.jpg)
Meneja Mawasiliano wa Shirika la Umeme (Tanesco), Badra Masoud
Vyanzo vinavyozalisha umeme kwa njia ya maji vimelazimika kuzalisha chini ya kiwango ili kuvinusuru visikauke kabla ya msimu wa mvua.
Akizungumza na waandishi wa habari waliotembelea bwawa la Mtera, Mhandisi Mkuu Uendeshaji, Julius Chomola, alisema hivi sasa bwawa hilo linazalisha MW 33 kutoka 80 za kawaida kutokana na kuendelea kupungua kwa kina cha maji.
Alisema kina cha maji kimeshuka kutoka mita za ujazo 698.50 hadi mita za ujazo 690.74, ambazo zikifikia mita 690, bwana litasimamisha uzalishaji.
Alisema uzalishaji unafanyika kwa saa kadhaa kuanzia saa 5:00 asubuhi hadi saa 8:00 mchana ambapo uzalishaji husimama na kuwashwa tena saa 1:00 usiku hadi saa 4:00 usiku.
“Tunajitahidi sana kwa nguvu zetu zote, maarifa na ujuzi tulionao kuzalisha umeme kwa kiasi hiki cha maji kilichopo ili tusimalize maji tuliyonayo na kusimamisha uzalishaji kabisa,” alisema Chomola.
Alisema wameweka mpango maalum wa uzalishaji ili Mtera iweze kuendelea kuzalisha hadi msimu wa mvua katika mikoa ya Mbeya na Iringa ambayo inaingiza maji katika mto Ruaha unaolisha bwawa hilo.
Meneja Mawasiliano wa Shirika la Umeme (Tanesco), Badra Masoud, alisema mtambo wa Kidatu unazalisha MW 40 kutoka uzalishaji wa kawaida wa MW 204, Kihansi ni MW 90 kutoka MW 180, Nyumba ya Mungu inatoa MW 3.5 kutoka MW 8 na New Pangani inazalisha MW 20 kutoka 68.
Alisema hivi sasa uzalishaji mkubwa unaotegemewa ni wa mitambo ya gesi ya Songas MW 182, Ubungo MW 100, Tegeta MW 45 na Symbion MW 70.
Kuhusu mtambo wa IPTL, Badra alisema hauzalishi kabisa.
CHANZO: NIPASHE
No comments:
Post a Comment