ANGALIA LIVE NEWS

Monday, July 18, 2011

Zanzibar kwachafuka

Waziri wa Kilimo na Mali Asili wa Zanzibar, Mansour Yussuf Himid
Waziri wa Kilimo na Mali Asili wa Zanzibar, Mansour Yussuf Himid, ametakiwa kujiuzulu nyadhifa zake katika Chama Cha Mapinduzi (CCM) na Serikali, kutokana na msimamo wake wa kutetea muundo wa Serikali tatu katika mfumo wa Muungano wa Tanganyika na Zanzibar .

Madai ya kumtaka ajiuzulu yametolewa kupitia vipeperushi maalumu vilivyosambazwa katika Manispaa ya Mji wa Zanzibar na watu wanaodai kuwa ni makada wa CCM, zikiwa ni siku chache baada ya Waziri Mansour kueleza kuwa muundo wa Muungano wa serikali mbili ni butu wakati akichangia bajeti ya Wizara ya Ardhi, Makazi, Maji na Nishati katika kikao cha Baraza la Wawakilishi wiki iliyopita.
Kwa mujibu wa vipeperushi hivyo, kauli ya Waziri huyo inakwenda kinyume na sera na ilani ya uchaguzi ya CCM ambayo alishiriki kuijadili na kuipitisha kabla ya Uchaguzi Mkuu wa mwaka jana, akiwa Mjumbe wa Halmashauri Kuu ya Taifa (NEC).
Vipeperushi hivyo vimesema wanachama wa CCM wameshangazwa na hatua ya kutetea mfumo wa Serikali tatu katika Baraza la Wawakilishi wakati suala hilo alitakiwa kulieleza wakati wa kuijadili na kupitisha ilani ya uchaguzi.
"Wewe ni mjumbe wa Halmashauri Kuu ya Taifa ya CCM, mjumbe wa Kamati Maalumu ya Halmashauri Kuu ya Taifa Zanzibar, mjumbe wa Sekretarieti ya Kamati Maalumu ya NEC Zanzibar ukiongoza Idara ya Uchumi na Fedha, kwanini hukusema hayo katika vikao halali vya chama?” vilihoji vipeperushi hivyo.
Aidha, vipeperushi hivyo vimesema msimamo wa Waziri Mansour unalenga kuwavuruga wana CCM na kuzorotesha umoja wa kitaifa uliopo tangu kuasisiwa kwa Muungano mwaka 1964.
Maneno mengine yaliyoandikwa ni kuwa waziri huyo anafanya hivyo ili aonekane kuwa ni mtetezi wa Zanzibar wakati alipokuwa Waziri wa Ardhi, Nishati na Majenzi na Nyumba alifanya vitendo visivyo vya uadilifu.
Vipeperushi hivyo vinaendelea kusema kwamba : "Tunajua kuwa una haki ya kusema lolote ndani ya Baraza na kwa mujibu wa katiba unahifadhi kwa lolote utakalolisema kwenye Baraza. Lakini kwa hili la kukisaliti chama huna pakutokea,”vilieleza vipeperushi hivyo vilivyosambazwa katika maskani za CCM na Baraza za Msikitini Zanzibar.
Aidha, vipeperushi hivyo vilisema kumekuwepo na watu Zanzibar ambao wameamua kuzungumza lugha kali dhidi ya Muungano wakiwa na nia mbaya ya kuhakikisha Muungano unavunjika na wao wakimbilie nje ya nchi watumie fedha walizochuma kwa njia zisizokuwa mwafaka.
Vipeperushi hivyo vilisema kwamba hatua ya Waziri Mansour kutoa kauli inayokwenda kinyume na sera na ilani ya chama chake ni vizuri ajivue uwanachama na kujiunga na vyama vyenye sera za Serikali tatu.
"Sasa chagua moja kusuka au kunyoa rudi kwenye CUF (Chama cha Wananchi) yako utuachie CCM yetu tunataka uturudishie kadi yetu haraka," ni maneno mengine yaliyoandikwa katika vipeperushi hivyo. Hata hivyo, Waziri Mansour alipoulizwa kuhusiana na vipeperushi hivyo, alisema hana chochote cha kuzungumza.
"Siku hizi Zanzibar watu wana karatasi nyingi sana, mtu akizungumza kidogo tu tayari wameshamwaga vipeperushi, mimi sina la kuzungumza," alisema.
Naibu Katibu Mkuu wa CCM Zanzibar, Vuai Ali Vuai, alisema vikao ndivyo vitakavyoamua kuhusu suala hilo, kwa vile linahusu sera na ilani ya uchaguzi ya chama hicho.
"Miye nilianza kupokea malalamiko kutoka kwa wanachama Zanzibar nikiwa safarini Dodoma kuhusu kauli ya Waziri kutetea Serikali tatu, lakini siwezi kusema kama kafanya kosa au si kosa, vikao ndio vitakavyoamua,” alisema Vuai. Alisema suala hilo litajadiliwa katika vikao kama kutaonekana kuna makosa yatapatiwa ufunbuzi kulingana na taratibu za chama na kama kauli ya Waziri haitakuwa na makosa chama kina haki ya kumpongeza kwa ushauri wake.
Hata hivyo, alisema CCM kinaamini muundo wa Serikali mbili ndio mwafaka katika Muungano na ndio maana ilitetea muundo huo katika sera na ilani yake ya uchaguzi wa mwaka 2010.
"Hapa mpango wa Serikali moja hatutaki kuusikia mfumo huu butu wa Serikali mbili, sasa basi twende kwa jambo ambalo kila mmoja wetu analizungumza la Serikali tatu na mengineyo," alisema Mansour huku akipigiwa makofi na wajumbe wa CUF na baadhi wa CCM.
Hata hivyo Kamanda wa Polisi wa Mkoa wa Mjini Magharibi Unguja, Azizi Juma Mohammed, alisema jeshi lake bado halijapokea malalamiko yoyote kuhusu kushambuliwa kwa Waziri huyo kupitia vipeperushi hivyo.
"Polisi bado hatujaviona vipeperushi hivyo na iwapo tutavipata tutafanya uchunguzi," alisema. Waziri Mansour alitoa ushauri huo wa Serikali tatu baada ya kuibuka mjadala mkali ndani ya Baraza la Wawakilishi juu ya kuchelewa kuondolewa kwa suala la mafuta na gesi asilia katika orodha ya mambo ya Muungano.
CHANZO: NIPASHE

No comments: