Mwishoni gazeti liliwaudhi wananchi zaidi ilipofahamika lilikuwa limekita makucha yake kusikiliza habari za watu waliouliwa au kufa. Kati yao ni wasichana watatu waliouliwa kinyama Milly Dowler, Jessica Chapman, Holly Wells na ndugu za waliofariki Julai 2005 kutokana na mabomu ya magaidi mjini London.
Suala la kutafuta habari hata za maiti lilikuwa kilele cha uhalifu na gazeti lilifungwa na mwenyekiti wake Rupert Murdoch.
Bilionea Murdoch ni miongoni mwa watu wenye nguvu sana duniani. Alizaliwa Australia 1931 na kununua News of the World (na magazeti mengine, ikiwemo The Sun) mwaka 1969. Alianza shughuli za vyombo vya habari zaidi ya miaka 60 iliyopita. Ana mali bara Asia, Uingereza na Marekani.
Mwaka 1986 alianzisha runinga maarufu ya Marekani iitwayo Fox Broadcasting Corporation (FBS). Kitakwimu FOX na CBS ndizo runinga kubwa kuzidi zote Marekani. Mbali na The Sun, News of the World na Times hapa Uingereza alianzisha runinga maarufu ya Sky mwaka 1989.
Tajiri Murdoch anatawala pia vyombo vya habari bara Asia. Mwaka 1993 alinunua Star TV toka mfanyabiashara Richard Li aliyekuwa na matatizo ya kifedha kwa dola milioni moja. Star TV yenye makao makuu Hongkong ina nguvu kuzidi zote bara hilo, ingawa Wachina wamekuwa wakizuia nguvu zake. Pamoja na hayo mkewe Murdoch wa tatu pia ni Mchina (anaitwa Wendi Deng na alizaliwa mwaka 1968). Kifupi himaya yake inahesabika kuwa ya pili kwa utawala wa habari dunia nzima.
Mwananchi
No comments:
Post a Comment