.jpg)
Mohamed Banka
Uongozi wa klabu ya soka ya Simba hatimaye umesalimu amri kwa wachezaji, Mohamed Banka, Juma Jabu na Meshack Abel, ambao wamegoma kupelekwa kwa mkopo katika timu za Villa Squad, Moro United na Ruvu Shooting na sasa umewaita rasmi nyota hao kwa ajili ya kukaa nao chini ili kumaliza sintofahamu hiyo.
Awali, Mwenyekiti wa Simba, Ismail Aden Rage, alikaririwa akiwaambia wachezaji hao kwamba ni lazima wataenda katika timu walizopangiwa kwa sababu wao ni waajiriwa na mtumishi hawezi kuhoji anapohamishwa kituo cha kazi.
Kauli hiyo ya Rage ilifuatia kauli za wachezaji hao zilizotolewa kwa nyakati tofauti wakisema kwamba hawako tayari kupelekwa-pelekwa kama kuku anayebebwa bila ya kujua anaenda kuchinjwa mahala gani.
Na jana Shirikisho la Soka nchini (TFF), kupitia kwa mkurugenzi wake wa mashindano, Saad Kawemba, alikaririwa akisema kwamba wachezaji wana haki ya kukubali ama kukataa kupelekwa kwa mkopo katika klabu nyingine kwa sababu ni lazima pande tatu zinazohusika na uhamisho wa mchezaji (ambazo ni klabu anayotoka, klabu anayoenda na mchezaji mwenyewe) zisaini maridhiano ya kimaandishi kabla ya uhamisho kufanyika.
Kanuni za Shirikisho la Soka la Kimataifa (FIFA) kuhusiana na uhamisho wa wachezaji zinasisitiza umuhimu wa maridhiano ya pande hizo tatu kimaandishi, kupitia ibara ya 10, kifungu cha kwanza (toleo la 2010). Kwa mujibu wa FIFA, vyama vya soka vya nchi wanachama ni lazima vizingatie matakwa ya kanuni hii (Ibara ya 10) na kuitwaa kama ilivyo kwani ni moja ya ibara ambazo si ruhusa kuzifanyia marekebisho.
Hatimaye jana, Afisa Habari wa Simba, Ezekiel Kamwaga, aliiambia NIPASHE kuwa wamewaandikia wachezaji hao barua ya kuwaita kwa ajili ya kuzungumza nao ili kumaliza tatizo hilo leo.
"Tumewaandikia barua ya kuwaita ili kesho (leo) tukutane nao kwa ajili ya kuweka mambo sawa," alisema Kamwaga.
Wakati Simba wakianza mchakato wa kuzungumza na akina Banka kuhusu klabu walizowapeleka, imebainika kuwa hata baadhi ya timu zilizokopeshwa nyota hao hazina taarifa hizo.
Katibu wa Villa, Yasin Masoud, alisema kuwa wao hawajui lolote kuhusu ujio wa Banka na ndio maana hawajamjumuisha katika orodha ya wachezaji wao 28 waliowaombea usajili, wakiwemo 10 kutoka michuano ya Copa Coca Cola.
Alisema kuwa wao waliuandikia uongozi wa Simba wakiomba wapewe kwa mkopo wachezaji Mohamed Kijuso na Ali Ahmed 'Shiboli' aliyeenda Kagera Sugar, lakini hawakujibiwa na badala yake wakasikia wamepewa Banka.
"Ndio maana tunasema suala la Banka kwetu hatulijui," alisema Katibu huyo.
Katika hatua nyingine, Kamwaga alisema kocha wa Simba, Mganda Moses Basena atawasili nchini leo kuanza kukinoa kikosi chake kwa ajili ya msimu mpya wa ligi kuu ya Bara.
CHANZO: NIPASHE
No comments:
Post a Comment